Nimekuwa nasema kama huna njia bora ya kujifunza kanuni za mafanikio, kama huna watu wazuri unaoweza kuwaiga na wakawa mamenta kwako, basi una mwalimu mzuri ambaye uko naye popote pale ulipo.

Mwalimu huyo ni asili, huyu ni mwalimu mzuri sana kwako kujifunza kanuni za mafanikio, na ukiweza kuzifuata kama asili inavyofanya, utaweza kufanikiwa sana, bila ya kujali uko wapi au unafanya nini.

Labda tuanze na mifano michache ili tuweze kuelewana;

Ukipanda mbegu ya mchicha leo na mbegu ya mbuyu, ni ipi itakayoanza kuchomoza? Jibu lipo wazi, ni mbegu ya mchicha, ya mbuyu itachelewa mno. Lakini ondoka na urudi miaka mitano baadaye, kati ya mbegu ya mchicha na ya mbuyu uliyopanga, ni mmea upi utakaoendelea kuwepo? Jibu lipo wazi, mchicha utakuwa umeshasahaulika wakati mbuyu ndiyo unaanza kutoa matunda. Hapa tunajifunza kwamba vitu vinavyokua haraka hupotea haraka pia, vitu vinavyokua taratibu vinadumu.

Kila siku tunaona jua linachomoza na kuzama, mwezi unakuwa mchanga, unakomaa, unapotea na kurudi tena, kila siku na kwa nyakati zile zile. Hii ni kwa sababu dunia inajizungusha kwenye mhimili wake na wakati huo huo inalizunguka jua. Haiachi hata siku moja na ndiyo maana maisha yanaendelea hapa duniani. Lakini wewe unataka ujaribu kitu siku chache na uone matokeo, usipoyaona unaacha kufanya. Huwezi kufanikiwa kama hufanyi kitu unachotaka kufanikiwa kila siku.

Dunia inaenda na mambo yake, haijali wewe unaona ni sawa au siyo sawa, haijali kama wewe upo katika hali nzuri au mbaya. Hebu fikiria kama dunia ingekuwa inasikiliza maoni ya watu, ingefanya nini? Maana wewe unaweza kuwa na mazao yako umepanda, unataka mvua inyeshe, jirani yako kuna ujenzi anafanya, hataki mvua inyeshe, sasa fikiria hapo dunia inataka kuwasikiliza wote, itafanya nini? Ni vigumu sana kwa dunia kufanya maamuzi kama ingekuwa inasikiliza kila mtu. Badala yake haimsikilizi yeyote, bali inafanya mambo yake. Na sisi ndiyo tunaangalia tutaendaje na yale yanayotokea, kama mvua hainyeshi na tunataka mvua tunatafuta namna mbadala. Hivyo ndivyo unavyopaswa kuwa kama unataka kufanikiwa, kuacha kumsikiliza kila mtu, kwa sababu maoni ya watu yanapingana, wapo watakaokuambia fanya hivi, wengine usifanye hivyo. Wewe fanya kile ambacho kwako ni sahihi na usibabaishwe na yeyote.

Asili ni mwalimu mzuri, kuna mengi ya kujifunza kwa namna asili inafanya mambo yake, kuwa mwanafunzi wa asili na utajifunza misingi bora sana ya mafanikio kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha