Pambana na hali yako ni usemi ambao ni rahisi sana kuwaambia watu wengine, lakini huwa hatupo tayari kujiambia sisi wenyewe.

Huwa tunafikiri hali zetu ni za kipekee sana hivyo lazima kila mtu ahusike nazo.

Na hapo ndipo tunapojidanganya, kwa sababu kila mtu tayari anapambana na hali yake, na hakuna anayepoteza muda wake kukufikiria zaidi wewe kuliko anavyofikiria mambo yake.

Hivyo ni wakati sasa wa wewe kupambana na hali yako kwa kumaanisha kweli.

Watu wengi wamekuwa wanashindwa kupiga hatua fulani kwenye maisha yao kwa kujali sana kuhusu wengine. Wengi wamekuwa wanaona wengine watawachukuliaje kwa kuwaona wakifanya kitu fulani.

Ambacho wanasahau ni kwamba, hakuna mtu anayekosa usingizi kwa sababu ya maisha ya mtu mwingine. Kila mtu tayari ana matatizo ya kumtosha kumkosesha usingizi, hawezi tena kuongeza mambo yako.

Hivyo kuwa huru kuishi maisha yako, kuwa huru kufanya kile unachotaka kufanya ana acha kufikiria wengine watakuchukuliaje, tayari wametingwa na mambo yao, hawana muda wa kuhangaika na mambo yako.

Hata wale unaoona wanakufuatilia sana, jua ni kwa muda tu ambao uko mbele yao, ukishaondoka wanakusahau na wanahangaika na mambo yao.

Kujua hili ni uhuru mkubwa sana kwa kila mmoja wetu kuweza kuchagua maisha sahihi kwake na kuacha wengine nao wachangue maisha sahihi kwao.

Kila mtu tayari anapambana na hali yake, ni wakati wako sasa kupambana na hali yako mwenyewe na kutokujali sana kuhusu wengine wanakuchukuliaje.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha