Rafiki yangu mpendwa,
Unazikumbuka zile hadithi za utotoni, zile hadithi ambazo zinaanza na mtu akiwa kwenye mazingira fulani magumu, anayashinda na hadithi inamalizia kwa kusema; wakaishi kwa raha mustarehe maisha yao yote!
Rafiki, leo nina habari za kusikitisha kidogo kwako, hicho kitu hakipo, hakuna namna ukaishi kwa raha mustarehe maisha yako yote.
Kutafuta furaha imekuwa ndiyo nguzo kuu ya biashara nyingi hapa duniani. Fikiria biashara zote za burudani na sanaa, zote ni njia ya kuwapa watu furaha. Fikiria biashara za vilevi mbalimbali, yote ni kutaka kuwasahaulisha watu shida zao na kuwapa furaha, japo inakuwa kwa muda mfupi.
Na hata simu janja na mitandao ya kijamii ambayo imepata umaarufu mkubwa sasa, yote ni kwa sababu imekuwa sehemu ya kuwapa watu raha, japo pia ni kwa muda mfupi.
Rafiki, dhana kwamba utakuwa na furaha ya kudumu maisha yako yote ni ya uongo. Hakuna kitu kama hicho, hakuna mtu anayeweza kuwa na furaha inayodumu muda wote, hata angekuwa nani.
Kila mmoja wetu huwa anapata furaha kwa muda mfupi, halafu baada ya hapo anarudi kwenye hali ya kutokuwa na furaha au kutokuridhika, na hiyo inamsukuma kutafuta furaha zaidi. Sasa wale wanaojua dhana hii wanaitumia vizuri, lakini wasioijua wanaishia kuwa wateja na walevi wa vitu vinavyoleta raha ya muda mfupi.
Leo na kwenda kukushirikisha sababu nne kwa nini huwezi kuwa na furaha ya kudumu kwenye maisha yako, na kisha nitakuonesha kwa nini hilo ni zuri sana kwako. Ukimaliza kusoma makala hii, utaondoka ukiwa na mtazamo sahihi kuhusu furaha na hutakuwa na tamaa wala kutumbukia kwenye ulevi wa kitu chochote kile.
Mwandishi Nir Eyal kwenye kitabu chake kinachoitwa INDISTRACTIBLE, ameeleza moja ya sababu zinazopelekea wengi kusumbuka na teknolojia ni kushindwa kudhibiti vichocheo vya ndani vinavyowasukuma kutafuta usumbufu. Na moja ya vichocheo hivyo ni kutaka kupata furaha.
Ili uweze kudhibiti vichocheo vya ndani, hasa hali ya kutafuta furaha, ni muhimu kujua sababu nne zinazopelekea furaha isiwe ya kudumu, ambazo tunakwenda kujifunza hapa.
MOJA; UCHOSHI.
Uchoshi ndiyo sababu ya kwanza kwa nini hatuwezi kuwa na furaha ya kudumu. Sisi binadamu huwa tuna tabia ya kuchoshwa na kitu ambacho tumeshakizoea kwenye maisha yetu. Hivyo huwa tunatafuta njia ya kufanya au kuwa na kitu cha tofauti.
Huwa hatupendi kukaa bila ya kuwa na kitu cha kufanya, hivyo huwa tunajikuta tunafanya chochote, hata kama ni kibaya, ili tu kubadili hali tuliyonayo. Watu wengi hujikuta wamenunua kitu au wameingia kwenye ulevi kwa sababu hawana kitu cha kufanya kwa wakati huo.
MBILI; UPENDELEO HASI.
Ukiamka asubuhi na ukawa una maumivu makali sana ya kichwa, hutaanza kufikiria kwamba ni uchovu wa siku iliyopita, badala yake utaanza kufikiria kwamba una ugonjwa mkubwa sana, labda uvimbe kichwani. Hilo litakusukuma kwenda kupata huduma ya afya haraka.
Hivi ndivyo binadamu tulivyo, huwa tuna tabia ya kuyapa uzito sana matukio hasi kuliko matukio ambayo ni chanya. Kwa jambo lolote linalotokea, huwa tunaegemea zaidi upande hasi kuliko upande chanya. Hivyo mtu anaweza kukutana na kitu kizuri, badala ya kufikiria uzuri wa kitu hicho, anafikiria vipi kama atakipoteza. Na hilo ndiyo linasababisha furaha yoyote tuliyonayo isidumu.
TATU; ULINGANISHO HASI.
Mtu anaweza kuanzia chini kabia, akaweka juhudi akapata mafanikio fulani, lakini asifurahie mafanikio hayo, kwa sababu kila mafanikio anayopata, anagundua kwamba wengine wako hatua za juu zaidi. Mfano mtu ambaye amekuwa anatembea kwa mguu na kuota siku moja akiwa na baiskeli maisha yake yatakuwa mazuri, anapopata baiskeli anagundua inamhitaji nguvu kuchochea, anaona wengine wenye pikipiki wakiendesha bila ya kutegemea nguvu zao binafsi na hapo anaanza kutamani pikipiki. Akipata pikipiki anaanza kujilinganisha na wenye magari, na hali inakwenda hivyo.
Furaha tunayoipata kwa chochote tunachopata huwa haidumu kwa sababu huwa tuna tabia ya kujilinganisha na wengine, na pale wengine wanapokuwa wamepiga hatua zaidi, tunaona hakuna hatua tuliyopiga.
NNE; KUZOEA HALI MPYA.
Tunaweza kuwa na malengo makubwa, tukaweka juhudi kubwa sana, halafu tukayafikia. Tunakuwa na furaha kubwa sana baada ya kufikia malengo hayo, lakini muda mfupi baadaye tunazoea hali hiyo mpya na hivyo haitupi tena furaha. Hii ndiyo sababu watu wengi wamekuwa wanasema utajiri hauleti furaha, kwa sababu wanaanza wakiwa masikini na kufikiria wakipata utajiri watakuwa na furaha, wanaupata utajiri lakini baadaye wanauzoea, wanaona hakuna jipya, hivyo inawabidi watafute tena vitu vingine.
Hii ni hali ya kawaida kwetu binadamu, baada ya kupata kitu kipya, furaha yetu huwa inaongezeka kidogo na kisha kurudi kwenye hali yake ya zamani, wakati mwingine chini zaidi. Mfano watu wanaoshinda bahati nasibu, huwa wanakuwa na furaha sana mwanzoni, lakini baada ya muda wanajikuta wamerudi kwenye hali yao ya awali, na wengine wanashuka chini zaidi, kwa viwango vya furaha.
Rafiki, hali hizi nne tunakutana nazo kila siku, umekaa mahali huna cha kufanya badala ya kukaa utulie, uchoshi unakusukuma kuchukua simu yako na uangalie mitandao ya kijamii, ukiwa kwenye mitandao hiyo unakutana na habari hasi, labda msanii amefumaniwa, unasukumwa kuiangalia hiyo zaidi, wakati unaendelea kuangalia mitandao hiyo unaona rafiki yako ana gari jipya, unajilinganisha naye na kujiona wewe umeachwa nyuma, unaendelea kuperuzi lakini mwisho unajikuta huna raha uliyotegemea ungeipata kwa kuangalia mitandao hiyo, raha yoyote ambayo uliipata inakuwa imeisha baada ya kuizoea hali mpya.
Kwa nini hali ya kutokuwa na furaha muda wote ina manufaa kwetu?
Hebu fikiria kama ungekuwa na furaha na kuridhika na mpenzi wa kwanza uliyekutana naye, au kazi ya kwanza kufanya au biashara ya kwanza kufanya? Je ungeuwa hapo ulipo leo?
Hali ya kutokuwa na furaha ya kudumu ndiyo inatusukuma sisi binadamu kupiga hatua zaidi. Unapoweka malengo yako na ukayafikia, na kugundua hayakupi furaha, unaweka malengo makubwa zaidi, na hivyo kupiga hatua zaidi.
Bila ya sisi binadamu kuwa na hali ya kukosa furaha na kutokuridhika, tungeshapotea kabisa hapa duniani. Kinachotusukuma kuwa bora zaidi ni hali ya kutaka furaha, ambayo huwa haidumu.
Maendeleo yote yanayofanyika hapa duniani, msukumo mkubwa ni watu kupata furaha. Hivyo hali ya kutokuwa na furaha ya kudumu ina manufaa makubwa sana kwetu.
Muhimu ni wewe uweze kujua kwamba kukosa furaha kwa nyakati fulani siyo kwamba maisha yako hayafai, ni hali ya kawaida. Hivyo badala ya kutumia njia mbaya kutafuta furaha kama ulevi na mengineyo, tumia njia sahihi ambazo zinakuwezesha kupiga hatua zaidi.
Kupata kitabu cha INDISTRACTIBLE pamoja na uchambuzi wake wa kina, karibu kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA, kujiunga fungua www.t.me/somavitabutanzania
Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.
Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania