Watu wengi hawajui msingi wa kisababishi na matokeo kwenye mafanikio.
Hivyo wamekuwa wanaweka juhudi zao kwenye visababishi tofauti na huku wakitegemea matokeo tofauti.
Mfano mtu anataka kufanikiwa, lakini anafikiri kitakachomfanya afanikiwe ni kuwasoma wale waliofanikiwa, au kuisoma misingi ya mafanikio. Hivyo kila mara analipa hilo kipaumbele.
Lakini kuwajua waliofanikiwa au kujua misingi ya mafanikio siyo kisababishi cha mafanikio. Ni vitu muhimu, lakini peke yake havitasababisha matokeo kwako. Ni lazima uchukue hatua fulani, ni lazima ufanye kitu ili kiweze kuzalisha matokeo ya tofauti na hapo ndipo utakapofanikiwa.
Wahenga walieleza hili kwa lugha rahisi kabisa, kwamba unavuna kile ulichopanda, na siyo ulichofikiri au kupanga kupanda, bali kile unachopanda. Huo ndiyo msingi mkuu wa kisababishi na matokeo, panda na utavuna.
Pia waliendelea kutuambia, ukipanda mahindi usitegemee kuvuna mtama. Ni sheria ya asili, kisababishi kinaleta matokeo, hivyo kupata matokeo sahihi, weka kisababishi sahihi. Unapata kuvuna mtama, panda mbegu za mtama, na siyo kupanda mbegu za mahindi na kutamani uvune mtama.
Hii ni kusema hivi rafiki, kama hujapata unachotaka, kama hujafika unakotaka kufika, basi sababu ni moja, hujaweka visababishi sahihi. Siku za nyuma umekuwa unachukua hatua ambazo siyo sahihi, umekuwa unapanda mahindi na kutegemea kuvuna mtama.
Hivyo basi, kama unataka kupata matokeo ya tofauti siku zijazo, tengeneza visababishi sahihi sasa. Panda mbegu sahihi leo, nyeshea mbegu hiyo, weka mbolea kwenye mche unaotokea, upalilie na endelea kuulinda mpaka utakapovuna kile ulichopanda.
Ukitaka kufanikiwa, fuata sheria za asili, hakuna awezaye kuvunja sheria hizi, kila kitu kinasababishwa hivyo kwa chochote unachotaka, anza na kisababishi sahihi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante Sana kocha umetukumbusha Jambo muhimu Sana hatua muhimu kuchukua kwa vitendo
LikeLike
Asante kocha , kwa maarifa haya ni kazi kwangu kuweka visababishi sahihi kulingana na malengo niliyo nayo.
LikeLike
Vizuri sana.
LikeLike