Kinachofuata ni kutekeleza, kama ulivyoamua na kama ulivyoahidi.

Usianze kutafuta sababu za kwa nini huwezi kufanya ulichoamua au kwa nini huwezi kutekeleza ulichoahidi.

Ni wewe mwenyewe uliyefanya maamuzi hayo, ni wewe mwenyewe uliyeahidi, jiheshimu na tekeleza.

Zama tunazoishi sasa ni za watu laini, watu ambao wanafanya maamuzi lakini hawayatekelezi, wanaahidi lakini hawatimizi. Hii ni kwa sababu wanapokutana na kikwazo kidogo tu, unakuwa ndiyo mwisho wa safari yao.

Huwezi kufanikiwa kama kila aina ya kikwazo kinakuwa na nguvu kwako.

Mafanikio yanakwenda kwa wale waliojitoa kweli, wale waliojiambia watapata wanachotaka, ije mvua, lije jua, watapambana mpaka kufika wanakotaka.

Wale ambao hawajitoi kwa kiwango hicho, dunia huwa ina njia rahisi ya kuwaondoa kwenye njia waliyochagua. Kwa sababu kwa kila unachochagua, hatua ya kwanza ni kukutana na vikwazo na changamoto. Kama hujajitoa kweli, hutaweza kuvivuka.

Kuanzia leo anza kujiheshimu, anza kujichukulia ‘siriazi’, unapopanga kufanya kitu, hata kama ni kidogo kiasi gani, hakikisha unakifanya. Unapoahidi kufanya kitu, hata kama ni kidogo kiasi gani, hakikisha unakikamilisha kama unavyoahidi.

Anza hilo kwa mambo madogo na utajifunza vitu viwili;

Moja utajifunza uvumilivu na unga’ang’anizi ambao ni muhimu sana kwa mafanikio yako.

Mbili utajifunza kuweka mipango michache na kuahidi machache ili uweze kuyatekeleza. Hii inakupa nidhamu ya hali ya juu, ya kuhangaika na yale muhimu pekee na kuachana na mengine.

Ukipanga tekeleza, ukiahidi timiza, ni rahisi kama hivyo, lakini wengi hawawezi kufanya na ndiyo sababu wengi hawafanikiwi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha