“Many times an old man has no other evidence besides his age to prove he has lived a long time.”
—SENECA, ON TRANQUILITY OF MIND, 3.8b
Ni siku nyingine mpya, siku bora na ya kipekee sana kwetu.
Tumepata nafasi nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kuzingatia maeneo hayo matatu, siku hii ya leo itakuwa bora na ya kipekee sana kwetu.
Asubuhi ya leo tutafakari UNA USHAHIDI GANI WA MAISHA YAKO?
Rafiki, watu wengi wamekuwa wanajiambia kwamba wanaishi, lakini ukiangalia hakuna ushahudi wowote wa maisha yao.
Wengi wanasukuma tu siku hapa duniani na siku wanayoondoka ndiyo wanasahaulika kabisa.
Swali muhimu sana kwako kujiuliza ni je una ushahidi gani wa maisha yako?
Ni alama gani unayoweza kuonesha kwamba ulipita hapa duniani, ili hata ukiondoka leo, watu waendelee kukumbuka ulikuwepo?
Wengi sana hawana cha kuonesha, kwa sababu hawana cha tofauti wanachofanya, wanaendesha maisha yao kwa kawaida kama watu wengine.
Wewe unapaswa kuwa tofauti, unapaswa kukumbuka kwamba muda wako una ukomo, na hivyo kuutumia kwa mambo yenye tija kwako.
Ili unapoulizwa kama umeishi, usiishie kutumia umri kama ushahidi wako kwamba umeishi, bali kuonesha alama ulizoacha kwa maisha uliyoishi.
Wengi husingizia kwamba hawana muda ndiyo maana hawana ushahidi wowote wa maisha yao.
Na huo ni uongo.
Kama unasema huna muda, hebu fanye hesabu hii, chukua miaka yako, zidisha mara 365 kisha zidisha mara 24. Hapo utapata masaa ambayo umeshayatumia hapa duniani.
Yatakuwa ni masaa mengi sana, kama una miaka 30 ni zaidi ya masaa laki mbili na nusu, miaka 40 zaidi ya masaa laki yatu na nusu na kuendelea.
Hebu fikiria kama ungetenga masaa elfu moja tu au elfu 10 na kufanya kitu cha tofauti na chenye manufaa kwa wengie, je hutaacha alama hapa duniani?
Rafiki, muda unao sasa, anza kuutumia ili uache alama hapa duniani.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuishi na kuacha ushahidi wa maisha yako na siyo tu kuhesabu miaka.
#AchaAlama #UsihesabuMiakaHesabuUlichofanya #MudaUnaoMwingiUnaupoteza
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani
http://www.t.me/somavitabutanzania
Asante sana kocha kuanzia sasa sitahesabu miaka niliyoishi hapa duniani nitahesabu Yale niliyofanya ili nikiondoka duniani niache ushahidi hapa duniani .
LikeLike
Vizuri James.
Kila la kheri.
LikeLike