Rafiki yangu mpendwa,

Kila mmoja wetu anajua ya kwamba atakufa, kwamba mwisho wa maisha yetu hapa duniani ni kifo, ambacho hatujui ni lini kitakuja, ila tunajua kitakuja.

Katika kila kifo cha mwanadamu, huwa kunakuwa na sababu, na sababu ambazo zimezoeleka ni magonjwa mbalimbali, ajali na hata wakati mwingine kifo kimekuwa kinatokea ghafla.

Lakini sababu zote hizi ni za nje, na ni sababu ambazo zenyewe hazina nguvu kama hazijapata sababu moja kubwa na ya ndani ambayo ndiyo inapelekea watu wengi kufa kabla ya muda wao.

Kwenye makala hii ya leo, unakwenda kujifunza sababu hii moja kubwa ya kifo ambavyo imekuwa inasababisha watu kufa kabla ya wakati wao na jinsi unavyoweza kuitumia wewe na ukaishi kwa muda mrefu zaidi.

Lakini kabla hatujaingia kujifunza sababu hiyo kubwa ya kifo, tunakwenda kuangalia maisha ya wale ambao walipitia mazingira magumu sana ambapo walikuwa wanakutana na hali zinazopelekea kifo kila siku, lakini waliweza kuzivuka na kuishi.

Man's Search for Meaning.jpg

Viktor Emil Frankl (26 March 1905 – 2 September 1997) alikuwa daktari bingwa wa magonjwa ya akili wa Vienna, Austria wakati wa vita ya pili ya dunia. Moja ya mambo makubwa na ya kutisha yaliyotokea wakati wa vita ya pili ya dunia ni kuwepo kwa makambi maalumu ya kuwaweka wafungwa wa kivita, ambao wengi wao walikuwa Wayahudi.

Frankl naye alikuwa myahudi, hivyo mwaka 1942 alipelekwa kwenye moja ya makambi hayo. Mwaka 1944 alihamishwa kutoka kwenye makambi ya kawaida, kupelekwa kwenye makambi ambayo yaliandaliwa maalumu kwa ajili ya kuua watu. Makambi hayo, (kambi kuu ikiwa ni Auschwitz) yalikuwa na vifaa na maeneo maalumu ya kufanya mauaji ambayo yaliwalenga zaidi wayahudi. Maeneo hayo yalikuwa ni chumba chenye hewa ya sumu, tanuru la kuchoma watu na kazi ngumu ambazo zilipelekea wengi kufanya.

Kwenye kitabu chake kinachoitwa Man’s Search for Meaning, Frankl ameshirikisha mateso aliyopitia kwenye makambi ambayo alipitia kati ya mwaka 1944 mpaka 1945 ambapo vita iliisha na makambi yote kufungwa.

Anaeleza siku ya kwanza kufika kwenye kambi ya Auschwitz, asilimia 90 ya watu waliuawa siku hiyo hiyo. Mtu yeyote ambaye alikuwa na ugonjwa au udhaifu wowote unaomzuia asiweze kufanya kazi ngumu, aliwekwa kwenye kundi la watakaouawa.

Mateso yalikuwa makali sana, kazi ngumu kwenye mazingira magumu na chakula kilikuwa cha kipimo kidogo, kipande cha mkate kila siku na supu ambayo ilikuwa kama maji tu.

Frankl kwa taaluma yake ya daktari bingwa wa magonjwa ya akili (Psychiatry) aliweza kutumia nafasi hiyo kujifunza kwa kina zaidi kuhusu hali na mtazamo wa binadamu katika nyakati ngumu, hasa pale ambapo mtu anajua anakwenda kukutana na kifo.

Ni kupitia maisha hayo aliyopitia, Frankl anatushirikisha kitu kimoja ambacho kinawafanya wengi kufa kabla ya muda wao.

Frankl anaeleza kwamba katika kipindi ambacho alikaa kwenye makambi hayo, aliona watu wengi walikuwa wanakufa siyo kwa magonjwa wala mateso makali, bali kilichowaua wengi zaidi ni KUKATA TAMAA.

Franklin anaonesha kwamba wakati mtu anakuwa na matumaini, anakuwa imara na kuweza kukabiliana na ugumu wowote unaokuja mbele yake. Lakini pale tu anapokata tamaa, mwili wake unakuwa dhaifu na haichukui muda, anakufa.

Frankl ameshirikisha mifano miwili kuonesha jinsi KUKATA TAMAA kunavyoyachukua maisha ya mtu haraka.

Mfano wa kwanza ni wa mfungwa mwenzake ambaye alimshirikisha ndoto ambayo aliipata usiku huo. Mfungwa huyo alimwambia kwamba ameota kwamba kufikia Machi 30 ya mwaka 1945 watakuwa wameokolewa kutoka kwenye makambi hayo ya mateso. Wakati anapata ndoto hiyo ilikuwa Februari 1945. Wakati anamweleza ndogo hiyo, alikuwa na matumaini makubwa na mtu mwenye nguvu. Lakini kadiri siku zilivyoenda na machi 30 kukaribia, hakukuwa na dalili zozote za kukombolewa. Machi 29 mfungwa huyo aliugua ghafla kwa kupata homa kali, tarehe 30 alipoteza kumbukumbu na tarehe 31 alifariki duniani. Kwa mwonekano wa nje mtu huyu anaonekana alikufa kwa Taifodi, lakini kwa ndani, kilichomuua ni yeye KUKATA TAMAA, hasa pale ambapo matarajio yake hayakufikiwa.

Mfano wa pili ni takwimu ambazo Frankl alipewa na daktari mkuu wa kambi aliyokuwepo. Takwimu hizo zilionesha kwamba kati ya Krismasi ya mwaka 1944 na mwaka mpya 1945, idadi ya wafungwa waliokufa ilikuwa kubwa sana kuliko kipindi kingine chochote. Na hii ni kwa sababu wafungwa wengi walikuwa na matumaini kwamba watakuwa wameshaachiwa huru na kurudi majumbani mwao kabla ya Krismasi ya mwaka 1944. Hivyo Krismasi ya mwaka huo ilipofika huku bado wakiwa kwenye makambi, walikata tamaa na hapo vifo vikaongezeka.

Rafiki, kwa mifano hiyo miwili na mingine mingi ambayo tunaiona kwenye maisha yetu ya kila siku, ipo wazi kwamba sababu kuu ya kifo kwa wengi ni KUKATA TAMAA. Watu wawili wanaweza kuwa kwenye hali moja, mmoja akafa na mwingine akapona, na kinachokuwa kimewatofautisha ni hali ya KUWA NA MATUMAINI au KUKATA TAMAA.

VITU VIWILI VYA KUFANYA ILI UWE NA MAISHA MAREFU.

Rafiki, kwa haya tuliyojifunza, ili uweze kuwa na maisha marefu na kuepuka kufa kabla ya muda wako, kuna vitu viwili muhimu sana unavyopaswa kuvifanya.

Jambo la kwanza ni kujijengea MATUMAINI.

Lazima uwe na matumaini makubwa kwenye maisha yako, lazima uwe na kitu kikubwa unachokifanyia kazi, kinachokupa matumaini kwamba maisha ya kesho yatakuwa bora kuliko maisha ya leo. Haijalishi ni hali ngumu kiasi gani unayopitia, unapokuwa na matumaini ya kitu bora zaidi siku zijazo, unapata nguvu ya kuendelea kupambana na maisha yako kuendelea.

Matumaini yanajengwa kutoka kwenye maana ya maisha ambayo mtu unakuwa nayo, kwa kujua kusudi lako hapa duniani, kisha kuwa na maono na ndoto kubwa ambazo unazifanyia kazi. Kwa kujua kwamba kuna kitu umeletwa kufanya hapa duniani, na kuona jinsi ambavyo kinawagusa wengine, unakuwa na matumaini makubwa.

Na hata kama hujajua maana au kusudi la maisha yako, basi jiwekee lengo lolote kubwa ambalo litakusukuma sana kulifikia, kisha jikumbushe lengo hilo kila siku na amini utalifikia.

Wapo watu wengi ambao walijiwekea malengo makubwa, wakajituma sana na kuyafikia, lakini baada ya kufikia malengo hayo wakafariki dunia. Hii ni kwa sababu kufanyia kazi lengo ndiyo ulikuwa msukumo mkubwa kwao, lakini baada ya kufikia lengo wakakosa msukumo na hivyo kukaribisha kifo.

Usikubali kukaribisha kifo rafiki yangu, kila wakati jua maana na kusudi la maisha yako, kuwa na maono makubwa unayotaka kufikia na jiwekee malengo makubwa. Na kila unapofikia lengo ulilojiwekea, weka lengo jingine kubwa zaidi ya hilo. Maisha yako yakikosa mahali pa kupata matumaini, yanakuwa mafupi.

Jambo la pili ni KUTOKUKATA TAMAA.

Kama tulivyoona kwenye mifano ya Frankl, wale waliokata tamaa walikuwa dhaifu na kupelekea magonjwa kuwaondoa duniani haraka. Hivyo basi, lazima ujiwekee ahadi hii kwenye maisha yako, KAMWE SITOKATA TAMAA.

Haijalishi umekutana na nini, haijalishi unapitia hali gani, usikubali kabisa kukata tamaa, wala usiruhusu fikra hasi na za wasiwasi kuingia kwenye akili yako. Kila wakati jikumbushe kusudi la maisha yako, kumbuka maono yako na malengo uliyojiwekea na hilo litaondoa hali ya kukata tamaa.

Dunia haitakupa kila unachotaka kwa wakati unaotaka wewe. Utaweka mipango yako vizuri, lakini matokeo utakayokuja kupata yatakuwa ya tofauti kabisa. Utakuwa na mategemeo fulani, lakini utakachokuja kupata ni tofauti kabisa na mategemeo yako. Hivyo hakikisha hali hizo unazopitia hazikukatishi tamaa, chukulia ni sehemu ya kawaida ya maisha na endelea kuwa na matumaini kwamba kesho itakuwa bora kuliko leo, kisha nenda kachukue hatua ili hiyo kesho iwe bora kweli.

Winston Churchill ni mmoja wa watu walioweka juhudi kubwa na kuiwezesha vita kuu ya pili ya dunia kumalizika. Moja ya kauli zake ambayo aliiamini sana ilikuwa ni hii; “Never give in. Never give in. Never, never, never, never—in nothing, great or small, large or petty—never give in, except to convictions of honour and good sense. Never yield to force. Never yield to the apparently overwhelming might of the enemy.” Akimaanisha kawe usikate tamaa, kamwe, kamwe, kamwe, kwa chochote kikubwa au kidogo bali kwa yale yaliyo sahihi. Kamwe usikatishwe tamaa na nguvu ya adui.

Jiambie leo na jikumbushe hili kila siku; KAMWE SITOKATA TAMAA. Na ukiweza kuishi hali hii kila siku, basi utakuwa na maisha marefu.

Ili usikate tamaa zingatia haya; kuwa na maono makubwa, amini kwenye maono hayo, usitake dunia iende kama unavyotaka wewe, pokea kila kinachokuja kwako na kitumie vizuri na usiwe mtu wa kulalamika au kulaumu wengine.

Rafiki, kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA, tunakwenda kupata uchambuzi wa kina wa kitabu cha Viktor Frankl kinachoitwa Man’s Search for Meaning. Kwenye kitabu hiki Frankl ameshirikisha historia yake kwenye makambi ya mateso na kisha kushirikisha matibabu bora ya kisaikolojia anayoyaita LOGOTHERAPY. Matibabu haya yamejengwa kwenye msingi kwamba hitaji kuu la watu ni MAANA YA MAISHA. Na hili Frankl ameweza kulionesha kupitia makambi ya mateso, ambapo anasema kila kitu kinaweza kuondolewa kwa mtu, lakini siyo mtazamo wake juu ya kile anachopitia. Frankl anatuambia tukishakuwa na maana ya maisha, hakuna kitakachotusumbua.

 

Kwenye uchambuzi wa kitabu hicho tutajifunza pia jinsi ya kutumia mateso na magumu unayopitia kwenye maisha kutengeneza maana ya maisha yako na kuweza kuwa na maisha bora kabisa. Huu siyo uchambuzi wa kukosa, hasa kwa zama tunazoishi sasa, ambapo maisha ya wengi yamekosa maana na ndiyo maana wengi wana msongo wa mawazo.

Kupata uchambuzi wa kitabu Man’s Search for Meaning karibu ujiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA, fungua; www.t.me/somavitabutanzania kisha bonyeza JOIN CHANNEL na utakuwa umejiunga. Karibu sana upate maarifa bora ili uwe na maisha bora pia.

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania