Kuna hatua moja ambayo inaweza kuibadili biashara yoyote ile.

Hatua hiyo ni kuongeza wateja zaidi kwenye biashara hiyo.

Kila biashara ina ukomo wake kwenye wateja, kuna watu ambao wangeweza kunufaika na biashara hiyo, lakini hawajui uwepo wa biashara hiyo.

Hivyo kama biashara itawekeza kwenye masoko, ikaweza kuwafikia wateja wengi zaidi ya waliopo sasa, itaweza kufanikiwa zaidi ya pale ilipo sasa.

Lakini kwenye hilo la wateja pia kuna changamoto, biashara nyingi zimekuwa zinakumbatia kila aina ya mteja, kinachotokea biashara inakuwa na wateja wengi, lakini hawana manufaa.

Hivyo suluhisho ni kutafuta wateja bora, wateja ambao wana maumivu kweli na wapo tayari kutatua maumivu hayo kupitia biashara yako.

Kitu cha kwanza unachopaswa kujua ni kwamba wateja hawa hawawezi kuwa kila mtu. Unapolenga kila mtu awe mteja wako, ndiyo unabeba wateja wengi ambao hawakufai, wanakusumbua na siyo makini.

Lengo lako linapaswa kuwa kupata wateja bora, wateja ambao wanaielewa thamani ya biashara yako na wapo tayari kuigharamia. Wateja ambao unapenda kuwahudumia kweli kutoka ndani yako.

Hapa unaepuka wateja wasumbufu, wanaotaka kunufaika zaidi kwa kulipa kidogo, wasiokuwa tayari kulipa kwa wakati, wanaotaka punguzo au vitu vya bei rahisi na wasiokuwa makini na kile unachotoa.

Pata wateja bora na anza kwa kueleza sifa za wateja bora kwa biashara yako. Kisha nenda kawatafute wateja hao bora kwa biashara yako.

Hakuna biashara ambayo haiwezi kunufaika kwa kuwa na wateja bora zaidi, hivyo weka juhudi kwenye hilo na utaiona biashara yako ikikua zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha