Kanuni halisi za mafanikio zinaendana na kanuni za asili.

Moja ya kanuni za asili ni kabla kitu hakijatumiwa, lazima kitengenezwe kwanza.

Vitu huwa havitokei tu, vinafanyiwa kazi, vinatengenezwa kisha ndiyo vinatumiwa.

Simba huwa halali tu halafu swala akajileta mwenyewe, anakwenda kuwinda mpaka anampata swala ndipo anakula. Asipowinda hapati swala na hivyo hali.

Chanzo cha matatizo mengi tunayopitia kwenye maisha ni kutumia kabla ya kutengeneza. Tunataka kula kabla hatujazalisha au kuwinda.

Na kinachotokea ni tunakula vya wengine na hivyo kuwa watumwa kwao daima.

Chukulia mfano rahisi kwenye fedha, unapaswa kutengeneza fedha kwanza kabla hujazitumia. Kutoa thamani kisha ukalipwa fedha na hapo ukaenda kuitumia.

Lakini angalia wale wenye matatizo ya kifedha ni nini wanafanya. Wanatumia kwanza kabla hawajatengeneza. Wanatumia pesa ambazo hawajapata bado na hivyo wanatengeneza madeni. Kinachotokea ni watu hao kuwa watumwa wa madeni kwa kipindi kirefu.

Unapotengeneza kabla ya kutumia unakuwa umetoa mchango wako kwa dunia na hivyo unakuwa unaidai. Unapotumia kabla ya kutengeneza unakuwa umechukua kwenye dunia na hivyo inakudai. Ogopa sana kudaiwa na dunia, huwi na maisha huru.

Tengeneza kabla ya kutumia, ni msingi mzuri utakaokujengea uhuru mkubwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha