Naamini sana kwenye kujifunza, hasa kupitia usomaji wa vitabu.
Naamini ndani ya nafasi yangu kwamba mtu yeyote, anaweza kubadili maisha yake kupitia usomaji wa vitabu.
Pia naamini mtu ambaye hasomi vitabu, anajizuia yeye mwenyewe kuiga hatua za kumwezesha kufanikiwa kwenye maisha yake.
Pamoja na manufaa makubwa ya usomaji vitabu, ipo hatari moja kubwa kwenye usomaji wa vitabu.
Unaposoma vitabu vingi, unapata maarifa mengi, unakutana na mawazo mengi ambayo unatamani kuyafanyia kazi. Lakini hayo yanakuwa ni mawazo tofauti kabisa na kazi au biashara unayofanya.
Hivyo wengi wamekuwa wanajikuta wakianzisha vitu vipya kila wanapojifunza, lakini hawaviendelezi kwa muda mrefu, badala yake wanaanzisha tena vitu vingine vipya kupitia maarifa mapya ambayo wameyapata.
Sasa unahitaji njia sahihi a kuzuia maarifa mengi ambayo unayapata kwenye vitabu yasiwe usumbufu kwako na kukupoteza. Na nimekuwa nashauri mambo mawili muhimu ambayo kila msaka maarifa anapaswa kufanyia kazi.
Moja ni kuwa na maono makubwa ya maisha yake, ambayo anayafanyia kazi kila siku ili kuyafikia. Maono hayo yanapaswa kuwa makubwa na yanayomsukuma mtu kuchukua hatua za tofauti.
Pili ni kila unachojifunza jiulize kinakusaidiaje wewe kufikia maono yako makubwa na jinsi gani unaweza kukifanyia kazi kwenye malengo uliyonayo sasa. Usiwe mtu wa kuanza kitu kipya kwa kila maarifa unayojifunza, badala yake ni kutumia kila maarifa mapya unayoyapata kufikia kile ambacho umeshachagua kufanyia kazi.
Ukienda kwa namna hii, maarifa unayoyapata yatakuwa bora sana kwako, yatakupa hatua za kuchukua kufika unakotaka kufika, badala ya kuwa usumbufu kwako wa kujaribu vitu vipya kila wakati.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,