Kama watu hawakuheshimu, ni kwa sababu wewe mwenyewe hujiheshimu. Kama wewe mwenyewe unaweza kujipangia mambo ambayo unataka kuyafanya, halafu wakati wa kuyafanya unapofika unaahirisha, ina maana hujiheshimu, na wengine nao watajifunza kutokukuheshimu. Kama unapoongea na wengine unajishusha na kuonesha mambo unayofanya siyo muhimu, na wao pia wanayachukulia hivyo.

Kama watu hawaheshimu kazi au biashara unayoifanya, ni kwa sababu wewe mwenyewe huiheshimu. Wewe mwenyewe unapoongea nao unawaambia kikazi chako au kibiashara chako unachofanya, hivyo unawafundisha jinsi ya kudharau kile unachofanya. Wanachorudisha kwako ni kile ambacho umewafundisha kufanya.

Kama watu hawaheshimu muda wako, ni kwa sababu wewe mwenyewe huuheshimu muda wako. Kama watu wanakuweka mahali ukisubiri kwa muda mrefu bila ya kujali muda unaopoteza, jua wewe umeshawafundisha kwamba muda wako siyo muhimu kihivyo, hivyo wanaweza kuupoteza tu wanavyojisikia.

Kama unataka watu wakuheshimu, anza kujiheshimu wewe mwenye, anza kujiwekea uzito kwenye maisha yako, anza kufanya kile ulichopanga kwa wakati uliofanya, epuka kuwa mtu wa kuahirisha mambo na ukishatoa neno lako kwa wengine, litimize kama unavyolitoa. Watu wanapoona unafanya hivyo, watakuheshimu, maana wanajua chochote unachosema au kuahidi, unaamaanisha kweli na utafanya.

Kama unataka watu waheshimu kazi au biashara unayoifanya, anza kuiheshimu wewe kwanza, ichukulie kwa uzito wa hali ya juu, ipende na kuwa na hamasa kubwa juu ya hicho unachofanya. Unapokutana na wengine na kupata nafasi ya kuelezea kazi au biashara yako, ielezee kwa namna ya kipekee, namna ambayo mtu ataona ndiyo kitu bora kuliko vyote duniani.

Na kama unataka watu waheshimu muda wako, anza kuuheshimu wewe kwanza. Usiwe mtu wa kupoteza muda kwa mambo yasiyo na umuhimu. Usiwe mtu wa kuruhusu watu wakupotezee muda wako, mtu ajue kabisa kwamba kama mmekubaliana kukutana saa nane kamili mchana, na saa nane na dakika 5 bado hajafika, basi unaondoka.

Kama ulishajidharau kwa muda mrefu, utakapoanza kujiheshimu watu hawatakuelewa, wataona unaringa, watanona unadharau, lakini unapoendelea watakuelewa na watakuheshimu.

Anza kujiheshimu wewe mwenyewe na wengine watakuheshimu pia.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha