Uwanja wa ndege wa Schiphol uliopo mjini Amsterdam ulikuwa na changamoto moja kubwa sana. kwenye vyoo vya wanaume, gharama za kufanya usafi zilikuwa kubwa. Hii ilitokana na watu wengi kushindwa kulenga mkojo kwenye eneo sahihi na hivyo mkojo kwenda pembeni na kuchafua eneo kubwa la choo.

Kwenye miaka ya 1990, meneja wa usafi kwenye uwanja huo wa ndege alifikiria ni namna gani wanaweza kudhibiti hilo ili kupunguza gharama za kufanya usafi. Alipata wazo, wazo ambalo lingewawezesha watu kulenga mkojo wao sehemu sahihi na kupunguza uchafuzi wa eneo la choo.

Wazo alilolipata ni hili, kwenye eneo la wanaume kukojoa, aliweka picha ya nzi ambayo ilifanana na inzi wa kweli, picha hiyo ilikaa karibu kabisa na tundu sahihi la kulenga mkojo. Picha hiyo ilifanana kabisa na inzi wa kweli.

urinal fly.jpg

Baada ya miezi mitatu ya kuweka picha ya inzi kwenye eneo la kukojolea, matokeo yalianza kuonekana. Uchafuaji wa eneo la choo ulipungua kwa asilimia 80, watu waliweza kulenga vizuri zaidi na gharama za usafishaji wa vyoo zilipungua kwa zaidi ya asilimia 8.

Ni kitu gani kilisababisha matokeo haya makubwa kiasi hicho kupatikana ndani ya muda mfupi?

Jibu ni hili, mtu alipoenda kukojoa, aliona inzi karibu na tundu la kulenga mkojo, hivyo alikazana kumlenga yule inzi na mkojo wake na hilo lilipelekea wao kulenga eneo sahihi na kupunguza uchafuzi wa choo kwa kukojoa pembeni.

Swali jingine ni kwa nini walichagua inzi? Jibu ni inzi ni mdudu anayelinganishwa na uchafu, lakini pia asiyo na madhara, hivyo mtu haoni shida kumlenga na mkojo akiona ni sehemu ya kusaidia usafi. Angewekwa mdudu anayependwa na wengi kama kipepeo, huenda baadhi wasingemlenga. Na wangeweka mdudu ambaye anauma kama nge huenda baadhi wangeacha kabisa kutumia choo husika.

Rafiki, hivi ndivyo nguvu ya lengo ilivyo kubwa na inavyoweza kuleta matokeo sahihi kama lengo sahihi litawekwa kwa watu sahihi.

Wape watu lengo na wataacha kukusumbua.

Kupitia hadithi hii ya kweli, tunajifunza kitu muhimu sana ambacho tunaweza kukitumia kwa mafanikio yetu. Kitu hicho ni kama kuna watu ambao wanakusumbua, njia bora ya kuwafanya wasikusumbue ni kuwapa lengo fulani ambao wao wenyewe wanalifanyia kazi.

Tukirudi kwenye hadithi ya uwanja wa ndege, wangeweza kutumia njia mbalimbali kuwalazimisha watu kulenga mkojo sehemu sahihi. Kuweka matangazo kila mahali, kuweka faini kwa atakayechafua na mengine. Lakini yote hayo yangekuwa na gharama na yasingealisha matokeo mazuri. Lakini kwa kutambua saikolojia ya mwanadamu ya kupenda kukamilisha lengo, basi picha ya inzi imeweza kuleta matokeo makubwa na ya tofauti.

SOMA; Hii Ndiyo Nguvu Kubwa Iliyopo Ndani Yako Ambayo Ukiijua Na Kuanza Kuitumia Utakuwa Na Maisha Bora Sana.

Hili pia unaweza kulifanya kwenye maisha yako na wengine wanaokuzunguka.

Kwa kuanza na wewe mwenyewe, kama kila mara umekuwa unajikuta unapanga kufanya kitu lakini unahirisha, au ukianza kufanya unakosa hamasa ya kuendelea na kuacha, au usumbufu wa simu, tv na wengine unakufanya ushindwe kufanya kitu kwa muda mrefu, tatizo ni moja, unakosa lengo. Kila unapopanga kufanya kitu chochote jiwekee lengo ni hatua ipi unayotaka kufikia kwenye kufanya kitu hicho, kisha unapoanza kufanya, unakuwa unaongozwa na lengo hilo. unapokuwa na lengo, hutaruhusu usumbufu wowote wa pembeni ukutoe kwenye kile unachofanyia kazi. Pia ni rahisi kujiambia nikimaliza hiki ndiyo nitafanya kitu kingine.

Kwa wafanyakazi wako kama wewe ni mwajiri au mfanyabiashara ambaye una wasaidizi na wanakusumbua kukamilisha majukumu yao, wape lengo. Kaa chini na kila mfanyakazi wako na mpe lengo la kufanyia kazi, mpe namba fulani ambayo anapaswa kuikamilisha au kufikia kila siku, na hapo utakuwa umempa kitu cha kumsukuma. Kila mtu anayekufanyia kazi, hakikisha kuna kitu ambacho anapaswa kukamilisha ambacho kinapimika, hicho kinakuwa lengo lake na atakazana kulifikia. Utashangaa kuona watu wakikamilisha malengo kwa njia ambazo hata hujawahi kuzifikiria.

Hili pia linawezekana kwa wateja wako, kama unafanya biashara na wateja wanasumbua kununua, kila unapopata mteja kwenye biashara yako, msaidie kujiwekea lengo. Hakikisha mteja anakuwa na lengo fulani kupitia kile ambacho anataka kununua, na lengo hilo litamsukuma kukamilisha mauzo ili aondoke na kitu chake. Kwa mfano kama unauza simu na mteja kuna simu ameipenda au kuiulizia, mfanye aone kama tayari simu hiyo ni yake, na sifa zote za simu unazompatia mweleze kama ni yake. Akikuuliza kamera ya hii siku iko wapi, mjibu kamera ya HII SIMU YAKO, iko hapa. Endelea hivyo kwa maswali na maelezo mengine na mpaka mnafika mwisho mteja anakuwa ameshaichukulia simu kama yake.

Mwisho hili la kuwapa watu lengo unaweza kulitumia hata kwenye ngazi ya familia. Kama una watoto, ndugu wa karibu au hata mwenza wako anakusumbua, unaweza kutumia njia za ukali na adhabu na zisifanye kazi, lakini ukitumia njia ya lengo, matokeo yake ni mazuri, ya haraka na yasiyohitaji nguvu. Mfano kama mtoto hapendi kufanya kazi za shule yeye mwenyewe, unaweza kumpa lengo ambalo litamsukuma kila siku kufanya kazi zake. Labda kuna kipindi cha tv anapenda kuangalia, atakuwa na ruhusa ya kufanya hivyo kama atakuwa amefanya kazi zake. Hilo litamsukuma kufanya kazi zake haraka ili apate nafasi ya kuangalia kipindi chake pendwa.

Kisaikolojia, sisi binadamu huwa tunakuwa na ufanisi tunapokuwa na lengo, bila ya lengo akili zetu zinakosa umakini na hivyo tunajikuta tukifanya makosa au kutokukamilisha yale tuliyopanga.

Kuondokana na hali hii hakikisha kila wakati kuna lengo ulilojiwekea na unalofanyia kazi, na hata wale wanaokuzunguka nao wana malengo ambayo wanayafanyia kazi. Lengo hata kama ni dogo lina nguvu ya kumsukuma mtu kuchukua hatua sahihi.

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania