Raymond Dalio (kuzaliwa August 8, 1949) ni bilionea mwekezaji kutoka nchini Marekani ambaye ameweza kupata mafanikio makubwa sana kwenye uwekezaji. Ray ni mwanzilishi wa kampuni kubwa ya uwekezaji inayoitwa Bridgewater Associates. Jarida la Forbes linamtaja kuwa mtu tajiri namba 57 katika orodha ya mabilionea (orodha ya mwaka 2019), akiwa na utajiri wa dola bilioni 18.7 sawa na tsh zaidi ya trilioni 43.

Mwaka 1975 Ray Dalio alianzisha kampuni yake ya uwekezaji iliyojulikana kama Bridgewater. Kutokana na kiu yake kubwa ya kujifunza, aliweza kufanya tafiti mbalimbali kuhusu uchumi na hizo zikamwezesha kupata matokeo mazuri kwenye uwekezaji.

Matokeo mazuri aliyoyapata yalimpa kiburi, akaanza kujiona tayari anajua kila kitu. Hivyo alianza kuwa na maoni ambayo aliyaamini kupitiliza. Kati ya mwaka 1979 mpaka 1982 Ray alipata anguko kubwa sana kwenye uwekezaji. Alitabiri anguko la uchumi kutokana na changamoto ya madeni, na alijiamini sana kwamba itakuwa hivyo, hilo lilipelekea afanye uwekezaji ambao ulimpa hasara sana pale ambapo alichotabiri hakikutokea.

makosa2.jpg

Anguko hilo lilimrudisha chini kabisa, kampuni yake ilishakuwa na wafanyakazi lakini baada ya anguko alipoteza wafanyakazi wote na akabaki mwenyewe. Hata fedha ya kula kwake ilikuwa tatizo, ilimbidi akope kwa baba yake ili aweze kuendesha familia yake.

Kitu ambacho kilimsaidia Ray kuvuka kipindi hiki na hata kampuni yake ya Brigdewater kuanza upya na hata kufanikiwa sana (kwa sasa ina zaidi ya wafanyakazi 1,500 na inasimamia uwekezaji wenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 160) ni kwamba alijifunza kutokana na makosa aliyofanya na kuweka misingi ya kumzuia asifanye makosa hayo tena.

Kwenye kitabu chake anachokiita PRINCIPLES, Ray anatushirikisha yale ambayo amejifunza kupitia makosa mbalimbali aliyowahi kufanya kwenye uwekezaji. Uchambuzi kamili wa kitabu hiki kwenye misingi yote aliyoshirikisha unapatikana kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA, fungua www.t.me/somavitabutanzania

Yafuatayo ni yale muhimu Ray aliyojifunza kutokana na makosa yake mbalimbali na yamemsaidia sana kujijengea misingi imara.

  1. Amejifunza kwamba kushindwa ni zao la kukataa kukabiliana na uhalisia wa maisha, kutaka mambo yawe tofauti na yalivyo. Mafanikio ni kuukubali na kukabiliana na uhalisia wa maisha.
  2. Amejifunza kwamba kuutafuta ukweli, bila ya kujali ukweli huo ni nini, ni muhimu sana kwenye maisha. Unapoujua ukweli, unakusaidia kuchukua hatua sahihi na kutokukosea.
  3. Amejifunza kwamba hakuna cha kuogopa kwenye ukweli. Japo kuna ukweli unaotisha na kuumiza, mfano kujua una ugonjwa usiotibika, kuujua ukweli kunakusaidia kukabiliana na mambo kama yalivyo. Kuwa mkweli na kuwafanya wengine nao wawe wakweli inasaidia kupata mrejesho unaokuwezesha kupiga hatua.
  4. Amejifunza kwamba kuwa mkweli kunakupa uhuru wa kuwa wewe. Wale ambao ndani wanakuwa watu wa aina fulani ila kwa nje wanataka kuonekana watu tofauti ili kuwaridhisha wengine wanakuwa na maisha yasiyo na uhuru. Hili linawafanya washindwe kuwa wao na hivyo kushindwa kufanya makubwa.
  5. Amejifunza na anaamini kwamba watu anaojihusisha nao wanapaswa kusema kile wanachokiamini na kuwa tayari kuwasikiliza wengine ili pia wajifunze na hilo ndiyo litawawezesha kuujua ukweli. Amejifunza kwamba chanzo kikuu cha matatizo kwenye jamii ni watu kuwa na kanuni au imani ambazo siyo sahihi na hawakubali kupokea mapingamizi au ukosoaji wa wengine, hivyo hawapati nafasi ya kuujua ukweli.
  6. Amejifunza kwamba kila mtu huwa anafanya makosa na kila mtu ana udhaifu kwenye eneo fulani. Kinachowasaidia wale wanaofanikiwa ni jinsi wanavyopokea makosa wanayofanya na kuchukua hatua kwenye madhaifu yao. Amejifunza kwamba ndani ya makosa kuna somo kubwa la kujifunza ambalo linakusaidia kujiwekea msingi sahihi. Unapokabiliana na makosa yako au ugumu wowote unaopitia, kunakufanya kuwa imara zaidi.
  7. Amejifunza kwamba picha maarufu ya mafanikio inayooneshwa na kutukuzwa na wengi siyo sahihi. Ile picha kwamba mtu aliyefanikiwa anakuwa mtu asiyekosea, aliyechukua hatua sahihi na kufanikiwa kwenye kila hatua siyo uhalisia. Ray amekutana na wengi waliofanikiwa sana, na kwa kila mmoja, amejifunza kwamba wana madhaifu na wanafanya makosa mengi. Kilichowawezesha kufanikiwa ni kuwa tayari kukabiliana na makosa wanayofanya na kuhakikisha madhaifu yao hayawi kikwazo kwao. Kwa kifupi Ray amejifunza kuwa mkweli hasa kuhusu makosa na madhaifu ndiyo njia kuu ya kuweza kupiga hatua.

Kupitia msingi wake wa kuwa mkweli kuhusu makosa na madhaifu, kumemfanya Ray aamini mambo tofauti na wengine, baadhi ya mambo hayo ni kama ifuatavyo;

  1. Wakati watu wengine wanaamini kujifunza yale wanayofundishwa ndiyo njia ya kufanikiwa, Ray anaamini kujifunza mwenyewe kupitia kujaribu na kukosea ndiyo mtu unaweza kujua nini hasa unataka na utawezaje kukipata.
  2. Wakati wengine wanaamini kwamba kuwa na majibu ni bora kuliko kuwa na maswali, Ray anaamini kwamba kuwa na maswali bora kunakuwezesha kuyapata majibu sahihi, hivyo maswali ni muhimu kuliko majibu.
  3. Wakati wengine wanaona makosa ni kitu kibaya, Ray anaamini makosa ni kitu kizuri, kinachokusukuma kujifunza, unapokosea na ukatafakari, unajifunza zaidi.
  4. Wakati wengine wanaamini kujua madhaifu yao ni kitu kibaya, Ray anaamini kujua madhaifu yako ni kitu kizuri, ni hatua ya kwanza ya kujua jinsi ya kukabiliana na madhaifu hayo na kutoruhusu yawe kikwazo kwako.
  5. Wakati wengine wanaamini maumivu ni kitu kibaya kinachopaswa kukwepwa, Ray anaamini maumivu ni kitu muhimu na kinachohitajika ili mtu aweze kuwa imara.

Rafiki, hii ni sehemu ndogo ya yale ambayo Ray Dalio ameweza kujifunza kutokana na makosa yake mwenyewe. Kuna misingi mingi ameshirikisha, kuanzia misingi ya kazi mpaka misingi ya maisha ambayo ukiijua na kuitumia itakusaidia sana.

Karibu ujiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA upate uchambuzi wa kitabu cha PRINCIPLES ili uweze kuijua misingi hiyo na kuitumia kwenye maisha yako. kujiunga na channel fungua kiungo kisha bonyeza JOIN CHANNEL, kiungo; https://www.t.me/somavitabutanzania

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania