Watu wote wanaojaribu kitu mara moja kisha wanaacha kwa sababu hawajapata matokeo waliyotegemea kupata wamekuwa wanajidanganya.
Anza na wewe mwenyewe, je umewahi kununua kitu baada ya kukutana nacho kwa mara ya kwanza? Umewahi kumwamini mtu kwa mara ya kwanza anakuambia kitu? Majibu ni hapana, inakuchukua muda mpaka umwamini na kumwelewa mtu na kisha kukubaliana naye.
Ndiyo binadamu tulivyo, huwa inatuchukua muda kidogo kuelewa na kukubaliana na vitu.
Hivyo unapoanza kitu chochote kipya, jua kabisa hakuna atakayekuelewa kwa mara ya kwanza, hata ya pili na hata ya tatu. Hivyo unahitaji kuwa king’ang’anizi, unahitaji kujiamini na kuimamia kweli kile unachoamini. Kama mtu bado hajakubaliana na wewe basi jua bado hajakuelewa, hivyo una kazi zaidi ya kumwelewesha na kumshawishi.
Watu huwa hawafanyi vitu kwa mara ya kwanza wanapokutana navyo, hivyo ni wajibu wako kujiweka kwenye akili na fikra za watu kwa muda mrefu kabla hawajakubaliana na wewe.
Kwa wale wanaotangaza biashara zao, usijidanganye kwamba ukitangaza mara moja inatosha. Usiyaone makampuni makubwa yanarudia tangazo lile lile kwenye tv au redio kila siku na ukasema hawa wanapoteza muda. Wanaijua saikolojia ya watu, huwa hawaamini kitu mara moja, ni mpaka kitu kijirudie rudie ndiyo wanakielewa, wanakiamini na kuchukua hatua. Hivyo kama unatangaza biashara yako, huo unapaswa kuwa mwendelezo na siyo kitu cha kujaribu mara moja na kuacha kama huoni matokeo mazuri.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,