Kuna mambo mengi hayaendi sawa duniani, nchini, kwenye jamii, kwenye kazi na hata kwenye familia yako.
Mengi kati ya hayo yapo kabisa nje ya uwezo wako, hakuna namna unaweza kuyaathiri moja kwa moja.
Na hivyo unabaki ukilalamika kuhusu mambo yanavyokwenda, ambapo siyo sawa.
Kitu unachopaswa kujua ni kwamba, kulalamika hakujawahi kufanya kitu chochote kuwa bora.
Bali kuchukua hatua ndiyo kunaweza kufanya vitu bora.
Hapo ulipo, kuna hatua unaweza kuchukua na ikawa na mchango kwa yale yanayoendelea, hata kama siyo wa moja kwa moja.
Fanya kitu chanya, ambacho ni kinyume na yale yanayoendelea, na utawashawishi wengine wanaokuzunguka kufanya kitu chanya, kidogo kidogo unakuwa umeleta mchango bora kwa wengine.
Tafuta kona yako ambayo unaweza kufanya mazuri, kona unayoweza kuleta tofauti kwenye maisha ya wengine, kisha weka nguvu zako kwenye kuchukua hatua eneo hilo.
Usipoteze muda wala nguvu kulalamika, badala yake angalia ni kipi unachoweza kufanya na kifanye, matokeo yake hata kama ni madogo yatakuwa na manufaa kuliko malalamiko.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,