Hakuna kitu ambacho kinatuumiza zama hizi na kutuzuia kufanikiwa kama vitu vya bure.
Tunaishi zama ambazo kuna huduma nyingi mno ambazo zinapatikana bure, na hivyo tunazipokea haraka na kujenga tabia ambazo zinatugharimu.
Sehemu kubwa inayotuathiri ni kwenye mitandao ya kijamii. Mitandao yote mikubwa ni bure kabisa kutumia, ni wewe tu kuwa na kifurushi na kutumia. Tena mitandao mingine imekwenda mbali zaidi, imefanya huduma zao kubwa bure hata kama mtu hana kifurushi.
Wengi tunafurahia huduma hizi za bure, lakini tumekuwa hatuangalii madhara ya vitu hivi vya bure. Tumekuwa tunaona ni muda kidogo tunaweka kwenye huduma hizo, lakini pia tumekuwa hatupimi muda huo.
Njia bora kabisa kwako kupima umuhimu wa vitu unavyopewa bure ni kujiuliza kama ungekuwa unalipa je ungefanya?
Kama unafungua instagramu au facebook kila baada ya dakika 10 kuangalia nini kinaendelea, kama ungepaswa kulipia kila unapofungua au kwa kila dakika unayotumia huduma hizo, je ungeendelea kutumia? Na je ungetumia kwa dakika ngapi kwenye siku yako?
Kila kitu ambacho kinachukua muda wako wa siku kipime kwa malipo ambayo uko tayari kutoa. Na kama hautakuwa tayari kulipa ili kutumia kitu au huduma fulani unayoipata bure, basi hupaswi kuwa unaitumia kabisa, iondoe kabisa kwenye maisha yako.
Usidanganywe na neno bure, hakuna kitu cha bure duniani, kuna namna unalipa. Hivyo kuwa makini, weka thamani kwenye kila kitu na lipia thamani ambayo ni sahihi kwako.
Muda wako una thamani kubwa sana, usiugawe hovyo kwa vitu unavyoambiwa ni vya bure, kwa sababu vinakugharimu muda ambao una thamani kubwa zaidi kwako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,