“If someone is slipping up, kindly correct them and point out what they missed. But if you can’t, blame yourself—or no one.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 10.4

Kuiona siku hii mpya ya leo ni jambo la kushukuru sana.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.

Asubuhi ya leo tutafakari TATIZO SIYO WAO, TATIZO NI WEWE…
Ni rahisi kuwalaumu wale wanaokosea au wasiofanya kama ambavyo tunategemea.
Tukiamini kwamba tatizo kubwa liko kwao, na sisi hatuna tatizo kabisa.
Lakini hii siyo kweli, kama kuna watu wanaokuhusu, halafu wanakosea au hawafanyi kama ambavyo ulitegemea wafanye, tatizo siyo wao, bali tatizo ni wewe.
Tatizo ni wewe kwa sababu hujawapa maelekezo sahihi au kuwarekebisha pale wanapokosea.
Tatizo ni wewe kwa sababu hujawaonesha sababu sahihi ya wao kufanya kile ambacho unawataka wafanye.

Kama unafanya biashara na wateja hawanunui kama ulivyotarajia, tatizo siyo wateja, bali tatizo ni wewe. Hujawapa sababu ya kutosha kuwasukuma kununua kwako na siyo kwa wengine.
Kama una watu waliopo chini ya uangalizinna usimamizi wako, labda wafanyakazi au watu wengine wa karibu, halafu hawafanyi kana ulivyotegemea wafanye, tatizo siyo wao, bali tatizo ni wewe. Hujawapa maelekezo sahihi ya namna ya kufanya, na hata kama unewapa, hujawapa sababu yenye msukumo mkubwa kwao kufanya.

Unapokubali tatizo ni wewe, unaona njia bora za kuwawezesha watu kufanya kile ambacho ulitegemea wafanye. Lakini unapoona tatizo siyo wewe bali wao, unaziba kabisa kila nafasi ya kuweza kuwa na ushawishi kwa watu hao.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kukubali jukumu la wale ambao wanahusika na wewe moja kwa moja, kukubali kwamba kama wanakosea au hawafanyi vizuri, tatizo siyo wao, bali tatizo ni wewe mwenyewe. Na hapo utakuwa na hatua sahihi za kuchukua.
#UsikimbieTatizo #WengiHawapendiKukosea #WapeWatuMaelekezoSahihi

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1