Sisi binadamu ni viumbe wa hisia, huwa tunasukumwa kufanya maamuzi kwa hisia kabla ya kufikiri.
Kufanya maamuzi kwa hisia ndiyo chanzo cha matatizo yote tunayopitia kama binadamu.
Pamoja na kwamba tunapenda kufanya maamuzi yetu kwa kufikiri, hisia huwa zinatuingilia. Ni vigumu sana kupingana na hisia ukishakuwa katikati ya hisia.
Hivyo tunahitaji kitu cha kutuongoza wakati tumeshaingia kwenye hisia, wakati ambao fikra zetu zimeshakuwa mtumwa wa hisia zetu.
Na kitu hicho ni misingi. Unapokuwa na misingi uliyojiwekea na ambayo unaifuata wakati wote, itakuokoa wakati ambapo hisia zimekutawala.
Unapojikumbusha misingi yako, hisia zinakosa nguvu ya kukutawala kabisa, na hapo unaweza kufanya maamuzi sahihi.
Hivyo hakikisha kuna misingi uliyojiwekea ambayo unaiishi kwenye maisha yako, misingi ambayo unajikumbusha kila siku na kila wakati.
Kila unapoamka asubuhi andika misingi yako, unapoenda na siku yako na kukutana na vitu vinaibua hisia zako kabla hujaingia kwenye hisia hizo andika misingi yako.
Kwa kuwa karibu kiasi hicho na misingi yako, utaweza kuzishinda hisia zako na kuzuia zisiingilie maamuzi yako na kukugharimu.
Ishi kwa misingi na siyo hisia. Kwa sababu mwisho wa misingi ni utulivu, lakini mwisho wa hisia ni vurugu.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,