Ukitaka kuwa na furaha ndani ya saa moja, lala. Kwa kulala unapata pumziko ambalo linafanya upate raha. Lakini muda mfupi baada ya kuamka furaha hiyo huisha.

Ukitaka kuwa na furaha ndani ya siku moja, fanya kile unachopenda kufanya ambacho siyo kazi. Hapo utajisikia raha kupitia kile unachofanya, lakini siku ikishapita, furaha hiyo inatoweka.

Ukitaka kuwa na furaha ndani ya mwezi, oa. Kwa kuwa na mtu unayempenda na kuwa naye karibu, kunaleta raha, hasa siku za mwanzoni. Baada ya hapo, karaha zinaweza kuwa nyingi kuliko raha.

Ukitaka kuwa na furaha ndani ya mwaka, pata urithi. Hapa utafurahia kupata mali ambazo hujazitolea jasho, lakini ni vigumu sana mali hizo zikavuka mwaka mmoja.

Ukitaka kuwa na furaha ya kudumu maisha yako yote, msaidie mtu mwingine. Kwa kuona umeyabadili maisha ya mtu utaridhika na yule ambaye umemsaidia hatokusahau, na hilo litakufanya uendelee kujisikia vizuri.

Hivyo tunaona wapi tunaweza kupata furaha ya kudumu kwenye maisha yetu. Haimaanishi hivyo vingine vinavyotupa furaha ya muda mfupi hatupaswi kuvifanya, vifanye kama sehemu ya maisha, lakini siyo kutegemea vitakupa furaha ya kudumu.

Chochote unachopata kinakupa raha kwa muda mfupi na baada ya hapo raha ile inaondoka, hivyo inakubidi ufanye tena. Lakini chochote unachotoa, kinaacha furaha ya kudumu kwako. Hivyo weka zaidi kwenye kutoa kuliko kupokea.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha