Mpendwa rafiki yangu,
Watu wengi hawayathamini maisha yao ndiyo maana kila siku watu wanaingia kwenye migogoro ya nafsi zao. Kama ingekuwa watu wanayathimini maisha yao wangepata wapi muda wa kujifananisha na wengine?
Wangepata wapi muda wa kuwachukia wengine bila sababu?
Sisi ndiyo mawakili wakubwa wa maisha yetu, jinsi maisha yetu yalivyo basi sisi ndiyo tumeyatetea kuwa hivyo na wala siyo mtu mwingine. Nabii mkubwa wa maisha yako ni wewe mwenyewe na siyo hao wengine unaowafikiria kwa sababu wewe ndiyo unajua kile unachotaka kwenye maisha yako.
Ziko hisia mbili zenye madhara makubwa mno ambazo ni hisia za chuki na wivu.
Hapa kuna kazi kubwa sana kwa sababu watu wanaharibu maisha yao kwa vitu hivyo viwili ambavyo ni hisia za chuki na wivu. Hakuna wivu mzuri wala wivu mbaya, wivu ni wivu tu hivyo unapozalisha hisia za wivu ndani yako jua lazima utayaacha maisha yako katika hali ya hatari.
Angalia maisha ya watu yalivyo, yamejaa chuki. Watu wanaishi nyumba moja na hata pengine kulala kitanda kimoja lakini wanachukiana hawapendani kabisa.
Chuki walizonazo watu huwa zinazalisha asidi kali sana na matokeo yake zinawaharibu watu.
Kumchukia mtu bila sababu hiyo ni dalili ya wivu. Utashangaa mtu anaibua sababu zake tu binafsi za kumchukia mtu hapa ni baada ya kumuona labda amemzidi kimafanikio na hii ni baada ya kujilinganisha na kujiona hana maana ndiyo maana hatupaswi kujilinganisha kwani kujilinganisha ni mwizi wa furaha yetu.
Lazima tuwe watu chuki na wivu pale endapo tunakuwa hatuwathamini vizuri wale watu wetu wa karibu na sisi kutoheshimu maisha yetu.
Ukiheshimu maisha yako huwezi kuhangaika na maisha ya watu.
Ukijiona wewe ndiyo una stahili zaidi katika maisha yako lazima uzalishe hisia za chuki na wivu.
Usitamani vitu vya watu wala usijilinganishe na mtu maana hii njia mojawapo ya watu wengi kujiingiza kwenye wivu na chuki.
Hatua ya kuchukua leo; Ili uweze kuepukana na watu wenye wivu na chuki kwako dawa yao ni kuwapa hisia za upendo.
Hata kama unajua mtu anakuchukia mpende na ule upendo unaompa utageuza chuki alizonazo.
Tusipobadili fikra zetu basi maisha yetu yataishia kwenye wivu na chuki.
Kwahiyo, mtu ambaye ni makini anajua nini haswa anataka hawezi kupoteza muda wake kwenye mambo ya wivu na chuki kwa sababu ana mambo mengi ya kufanya na anajua akijiingiza huko atachelewa kufanya mambo yake muhimu.
Una muda mchache wa kutimiza ndoto zako hapa duniani hivyo kamwe usipoteze muda wako kwa kutumia vibaya kwenye wivu na chuki.
Kila la heri rafiki yangu.
Makala hii imeandikwa na
Mwl. Deogratius Kessy ambaye ni mwalimu, mwandishi na mjasiriamali.
Unaweza ukatembelea mtandao wake kujifunza zaidi ambao ni http://kessydeo.home.blog
Unaweza kuwasiliana naye kwa namba 0717101505//0767101504
deokessy.dk@gmail.com
Asante sana na karibu sana.