Rafiki yangu mpendwa,
Leo nakwenda kuzungumza na wale wanaofanya biashara za huduma, hasa huduma za ushauri wa aina mbalimbali.
Kwenye jamii zetu, ushauri umekuwa unachukuliwa kama kitu ambacho hakina thamani ya kulipiwa. Wengi wamekuwa wanaona ushauri ni kitu ambacho kinaweza kupatikana bure, hivyo wakiambiwa walipie ili kupata ushauri, wanaona kama wanaibiwa.
Na eneo ambalo limeathiriwa sana na hali hii ni kwenye ushauri na mafunzo ya maendeleo binafsi na mafanikio kwenye maisha.
Nimekuwa naona watu wengi wakiingia kwenye huduma hii ya kutoa maarifa ya maendeleo binafsi na mafanikio (personal development and success). Ni kitu ambacho ni kizuri, kwa sababu jamii yetu kwa kipindi kirefu haijapata huduma ya aina hii, hivyo watu walikuwa wanashindwa kupiga hatua kutokana na kukosa maarifa sahihi ya kufanya hivyo.
Huduma hii ina mfumo wa tofauti na biashara nyingine, kwa sababu unaanza kwa kutoa maarifa yako bure kabisa, iwe ni kwa mfumo wa maandishi, sauti au video. Kwa kuwa watu hawakujui na hawajui una nini ndani yako, inabidi uanze kutoa ulichonacho bure kabisa, na kupitia njia hiyo ndiyo wengi wanakujua.
Sasa wengi wamekuwa wanaingia kwenye huduma hii kwa kutoa maarifa yao bura, ila wanakwama hapo, wanashindwa kabisa kugeuza maarifa hayo kuwa sehemu ya kuingiza kipato. Kila wanapojaribu kuweka gharama kwenye mafunzo au ushauri wao, watu wanawarudisha nyuma, na kuwafanya wajisikie vibaya kuweka gharama kwenye ushauri.
Kwa hali hii, wengi wamekuwa wanashindwa kuendelea na huduma hii muhimu na kwenda kufanya mambo mengine.
Rafiki, kama upo kwenye huduma hii ya kutoa mafunzo ya maendeleo binafsi na mafanikio au hata kama upo kwenye huduma nyingine inayohusiana na utoaji ushauri kwa watu, nataka leo ujue kitu kimoja, unastahili kulipwa, hivyo usione aibu kuwaambia watu wakulipe kile unachotaka wakulipe.
Unapojaribu kutoka kwenye kutoa maarifa na ushauri wako bure na kuwataka watu walipie, wengi watakupa kauli za kukubeza na kukukatisha tamaa. Watakuambia huduma yako ni ya kusaidia jamii, hupaswi kulipisha watu. Wengine watakuambia kuwataka watu wakulipe fedha kwa ajili ya ushauri ni tamaa ya fedha na njaa. Haijalishi unawataka walipe gharama ndogo kiasi gani, hawatakosekana watu wa kukuambia maneno ambayo hutayapenda, lengo lao ni wewe ujisikie vibaya kutaka kulipwa kupitia ushauri unaotoa.
Na mimi rafiki yako nakuambia usiwasikilize, wewe weka utaratibu wa huduma yako, kwamba kuna maarifa ambayo yatapatikana bure kabisa, hayo mtu ataweza kuyatumia atakavyo, lakini anapotaka zaidi, basi lazima awe tayari kulipia ndiyo apate zaidi.
Kwa wale ambao bado hili linawapa tabu, au bado hawajaweka mpango mzuri wa kulipwa kwenye huduma yao, napendekeza mfanyie kazi hatua zifuatazo;
Moja; anza kwa kutoa maarifa au ushauri wa bure.
Kama nilivyotangulia kueleza, lazima kuwe na njia ya watu kujua nini kipo ndani yako. Hivyo huwezi kuanza kwa kuwaambia watu wakulipe wakati hawajajua una nini.
Kwa kuanza, toa maarifa au ushauri wako bure kabisa. Hapa unachagua njia unayotumia kutoa maarifa au ushauri huo. Kama ni njia ya maandishi basi kuwa na blog au njia nyingine ambapo unaweka maarifa hayo bure kabisa kwa kila mtu kuweza kutembelea na kujifunza. Kama umechagua njia ya sauti au video, chagua njia sahihi za kutoa mafunzo hayo bure kwa wengine.
Hatua hii wengi huwa wanaiweza, lakini pia ndipo wengi wanapokwama, wengi wanaishia kutoa maarifa na ushauri wao bure mpaka pale wanapochoka na kuacha.
Mbili; tengeneza vifurushi vya huduma zako.
Wakati unaendelea kutoa maarifa na ushauri wako bure, utaanza kujifunza kutoka kwa wale wanaokufuatilia. Watakuwa na maswali kwako, kuna maarifa fulani watu watayafuatilia zaidi kuliko mengine. Hapa sasa ndipo unapopaswa kutengeneza vifurushi vya huduma zako.
Hapa unagawa huduma zako kwenye mafungu mbalimbali kwa ajili ya wale wanaohitaji zaidi kutoka kwako.
Kifurushi cha kwanza ni hiyo huduma ya bure, ambayo itaendelea milele katika kipindi chote utakachokuwa kwenye biashara hiyo ya mafunzo na ushauri. Maana kupitia hapo ndiyo unatengeneza wateja wapya kwa huduma zako.
Kifurushi cha pili kinapaswa kuwa huduma au bidhaa ya bei ndogo kabisa, ambayo mtu yeyote anayethamini unachofanya hawezi kushindwa kuilipia. Hapa unaweza kuandaa kitabu kinachogusa lile eneo muhimu unalofundisha au kushauri, ambapo mtu anapata maarifa zaidi ya yale anayopata kwenye kifurushi cha bure. Kadhalika unaweza kuwa na kozi au mafunzo mengine ambayo mtu atapaswa kulipia ili kuyapata.
Kifurushi cha tatu kinapaswa kuwa ushauri wa moja kwa moja, iwe ni kwa njia ya simu au ana kwa ana. Hapa ni pale mtu anapohitaji zaidi kutoka kwako, na hivyo kuhitaji muda zaidi wa kumshauri yeye kwa karibu, hapa anapaswa kulipa gharama ya juu kidogo.
Unaweza kuendelea na vifurushi vingine kulingana na aina ya huduma unayotoa, unaweza kuwa na kifurushi cha ukocha kwa kumsimamia mtu kwa karibu kwa muda mrefu na vinginevyo.
Rafiki, kama unavyoona vifurushi hivyo, kadiri vinavyoongezeka, ndivyo wewe mtoa huduma unavyotoa muda wako zaidi kwa mtu mmoja, na hivyo gharama zake lazima ziwe juu ukilinganisha na vifurushi vya chini.
Kwenye biashara hii ya huduma, ni wachache sana ambao wanakaa chini na kuandaa vifurushi vyao huduma yao. Kama wewe upo makini kweli na huduma yako, ni lazima uandae vifurushi hivi.
Tatu; watu wanapotaka zaidi, lazima walipe.
Baada ya kuwa na vifurushi, kinachofuata ni utekelezaji. Unatoa maarifa na ushauri mzuri sana kupitia kifurushi cha bure ulichoweka, watu wanaelewa, wanachukua hatua na kupata matokeo mazuri, hivyo wanatamani kupata zaidi kutoka kwako. Na hapo wanakutafuta ili kupata zaidi.
Hapo sasa wape utaratibu wa huduma zako, kwamba wanaweza kupata nini kutoka kwako na kwa gharama kiasi gani. Waeleze wazi bila ya kuona aibu au kuogopa watakuchukuliaje, kumbuka siyo wewe umemtafuta, bali ni yeye amekutafuta. Amekutafuta kwa sababu kuna thamani unaitoa, hivyo ipe thamani kweli.
Unaweza kuanza kumweleza kifurushi kimoja kimoja kulingana na uhitaji wake, labda kitabu ambacho kina maarifa yatakayomsaidia kwa kile anachopitia au ushauri wa moja kwa moja kulingana na uhitaji wake.
Kama mtu hayupo tayari kulipia au hawezi kumudu kulipia basi mwelekeze arudi kwenye kifurushi cha kwanza, kile ambacho ni cha bure kabisa, ajifunze na kufanyia kazi yale anayojifunza na yatamsaidia. Na pale atakapoweza kulipia huduma zako nyingine basi anaweza kukutafuta.
Swali hapa ni unawekaje gharama za huduma zako, na hilo unaweza kulijibu mwenyewe, kulingana na aina ya maarifa na ushauri unaotoa, wale unaowalenga na kiasi unachohitaji kuingiza kupitia huduma yako. Lazima uchague huduma yako inawalenga watu gani na hapo kuona kiasi gani wanaweza kukimudu, muhimu ni usiwe rahisi sana, kwa sababu baadaye itakugharimu.
Nne; usiwe mwepesi kutoa ushauri wa haraka na bure.
Kuna watu watakupigia simu, watakuambia wamekutana na mafunzo yako, ni mazuri na yamewasaidia sana, wanaomba ushauri kidogo kwa haraka na kuanza kukueleza matatizo yao. Wasimamishe kabla hawajaendelea, washukuru kwa kufuatilia mafunzo au ushauri unaotoa, kisha wape utaratibu wa kupata ushauri kwako, ambao umeshauweka, na gharama wanazopaswa kulipa.
Wengi unapowapa utaratibu na gharama hizo watakuambia wanataka ushauri kidogo tu na kwa jambo dogo. Usiingie kwenye mtego huo, kama lingekuwa jambo dogo wangeshalitatua wao wenyewe, ni jambo kubwa ndiyo maana wanataka maoni ya mtu mwingine pia.
Kuwa makini sana na utoaji wa ushauri, maana huo ndiyo utajenga au kuua huduma yako. Acha kabisa utaratibu wa mtu kukueleza matatizo yake ndani ya sekunde 30 halafu anategemea wewe umpe suluhisho ndani ya sekunde nyingine 30. Huo hauwezi kuwa ushauri, ni ubabaishaji. Ushauri wa kweli ni pale unapomsikiliza mtu kwa makini, unamuuliza maswali mbalimbali, unaelewa namna anavyofikiri, mtazamo alionao na kujua wapi amekwama, kisha unamshauri njia sahihi. Hilo halitachukua chini ya nusu saa, na hivyo unapaswa kulipwa, kwa muda wako unaowekeza kwenye tatizo hilo la mtu.
Hapa ndipo watoa huduma wengi wanaposhindwa, huwa wanakimbilia kutoa ushauri haraka, yaani mtu anapiga simu ya kuomba ushauri na ndani ya dakika moja ameshaeleza tatizo lake na kupatiwa ushauri, haishangazi kwa nini watu wanadharau huduma hizi, kwa sababu tunazifanya kuwa rahisi sana na hatuzipi thamani inayostahili.
Tano; kumbuka hiyo ni kazi yako, unapaswa kulipwa.
Haijalishi unafanya nini ili kupata maarifa na ushauri ambao unawapa wengine, unawekeza muda, nguvu na akili katika kuandaa maarifa na ushauri huo. Hivyo ni kazi yako, ni biashara yako, na unapaswa kulipa kwa uwekezaji ambao umeufanya.
Usikubali kupoteza uwekezaji huo ulioufanya kwa sababu tu watu wanaona ni rahisi. Kumbuka wakati wewe unasoma au kuandika maarifa au ushauri unaotoa, watu wengine walikuwa wanafanya kazi zao, ambazo wanalipwa kuzifanya, halafu wakija kwako wanataka uwape bure. Usikubali, hiyo ni kazi yako, unastahili kulipwa.
Sita; usihadaiwe na maneno ya hila.
Watu wana maneno ya hila, watakusifia kwa maarifa na ushauri unaotoa bure na wewe utafutahia. Watataka kupata zaidi kutoka kwako, na utakapowapa utaratibu wako, ambao unahusisha gharama, hapo watabadilika, wataanza kukuambia maneno yenye hila, kwa lengo la kukufanya ujisikie vibaya.
Watakuambia huduma yako ni ya kuwasaidia watu, hupaswi kutoza fedha.
Watakuambia wao hawana fedha ya kukulipa, wana shida sana hivyo uwasaidie.
Watakuambia una tamaa kutaka kulipwa kwa ushauri ambao unapatikana bure kabisa kwa wengine.
Kabla hujaingia kwenye mtego wanaokuwekea watu hawa, jikumbushe haya;
Watu hawa wanaokuambia huduma yako ni ya kusaidia hivyo hupaswi kuwatoza fedha, wapo tayari kulipia vitu vingine vingi sana kwenye maisha yao, vingine hata havina maana. Utakuta wanaenda baa na kununua pombe, lakini hawapo tayari kukulipa wewe uwashauri.
Watu hao wanaokuambia wana shida sana, hawana fedha ya kukulipa uwashauri, hawaendi dukani na kueleza shida zao wakapewa chakula cha kwenda kula, wananunua. Hawaendi sokoni na kueleza shida zao wakapata mahitaji yao, wanalipa fedha. Wana simu ambayo wanaweka salio karibu kila siku, hawaelezi shida zao na salio likaingia, wanalipa fedha. Sasa kwa nini waweze kulipia kila kitu kwenye maisha yako halafu washindwe kulipia huduma yako?
Rafiki, ukishajiuliza maswali hayo, utapata jibu la wazi, kwamba siyo shida wala msaada, bali ni thamani ambayo watu hao bado hawajaiweka kwenye kile unachofanya. Hivyo waeleze thamani unayotoa na kama bado hawawezi basi waelekeze kurudi kwenye kifurushi cha kwanza ambacho ni cha bure.
Kamwe usikubali kunasa kwenye mtego wao na kuishia kuwapa ushauri au maarifa wanayoyataka bure, wataendelea kudharau huduma yako na hutaweza kupiga hatua.
Rafiki, haya nakushirikisha hapa ni uzoefu wangu binafsi na pia kupitia wale ambao nimekuwa nawakochi kwenye biashara hii ya huduma, ni vitu ambavyo nimejifunza kwa maumivu na naona wengine wengi wanajifunza kwa maumivu. Fanyia kazi hatua nilizokushirikisha hapa, na utaweza kuweka thamani kwenye kile unachofanya na watu kuwa tayari kulipia.
Na kama upo upande wa pili, upande wa mlaji, ambaye unaamini ushauri na mafunzo yote yanapaswa kupatikana bure na hakuna kulipia, basi nikusihi uthamini kazi za watu, kama hutaki kulipa usitafute watu, wewe soma yale yanayopatikana bure na yafanyie kazi. Lakini unapoanza kupiga simu ukitaka ushauri zaidi au maarifa zaidi, basi andaa mfuko wako kulipa pia.
Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.
Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania