Mtu anayesema siogopi kufa anaweza kuwa ndiyo mwoga wa kifo kuliko wengine wote, kwa sababu kama kweli angekuwa haogopi kifo, angekipuuza, asingekitaja kabisa.

Kadhalika mtu anayewaambia wengine kwamba anataka kujiua, kuna kitu anataka kutoka kwa watu hao anaowaambia. Angekuwa kweli dhamira yake ni kujiua, angefanya hivyo kimya kimya, kwa sababu anajua akiwaambia wengine hawatakubaliana naye.

Sisi binadamu huwa hatupendi kuonesha madhaifu yetu, hivyo huwa tunakazana kuyaficha madhaifu tuliyonayo kwa kuonesha kinyume chake.

Mtu asiyejiamini ndiyo anaonesha kujiamini sana kwa nje.

Asiyejua ndiye anayeongea sana.

Masikini huhangaika na vitu vya kifahari kuliko matajiri.

Hali hii huwa inakuja kwa asili, bila hata ya mtu kuchagua, unajikuta tu kuna hatua unachochukua, lakini lengo ni kuficha udhaifu uliopo ndani yako.

Hili lina mambo mawili muhimu ya kujifunza;

Tunapowaangalia wengine, tunapaswa kujua kile wanachokazana kuonesha ndiyo ambacho hawana. Hivyo kama tunahitaji kufanya maamuzi, tunapaswa kutumia kinyume cha yale ambayo mtu anakazana kuonesha.

Jambo la pili ni kwetu wenyewe, tusihangaike sana na madhaifu yetu na kujaribu kuyaficha, badala yake tuweke jitihada kwenye uimara wetu na kuutumia kufanya makubwa zaidi. Nguvu unazopeleka kwenye kuficha madhaifu yako ukizipeleka kwenye uimara wako utaweza kufanya makubwa. Achana na maisha ya maigizo, ishi uhalisia wako na utakuwa na maisha tulivu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha