Rafiki yangu mpendwa,

Kama umekuwa mfuatiliaji wa mambo yanayoendelea duniani, hasa kwenye upande wa sayansi na teknolojia, utakuwa unapata taarifa mbalimbali kwenye eneo la kazi.

Taarifa kubwa na ambazo ni nyingi kwa sasa ni uwezo wa maroboti (Artificial Intelligence) kufanya kazi ambazo binadamu pekee ndiyo walikuwa wanaweza kuzifanya huko nyuma. Maroboti haya yanapewa taarifa za kutosha na kisha yanapewa jukumu hivyo yanatumia taarifa yalizopewa kufanya maamuzi sahihi.

Kwa sasa maroboti yanaendesha magari, yanaendesha mitambo mbalimbali, yanafanya upasuaji kwenye miili ya binadamu, yanagundua dawa, yanaendesha bendi za muziki na yanahudumia watu kwenye migahawa na hata maofisi mbalimbali.

Unaweza kujiuliza nini kinawasukuma watu kutumia maroboti kwenye kazi na kuwaacha binadamu? Je ni kwamba binadamu wamekuwa wachache kiasi cha kuhitaji kutengeneza nguvu kazi ya ziada?

Jibu ni hapana, binadamu ni wengi, lakini bado watu wanatafuta nguvu kazi ya ziada. Na sababu kuu ni moja, SISI BINADAMU NI WASUMBUFU.

Kubali au ukatae, ni rahisi kupangia roboti kazi, likafanya kama unavyotaka bila hata ya kufuatiliana kwa karibu.

Lakini mpangie binadamu kazi, kwanza ataitekeleza kwa viwago tofauti na ulivyotaka wewe, inabidi umfuatilie kwa karibu katika kuitekeleza, atachelewa kufika eneo la kazi, ataahirisha kazi hiyo mara kwa mara, ataumwa, ataiba baadhi ya vitu vinavyohusika na kazi hiyo na mengine mengi.

Hivyo waajiri na wazalishaji, wanapokaa chini na kupiga hesabu, wanagundua ni rahisi kuyatumia maroboti kuliko binadamu, na ndiyo maana utegemezi wa maroboti unashika kasi kubwa duniani.

high output.jpg

PANDE MBILI ZA UFANISI NA UZALISHAJI.

Kwenye makala ye leo kuna pande mbili, ambazo zote zitakusaidia sana.

Upande wa kwanza ni wa mwajiri, kama wewe umeajiri watu au ni meneja ambaye unasimamia watu, utajifunza jinsi ya kuongeza uzalishaji na ufanisi wa wafanyakazi wako. Hivyo kama huwezi kupata maroboti, utaweza kuwatumia watu wako vizuri.

Upande wa pili ni wa mwajiriwa, kama wewe umeajiriwa au hata kama umejiajiri, utajifunza jinsi unavyoweza kuongeza uzalishaji na ufanisi wako, ili maroboti yasichukue nafasi yako kirahisi.

Karibu sana tujifunze, uondoke na hatua za kuchukua ili uweze kuwa bora na kupata watu bora pia.

MATATIZO MAWILI YA KAZI.

Andrew Grove, aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa kampuni ya teknolojia ya Intel, aliandika kitabu alichokiita HIGH OUTPUT MANAGEMENT. Hiki ni kitabu ambacho kinatoa mwongozo kwa wale wote ambao wameajiri au wanasimamia watu wengine kukamilisha majukumu fulani.

Kwenye kitabu hiki, Andrew anasema kama mfanyakazi hafanyi kazi yake vizuri, kuna mambo mawili; HAWEZI AU HATAKI.

Ili wewe kama meneja au mwajiri wake uweze kumsaidia mfanyakazi huyo, lazima kwanza ujue tatizo lake ni lipi na ndipo ulitatue kwa usahihi.

Unapaswa kujua mfanyakazi HAWEZI kufanya kazi yake na hapo kuhitaji mafunzo ya kumjengea uwezo au HATAKI kufanya kazi yake na hapo kumpatia hamasa ya kumsukuma kuifanya.

Kupitia matatizo haya mawili ya wafanyakazi, tunapata njia mbili za kuwasaidia kufanya kazi zao vizuri, hivyo kuongeza uzalishaji na ufanisi wa wafanyakazi hao na hata wa kwako mwenyewe.

SOMA; Makosa Mawili (02) Makubwa Yanayogharimu Maisha Ya Watu Wengi.

NJIA YA KWANZA; MAFUNZO.

Watu huwa wanaajiri wafanyakazi, kisha wanawapa majukumu ya kufanya na kuwaacha wayafanye majukumu hayo. Kinachotokea ni wafanyakazi hao kuwa na uzalishaji mdogo na ufanisi mbovu. Wafanyakazi hawa wanakuwa HAWAWEZI kufanya kazi zao na hivyo wanahitaji kupata mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kufanya kazi zao vizuri.

Hivyo angalia wafanyakazi wako na jua kwa nini hawafanyi kazi zao vizuri, kama hawawezi, basi lazima uwafundishe jinsi ya kufanya kazi hizo.

Wewe kama mwajiri au meneja ndiye mwenye jukumu la kuwafundisha wafanyakazi wako jinsi ya kufanya kazi zao kwa ufanisi na uzalishaji mkubwa.

Andaa mafunzo ya kuwajengea uwezo wafanyakazi wako kisha wape mafunzo hayo. Mafunzo yanapaswa kuwa rahisi na yenye hatua za kuchukua ambapo mtu akijifunza anajua anapaswa kufanya nini.

Pia baada ya mafunzo wafuatilie wafanyakazi wako katika utekelezaji.

Kwa upande wa pili, kama wewe ndiyo mfanyakazi unapaswa kutathmini matokeo unayozalisha na kisha kujiuliza kama ndiyo matokeo bora kabisa unayoweza kuzalisha. Kama siyo, jiulize sababu ni nini. Kama ni UWEZO, basi angalia ni vitu gani hujui na kisha jifunze.

Dunia ya sasa ni rahisi sana kujifunza kitu chochote kile, kila kitu kipo mtandaoni, ni wewe kujua unataka kujifunza nini kisha kukitafuta na kujifunza.

SOMA; Wape Watu Lengo Na Wataacha Kukusumbua.

NJIA YA PILI; HAMASA.

Wafanyakazi wanaweza kuwa wanajua nini wanapaswa kufanya na wanajua jinsi ya kufanya, lakini bado hawafanyi. Hapa wafanyakazi hao wanakuwa HAWATAKI kufanya na hivyo wanachohitaji ni HAMASA ya kuwasukuma kufanya wanachopaswa kufanya.

Wewe kama mwajiri au meneja, unapaswa kuwa na njia za kuwahamasisha wafanyakazi wako kuwa na uzalishaji na ufanisi mkubwa. Ukishajua kwamba tatizo siyo ujuzi bali hamasa, basi wape hamasa.

Kuna njia mbili za kuwahamasisha watu, ambazo ni ZAWADI na ADHABU.

Zawadi inawahamasisha watu kufanya zaidi jambo kwa sababu wananufaika. Mfano kama mtu akifikia kiwango fulani cha uzalishaji au ufanisi basi kuna zawadi au bonasi anapewa, hivyo atajisukuma zaidi kufikia kiwango hicho ili apate zawadi hiyo.

Adhabu inawahamasisha watu kutokufanya makosa au uzembe kwa sababu wataumia. Kwenye adhabu, mtu anapofanya makosa au kushindwa kufikia viwango alivyowekewa, basi anapewa adhabu fulani, labda kukatwa malipo yake au kuondolewa kwenye kazi na kadhalika.

Kama mwajiri au meneja, unapaswa kupanga aina ya hamasa kulingana na wafanyakazi wako na aina ya kazi wanazofanya.

Kwa upande wa pili, kama wewe ni mfanyakazi, unaweza kujihamasisha mwenyewe kwa kujipa zawadi au adhabu kulingana na matokeo unayozalisha. Hilo litakusukuma kuzalisha matokeo bora zaidi.

Rafiki, hizo ndizo njia mbili za kuongeza uzalishaji na ufanisi wa wafanyakazi wao na wewe mwenyewe, ambazo ni MAFUNZO kwa WASIOWEZA na HAMASA kwa WASIOTAKA.

Kitabu HIGH OUTPUT MANAGEMENT kina mafunzo mengi sana ya jinsi ya kuwasimamia watu vizuri ili kuweza kuzalisha matokeo makubwa. Hiki ni kitabu ambacho kila mtu anayetaka kufanya makubwa anapaswa kukisoma.

Kitabu hiki kimechambuliwa kwa kina na kina hatua mbalimbali za kuchukua. Uchambuzi wa kitabu HIGH OUTPUT MANAGEMENT kinapatikana kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA. Jiunge na channel hii upate uchambuzi wa kitabu hicho na vingine vingi. Kujiunga na channel hii, fungua; https://www.t.me/somavitabutanzania kisha bonyeza JOIN CHANNEL.

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania