Vitu rahisi kufanya havina thamani kubwa, hata kama vinatumia nguvu kubwa. Vitu vyenye thamani kubwa ni vile ambavyo ni vigumu kufanya.
Chukulia kazi mbili, upasuaji wa ubongo na ubebaji wa mizigo sokoni. Ni kazi ipo inatumia nguvu nyingi kufanya? Jibu liko wazi, ni kubeba mizigo sokoni. Lakini ni ipi ngumu kufanya, upasuaji wa ubongo. Karibu kila mtu anaweza kubeba mizigo sokoni, lakini ni wachache sana wanaoweza kufanya upasuaji wa ubongo. Ndiyo maana wanaofanya upasuaji wa ubongo wanalipwa mara 100 ya kile anacholipwa mbebaji wa mizigo sokoni.
Kuna vitu vitatu ambavyo ni vigumu sana kwako kuvifanya, lakini ukiweza kuvifanya vina thamani kubwa mno. Vitu hivi vinahusisha maisha ya kila siku, siyo watu wengi wanaoweza kuvifanya, ndiyo maana thamani yake inakuwa kubwa sana.
Kitu cha kwanza ni kujibu chuki kwa upendo.
Hebu fikiria, mtu amekufanyia ubaya, lakini wewe unamjibu kwa wema, unamjibu kwa upendo. Ni zoezi gumu, kwa sababu kwa asili, tunapenda kulipa ubaya kwa ubaya, hatupendi watu watuonee, hivyo tunapenda kuwaonesha kwamba hawawezi kutufanyia wanavyojisikia wao.
Lakini jiulize, unapojibu ubaya kwa ubaya nani anakuwa ameshinda? Aliyeshinda ni yule aliyeanzisha ubaya, kwa sababu ameweza kukupeleka kwenye ubaya.
Lakini pata picha mtu amekufanyia ubaya ukamjibu kwa wema, anakuchukia wewe ukampenda, nani anayeshinda? Ni wewe, yule aliyefanya ubaya au chuki, matendo yake mwenyewe yatamuumiza kuliko unavyoumia wewe.
Kitu cha pili ni kuwajumuisha waliotengwa.
Kwenye jamii kuna watu mbalimbali ambao wametengwa na mifumo mbalimbali. Wewe unapochukua hatua ya kuwajumuisha wale waliotengwa siyo tu unawanufaisha, lakini pia unaweza kupata watu ambao ni bora.
Wale watu ambao wanaonekana hawafai, ambao hawana mtetezi, wamekubali hukumu waliyopewa na jamii, unapoona kitu kikubwa ndani yao na kuwapa nafasi, huwa wanakuwa watu bora sana.
Kitu cha tatu ni kukubali umekosea.
Jamii yetu imekuwa inaadhibu makosa, tangu ukiwa mdogo ulikuwa unaadhibiwa unapokosea, ukaenda shule na mwendelezo ukawa huo, ukikosea adhabu. Umeenda kwenye kazi na mambo ni hayo hayo, ukikosea ni adhabu.
Hivyo kila mtu anahusisha makosa na adhabu kali, hivyo wajibu wa kwanza wa kila mtu ni kuhakikisha hakosei na akikosea basi analikataa kosa au kuwasingizia wengine.
Lakini hakuna anayeweza kupiga hatua bila kupiga makosa, na hakuna anayejifunza bila kukiri makosa. Hivyo kuwa tayari kukubali kwamba umekosea, kunakupa nafasi ya wewe kujifunza na kuwa bora zaidi.
Kukiri makosa kunahitaji ujasiri wa hali ya juu, kwa sababu kila mtu atakuchukulia mzembe na usiyejali, lakini manufaa utakayopata ni makubwa.
Wapende wanaokuchukia, wajumuishe waliotengwa na kubali umekosea, ukiweza kuyafanya haya matatu, utapata manufaa makubwa sana.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Ahsante kwa mambo haya matatu ya kufanya kila siku.
LikeLike
Asante sana , kocha kwa mambo hayo matatu magumu yenye kuleta thamani kubwa. Kazi kwangu kulipa ubaya kwa wema ,kuwajumuisha waliotengwa na kukubali pale ninapokosea na kujua hatua ya kujifunza zaidi
LikeLike