Rafiki yangu mpendwa,

Hakuna kitu chochote kikubwa ambacho kimewahi kufanya na mtu ambaye hana mapenzi ya kweli kwenye kile anachofanya. Kama unataka kufanikiwa kwenye maisha, kama unataka kufanya makubwa na kuacha alama hapa duniani, lazima kwanza upende kile ambacho unakifanya. Unapaswa kukipenda kweli kiasi kwamba upo tayari kujitoa kwa ajili ya kitu hicho.

Hivi ndivyo watu wote tunaowaona wana mafanikio makubwa wameweza kufikia mafanikio hayo. Wengi walipokuwa wanaanza walikatishwa tamaa na wengine, walikutana na mambo magumu, changamoto na hata kushindwa. Lakini hawakukata tamaa, kwa sababu ni kitu ambacho walikipenda kweli, kitu ambacho kilitoka ndani yao.

Mwandishi Keith Abraham kupitia kitabu chake kinachoitwa IT STARTS WITH PASSION; Do What You Love and Love What You Do, anatufundisha umuhimu wa kufanya kile tunachopenda au kupenda kile tunachofanya. Njia pekee ya sisi kufanikiwa ni kujua kile ambacho tunakipenda kweli na kisha kukifanya au kama hatutajua kipi tunapenda, basi kile ambacho tunakifanya sasa tunapaswa kukipenda sana.

Kwenye kitabu chake, Keith anatuambia kama unataka kupata zaidi ya unachopata sasa, kama unataka kuwa zaidi ya ulivyo sasa, basi lazima upende sana kile unachokifanya. Upendo una nguvu kubwa sana, nguvu ya kuvunja kila aina ya kikwazo na changamoto, nguvu ya kukuwezesha kuendelea hata pale unapokuwa umechoka na kukaribia kukata tamaa.

passion.png

Kwenye kitabu chake, Keith ametushirikisha maeneo manne ambayo tunapaswa kuyazingatia katika kutengeneza maisha ambayo tunayapenda, tunapenda kile tunachofanya na tunafikia mafanikio makubwa. Kwenye makala hii ya juma tunakwenda kuyaangalia maeneo hayo manne, na hatua tunazopaswa kuchukua kwenye kila eneo ili tuweze kuwa na maisha bora. kwenye makala ya TANO ZA JUMA (ambayo inapatikana kwenye telegram tu) tutachambua kila eneo kwa kina na kujifunza hatua kwa hatua jinsi unavyoweza kufikia mafanikio makubwa kupitia chochote unachochagua kufanya.

MAENEO MANNE YA KUTENGENEZA MAISHA UNAYOYAPENDA NA YENYE MAFANIKIO MAKUBWA.

ENEO LA KWANZA; MAANA – JINSI YA KUTENGENEZA UHAKIKA KWENYE MAISHA YAKO.

Kila mtu anapenda kuwa na maana kwenye kitu anachofanya kwenye maisha yake, kazi na hata biashara. Japokuwa wengi wanafanya kazi wanazofanya ili walipwe, lakini kinachowafanya waridhike na kazi hizo siyo malipo wanayoyapata, bali maana wanayoipata kupitia kile wanachofanya.

Tunapaswa kujua uhusiano uliopo baina ya kusudi la maisha yetu, kile tunachopenda kufanya na malengo ambayo tumejiwekea. Vitu hivi vitatu, yaani kusudi, mapenzi na malengo ndiyo vinatengeneza maana kwenye maisha yetu.

Tunapokuwa na kusudi kwenye maisha, na tukapenda kile tunachofanya na kisha kuwa na malengo ambayo tunayafanyia kazi, maisha yetu yanakuwa na maana kubwa na tutapata msukumo wa kujituma zaidi ili kufanikiwa.

Maana inaanza na KWA NINI unafanya kile unachofanya. Kuna maswali matatu unayopaswa kuyajibu kupitia kile unachofanya. Maswali hayo ni KWA NINI (WHY), NINI (WHAT) na VIPI (HOW). Kwa nini inakufanya ujue msukumo ulionao kwenye kile unachofanya. NINI unafanya hapa ndiyo unachagua kile unachofanya na VIPI unavyofanya kitu hicho unaelezea hatua unazochukua katika kufanya kitu hicho.

HATUA YA KUCHUKUA; Tengeneza maana kupitia kila unachofanya kwa kujua kusudi la maisha yako, kujua kwa nini unafanya chochote unachofanya, kupenda kile unachofanya na kisha kujiwekea malengo ya kupiga hatua zaidi kupitia hicho unachofanya.

SOMA; USHAURI; Hatua Za Kuchukua Kama Bado Hujalijua Kusudi La Maisha Yako.

ENEO LA PILI; HATUA – JINSI YA KUPATA UWAZI KWENYE MAISHA YAKO.

Baada ya kujua kusudi la maisha yako na kujiwekea malengo ambayo unayafanyia kazi, unapaswa kuwa na njia ya kujipima jinsi unavyoyafanyia kazi malengo hayo. Kwa sababu unapoweka malengo, unaiona ile picha ya mwisho, lakini zile hatua ambazo unachukua mpaka kufikia picha hiyo ya mwisho hazionekani.

Hivyo eneo la pili tunalopaswa kulifanyia kazi ni zile hatua ambazo tunapaswa kupiga ili kufika kule ambapo tunataka kufika, ili kuweza kukamilisha kusudi la maisha yetu, ili maisha yetu yaweze kuwa na maana.

Kwenye kila ndoto kubwa tuliyonayo, tunapaswa kuivunja kwenye vipande vidogo vidogo na kisha kuchukua hatua kwenye vipande hivyo. Vipande hivi vidogo vidogo ndiyo vinatupa uwazi kwenye safari yetu ya mafanikio. Kwa sababu kama huwezi kupima kitu, huwezi kukielewa wala kukikuza. Vipande vidogo tunavyogawa tunaweza kuvipima na hivyo kujua kama tunafanya vizuri au vibaya.

Njia ambayo watu wengi wamekuwa wanatumia kuweka malengo ni kuanza kuchukua hatua, kufikiri jinsi ambavyo watachukua hatua hizi na kupata hisia pale ambapo mtu anakamilisha lengo hilo. Njia hii imekuwa inawafanya wengi kuishia njiani. Mwandishi anatushirikisha njia sahihi ya kujiwekea malengo na kuyafikia, ambayo inaanza na zile hisia ambazo tunataka kuwa nazo pale tunapofikia malengo hayo, kufikiria hatua za kuchukua na kisha kuchukua hatua ili kufikia malengo hayo. Unapoanza na hisia, unapata msukumo mkubwa wa kufikia malengo yako.

HATUA YA KUCHUKUA; Chukua lengo au ndoto kubwa uliyonayo, kisha gawa kwenye vipande vidogo, tengeneza hisia ambazo utakuwa nazo baada ya kufikia lengo hilo, kisha anza nazo. Jua hatua unazopaswa kuchukua kisha anza kuchukua hatua hizo huku ukiwa tayari una hisia za ushindi. Angalia zile hatua unazochukua katika kukamilisha vipande vidogo vya lengo lako kubwa. Kadiri unavyokamilisha, ndivyo unavyopata uwazi na kujiamini zaidi, kitu kinachokusukuma kuchukua hatua zaidi.

ENEO LA TATU; MTAZAMO – JINSI YA KUONGEZA KUJIAMINI KWENYE MAISHA YAKO.

Kila mtu ana uwezo mkubwa sana ndani yake, uwezo wa kufanya makubwa kwenye maisha. Lakini wengi wamekuwa wanashindwa kutumia uwezo huu mkubwa ulio ndani yao kwa sababu hawajiamini. Kutokujiamini kimekuwa kikwazo kwa wengi kufanikiwa kwenye maisha.

Kila mtu anajua nini anataka kwenye maisha na anazijua hatua za kuchukua ili kupata kile anachotaka. Lakini inapofika kwenye kuchukua hatua, wengi hukwama, kwa sababu hofu ya kushindwa na ugumu wa safari unawafanya wengi kusita kuanza. Maneno ya kukatisha tamaa kutoka kwa wengine na hata hadithi za wale walioshindwa ndiyo zinazidi kuwarudisha nyuma wengi.

Ili kufanikiwa, lazima uanze kwa kujiamini wewe mwenyewe, lazima uwe mfano wa mtu mwenye uhakika, mwenye kujua wapi anakwenda na kuamini ana uwezo ndani yake wa kufikia malengo aliyojiwekea.

Hilo linawezekana kupitia mtazamo ambao mtu unakuwa umejijengea, mtazamo wa kwamba inawezekana, mtazamo wa kwamba unaweza. Kadiri unavyojijengea mtazamo huu, ndivyo unavyokuwa imara na kuweza kuchukua hatua kubwa kufikia malengo yako.

Ukishajiwekea malengo, unapaswa kuwa na uhakika kwamba utayafikia, unapaswa kuondokana na wasiwasi wowote unaoweza kuwa umejijengea na kuchukua hatua ukiwa unajiamini kwamba utafikia malengo hayo.

HATUA YA KUCHUKUA; Jijengee kujiamini, jua kwamba ndani yako una uwezo mkubwa ni wewe kuanza kuutumia uwezo huo. Unapoweka malengo, amini utayafikia na hakuna kinachoweza kukuzuia, kisha chukua hatua kwa kujiamini na ondokana na wasiwasi wowote unaoweza kuwa nao.

SOMA; Kwa Nini Masikini Wanazidi Kuwa Masikini Na Matajiri Wanazidi Kutajirika…

ENEO LA NNE; MWENDO – JINSI YA KUISHI MAISHA YENYE MSIMAMO.

Hamasa huwa haidumu kwa muda mrefu, na ndiyo maana watu ambao wanaishi kwa hamasa hawana msimamo. Huwa wanaanza jambo baada ya kuwa wamepata hamasa, na hamasa hiyo inapoisha wanaacha jambo hilo. Wakipata hamasa nyingine wanaanza jambo jingine jipya. Hivyo unakuta watu hawa wanaanza na kuacha mambo mengi na hakuna hata moja ambalo wamekamilisha.

Ili kufanikiwa, unapaswa kutengeneza mwendo kwenye maisha yako, kuwa na msimamo wa kuchukua hatua kwenye jambo moja mpaka upate matokeo unayoyataka. Kuacha kutegemea hamasa pekee na kuwa na mpango wa utekelezaji utakaokuwezesha kufanyia kazi malengo yako mpaka kuyafikia.

Njia pekee ya kutengeneza mwendo na kujijengea msimamo kwenye maisha yako ni kuchagua kuchukua hatua ndogo ndogo kila siku kufikia malengo yako. Hatua ndogo kabisa ambazo huwezi kuona ugumu kuzichukua. Kwa kufanya hivyo kila siku, unatengeneza tabia ambayo inakusukuma kuendelea kufanya.

Usisubiri mpaka uweze kuchukua hatua kubwa kwa wakati mmoja. Usiwe mtu wa kusubiri mpaka kila kitu kiwe tayari ndiyo uanze. Ukishajua nini unataka, ukishaweka malengo, basi anza kuchukua hatua ndogo ndogo kila siku kuelekea kwenye malengo hayo. Mpango mzuri ambao unaufanyia kazi leo ni bora kuliko mpango bora ambao unasubiri mpaka kesho.

Unapotengeneza mwendo kwenye maisha yako, inakuwa rahisi kuendelea kuliko kuanza. Hivyo hakikisha kila siku kuna hatua unachukua kuelekea kwenye lengo lako.

HATUA YA KUCHUKUA; Usitegemee hamasa ya mara moja kufanya mambo makuba, badala yake chukua hatua ndogo ndogo kila siku, hizi zitakujengea mwendo ambao utakusukuma kuendelea kuchukua hatua zaidi. Kila siku piga hatua kuelekea kwenye malengo yako, na utajikuta unayafikia bila ya kujua.

Rafiki, hayo ndiyo maeneo manne ya kuzingatia katika kujenga maisha unayoyapenda na yenye mafanikio makubwa. Kwenye makala ya TANO ZA JUMA tutajifunza kwa kina kile eneo na hatua muhimu zaidi za kuchukua ili kuwa na maisha yenye mafanikio makubwa, maisha ambayo unayapenda na yenye maana kwako na kwa wengine pia. Makala ya TANO ZA JUMA itapatikana kwenye channel ya TELEGRAM, ili kuipata makala hiyo, kitabu na #MAKINIKIA, jiunge na channel hiyo, maelezo yako hapo chini.

#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI.

Rafiki yangu mpenda, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.

Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.

Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu