Karibu rafiki kwenye makala ya ushauri wa changamoto mbalimbali ambazo zinakuwa kikwazo kwako kufikia mafanikio makubwa.

Kama ambavyo nimekuwa nasisitiza, changamoto siyo mwisho wa safari ya mafanikio, bali ndiyo vitu vinavyokuwezesha kufika kule unakotaka kufika.

Leo tunakwenda kupata ushauri wa jinsi ya kumshawishi mwenza wako kujijengea tabia ya kujisomea.

kusoma pamoja.jpg

Kabla hatujaangalia ni jinsi gani unaweza kufanya hivyo, tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyeomba ushauri kwenye hili.

Napata changamoto namna ya kumshawishi mke wangu kupenda kusoma vitabu na kuchukua hatua kama mimi, sijui nifanyeje? – Ramadhani O. S.

Hii ni changamoto inayowakumba wengi ambao wanabadili tabia zao lakini wenza wao au watu wengine wa karibu wanabaki na tabia za awali.

Hivyo wengi hutamani sana kuweza kuwabadili wenzao ili waweze kwenda pamoja, lakini huwa linakuwa ni zoezi gumu sana.

Kabla hatujaangalia unawezaje kumshawishi mwenza wako kujenga tabia ya kujisomea, kwanza nikushirikishe mambo muhimu unayopaswa kujua kuhusu tabia.

  1. Tabia ni kitu ambacho kinajengwa kwa muda mrefu, na hata kuvunja inahitaji muda mrefu.
  2. Huwezi kumlazimisha mtu kubadili tabia yake, tena kadiri unavyomlazimisha, ndivyo anavyozidi kufanya tabia ambayo unataka aache.
  3. Mabadiliko pekee ya tabia yanaweza kuanzia ndani ya mtu, kwa ridhaa yake na kuona umuhimu wa mabadiliko. Nguvu ya nje haiwezi kumbadili mtu ambaye hajakubali ndani yake

Kwa kujua hayo muhimu kuhusu tabia, tunatambua kwamba kitu pekee tunachoweza kufanya kwa wengine, ni kuwashawishi kwa kuwaonesha umuhimu wa tabia fulani, halafu wao wenyewe waridhie na kuchukua hatua.

Zifuatazo ni baadhi ya njia unazoweza kutumia kumshawishi mwenza wako ajijengee tabia ya kusoma.

Moja; badili mazingira ya nyumbani yahamasishe usomaji.

Mazingira yana nguvu kubwa sana ya kubadili tabia. Tafiti zimekuwa zinaonesha kwamba mara nyingi huwa tunafanya mambo siyo kwa sababu tumepanga, bali kwa sababu yapo kwenye mazingira.

Kwenye nyumba nyingi, TV ipo sebuleni na ni rahisi kila mtu kuwasha na kuangalia. Hivyo mtu anapokuwa amekaa na hana cha kufanya, anaishia kuwasha tv na kuangalia.

Unaweza kubadili mazingira hayo ya nyumbani, kwa kuweka maktaba ndogo sebuleni au karibu na tv. Pembeni ya tv, weka shelfu la vitabu na vitabu vipangiliwe kwa namna ambayo ni rahisi mtu kuona na kuvutiwa kuchukua kusoma.

Uwepo wa vitabu eneo ambalo kila mtu anaona kwa urahisi linachochea mtu kujijengea tabia ya kusoma vitabu.

SOMA; Je Una Tv Nyumbani Kwako? Soma Hapa Ujue Jinsi Ya Kuitumia Kuongeza Kipato Chako Zaidi.

Mbili; tenga muda wa kusoma kwa pamoja.

Ni vigumu mtu kufanya kitu kipya mwenyewe kama hana msukumo mkubwa ndani yake. Lakini anapokuwa anafanya na mtu mwingine, inakuwa rahisi, kwa sababu hataki kumwangusha mtu huyo.

Pangeni muda wa kusoma pamoja, kitabu kimoja. Unaweza kuwa nusu saa au saa moja, kulingana na nafasi yenu na inaweza kuwa asubuhi mapema mnapoamka au usiku kabla hamjalala. Pia mnaweza kuchagua kusoma kurasa chache na kujadiliana mlichoelewa kwenye kurasa hizo.

Kwa hatua hii, kidogo kidogo mwenzako anaanza kujenga mapenzi na usomaji wa vitabu.

Tatu; jua ni mambo gani anapendelea na mtafutie vitabu vinavyohusu mambo hayo.

Kila mtu kuna kitu fulani ambacho anakipendelea, anapenda kufuatilia, kuzungumzia na hata kujifunza zaidi. Jua hilo kwa mwenza wako kisha mtafutie vitabu vinavyoendana na kile ambacho anakipenda.

Unaweza kupitia kitabu kabla ya kumpatia na kumpa sifa za kitabu hicho na kwa nini atakipenda au kitamfaa. Kwa njia hii mwenza wako atavutiwa kusoma kitabu hicho, na akishaanza kimoja, kazi ni kwako kumtafutia vitabu vingine zaidi ili tabia hiyo iendelee.

Nne; jua changamoto anazopitia na mpe vitabu sahihi.

Uzuri wa vitabu ni kwamba, kila changamoto ambayo mtu unapitia sasa, mtu mwingine alishaipitia na akaiandika kwenye kitabu. Au kuna watu wamefanya tafiti na kuja na njia sahihi za kutatua changamoto hiyo.

Na kila mmoja wetu kuna changamoto fulani ambayo anayo, inaweza kuwa changamoto binafsi, changamoto za kikazi, kibiashara na nyinginezo.

Jua changamoto ambazo mwenza wako anapitia, kisha tafuta vitabu sahihi vitakavyomsaidia kutatua changamoto hizo na mshawishi avisome. Hapa pia pitia kitabu na upate mwanga, kisha mwambie ni jinsi gani kitabu kinaelezea utatuzi wa changamoto yake.

Mshawishi asome kitabu na baadaye mjadiliane hatua za kuchukua ili aweze kutata changamoto anayopitia. Kwa kufanya hivi, utaweza kumshawishi mwenza wako kujenga tabia ya kusoma vitabu.

SOMA; Hatua Nne Za Kujijengea Tabia Ya Kujisomea Ambayo Itakuwa Na Manufaa Makubwa Kwako.

Tano; nendeni pamoja kwenye mambo yanayohusu vitabu au kujifunza.

Badala ya kwenda peke yako na kumletea mwenzako taarifa, jitahidi kwenda naye kwenye maeneo yanayohusu vitabu au kujifunza. Mfano kama kuna klabu ya usomaji vitabu, basi nenda naye. Kama kuna semina au mafunzo yanayohusu vitabu na mambo mengine ya mafanikio basi nenda naye. Na kama unaenda kwenye duka la vitabu pia nenda naye.

Kuna nguvu fulani huwa ipo kwenye tukio husika, ambapo mtu anayehudhuria anaipata nguvu hiyo na kuhamasika kuliko ambaye hajahudhuria. Ukienda na mtu kwenye duka la vitabu, akaanza kuperuzi vitabu mbalimbali, atakutana na kitabu kizuri kwake na kuchagua kukinunua. Akishakinunua onesha shauku ya kutaka kujifunza kutoka kwake kuhusu kitabu alichonunua, na hapo atapata msukumo wa kukisoma ili akushirikishe.

Hizo ndiyo baadhi ya njia unazoweza kutumia kumshawishi mwenza wako kujijengea tabia ya usomaji vitabu. Kumbuka hili ni jambo ambalo linahitaji muda na uvumilivu, mtu amekaa miaka zaidi ya 20 bila ya usomaji wa vitabu, usitegemee awe msomaji ndani ya mwezi mmoja. Kidogo kidogo na kwa kutumia kila fursa inayojitokeza, mtu anaweza kubadilika na baada ya muda akawa msomaji mzuri.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania

WhatsApp Image 2019-07-13 at 18.40.49
Soma uchambuzi wa vitabu 50 ndani ya kitabu hiki cha TANO ZA MAJUMA 50 YA MWAKA, piga simu 0678 977 007 kupata kitabu hiki.