Maisha ni mchezo, na kwenye huo mchezo kuna ambao wanashinda na wapo wengi ambao wanashindwa.
Kushinda au kushindwa kwenye mchezo huu wa maisha kunategemea sana jinsi ambavyo umezielewa sheria za mchezo huo na kuzizingatia.
Lakini pia ipo njia ya uhakika ya kushinda kwenye huu mchezo wa maisha, ambayo wengi hawaijui wala hawaitumii.
Njia hiyo ni kutengeneza mchezo wako mwenyewe na kuanzia kileleni.
Iko hivi rafiki, unapoingia na kushindana kwenye mchezo ambao wengine wameanzisha, unakwenda kushindwa, kwa sababu wao wanaujua zaidi mchezo huo kuliko wewe.
Hivyo kama unataka ushindi wa uhakika, tengeneza mchezo wako mwenyewe, ambao wewe unauelewa kwa undani, na yeyote atakayekuja kushindana na wewe kwenye mchezo wako, unampoteza kabisa.
Unaweza kutumia dhana hii ya kutengeneza mchezo mpya kwenye kila eneo la maisha yako.
Kwa mfano kwenye biashara, badala ya kuingia kwenye biashara ambayo tayari wengine wanafanya, anzisha biashara ya tofauti kabisa na wengine. Tengeneza aina mpya ya biashara, ambayo ina namna ya tofauti na bora kabisa ya kutatua changamoto za wateja na kutimiza mahitaji yao. Kwa namna hii, wateja watakuja kwako zaidi na hapo utaweza kuwageuza kuwa wateja wa maisha kwa kuwahudumia vizuri.
Kama mtu mwingine atajaribu kuingia kwenye aina hiyo ya biashara unayofanya, unaweza kumpoteza kabisa kwa sababu wewe una uelewa mkubwa kwenye biashara hiyo kuliko yeye.
Angalia ni maeneo yapi ya maisha yako ambayo unahitaji kupata ushindi mkubwa, kisha angalia ni mchezo wa aina gani unaocheza. Kama ni mchezo ambao wengine wanacheza, jua upo kwenye mchezo mbaya kwako. Kaa chini na tengeneza mchezo mpya kwako na hapo utakuwa na uhakika wa kushinda.
Tengeneza mchezo wako, ambao unazijua kanuni na sheria zake na kisha ucheze kwa viwango vya juu sana, yeyote atakayekuja kuleta ushindani, unampoteza kabisa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,