“When you are distressed by an external thing, it’s not the thing itself that troubles you, but only your judgment of it. And you can wipe this out at a moment’s notice.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 8.47
Shukrani ndiyo namna pekee ya kuipokea zawadi hii ya siku mpya tuliyoiona leo.
Na njia bora ya kushukuru ni kuitumia siku hii vizuri, kuiishi siku hii kwa ukamilifu na siyo kuipoteza kama ambavyo tumekuwa tunafanya kwa siku nyingine.
Tuweke vipaumbele sahihi na kuvifanyia kazi.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.
Asubuhi ya leo tutafakari KINACHOKUSUMBUA SIYO KINACHOTOKEA…
Kuna vitu vingi ambavyo vinatokea kwenye maisha yetu, vingine tulitegemea na vingine hatukutegemea.
Katika vile ambavyo hatukutegemea, kuna ambavyo tunaona ni vizuri na vingine tunaona ni vibaya.
Huwa tunaruhusu vitu hivi vilivyotokea kutuvuruga kwenye maisha yetu, tunaona mipango yetu haiwezekani tena.
Lakini ukweli ni huu, kinachokusumbua wewe siyo kinachotokea, basi tafsiri yako kwenye kile kilichotokea.
Mambo huwa yanatokea, kwa mipango yao yenyewe na siyo kwa kuangalia wewe umepanga nini.
Jinsi unavyopokea na kutafsiri yaliyotokea ndiyo kunakokusumbua.
Kama utaona yaliyotokea ni mabaya basi utasumbuka.
Njia bora ya kuwa na maisha tulivu ni kupokea kila kinachotokea kwa mtazamo chanya na kutumia kama njia ya wewe kufika kule unakotaka kufika.
Usihukumu chochote kinachotokea kama ni kizuri au kibaya, bali kichukulie kama njia ya wewe kufika unakotaka.
Ukibadili mtazamo wako kwa namna hii, hutasumbuka na chochote kile na utaweza kutumia kila unachokutana nacho kama njia ya kufanikiwa zaidi.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kutosumbuka na yale yanayotokea, badala yake kuyapokea na kuyatumia kufika kule unakotaka kufika.
#TatizoNiTafsiriYako #UsihukumuKinachotokea #TumiaKilaKinachotokeaKwaManufaaKwako
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1