Kama kuna kitu rahisi kupata kwenye maisha basi ni sababu,

Haijalishi ni za kweli au uongo, sababu huwa rahisi sana kupatikana, na nyingi huwa ni za uongo.

Kwa matokeo yoyote yale unayopata, sababu tayari inakuwa inaambatana na matokeo yake.

Kama umeshinda utakuwa na sababu nyingi za kukuaminisha kwa nini umeshinda. Na kama umeshindwa pia utakuwa na sababu ambazo unaamini zimepelekea wewe kushindwa.

Ubaya si tu kwamba sababu hizo siyo sahihi, lakini pia hazikusaidii kupiga hatua. Kama umejipa sababu za kushinda, sababu hizo hizo hazitakuwezesha kushinda tena. Na kama umejipa sababu za kushindwa, haziwezi kukuondoa kwenye kushindwa na kukupeleka kwenye ushindi.

Hivyo usiwe mtu wa kutafuta sababu, bali kuwa mtu wa kuujua ukweli na kuweka misingi ambayo utaifuata mara zote, bila ya kujali ni matokeo gani unayopata.

Wale wanaofanikiwa sana, huwa hawaanzi kwa kufanikiwa, bali huwa wanaanza kwa kushindwa na kujifunza kupitia kushindwa kwao, wanajiwekea misingi sahihi na kuifuata.

Hivyo achana na sababu sasa na kazana kujenga misingi, sababu ni vitu vya kubahatisha lakini misingi ni kitu cha uhakika.

Mtu anaweza kuvaa nguo nyekundu akapata matokeo mazuri, siku nyingine tena akavaa nguo nyekundu akapata matokeo mazuri tena, hapo atajiambia kinachompa matokeo mazuri ni kuvaa nguo nyekundu. Lakini huu siyo ukweli, ni sababu tu ambayo anaifananisha. Kuna misingi fulani mtu huyo anakuwa anaifuata na ndiyo inamwezesha kupata matokeo mazuri, asipoijua hiyo na kuifuata, anaweza kuhangaika na nguo nyekundu kila wakati na asipate matokeo mazuri.

Misingi ndiyo inakupa matokeo ya uhakika, sababu ni kitu unachohusianisha na matokeo, ambacho mara nyingi siyo kitu halisi.

Usikimbilie kwenye sababu kama wengine, badala yake kazana na misingi.

Kukimbilia sababu kumeleta matatizo mengi sana kwenye jamii zetu, uchawi, ushirikina, wivu, chuki na hata kufanyiana ubaya inatokana na watu kuamini kwenye sababu kuliko kwenye misingi. Hivyo ukiijua misingi, mambo hayo ya kijamii hayatakusumbua kamwe.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha