Mpendwa rafiki yangu,
Huwa wazazi wanaamini kuwa wakishampa mtoto mahitaji yake muhimu basi wamemaliza kazi. Kumbe, unaweza kumpa mtoto mahitaji yote muhimu lakini bado unakuwa hujamaliza kazi.
Malezi kwa mtoto ni kama vile kitendo cha kuoga, huwezi kusema unaoga kwa siku moja na ukasema umemaliza kazi. Hata malezi nayo yako hivyo hivyo, ni kitendo endelevu.
Mzazi anaamini kuwa akishamlipia mtoto wake ada, basi kuhusu mambo ya shule amemaliza kazi, anamwachia mwalimu kila kitu ndiyo ashughulike na mtoto wako.
Wako wazazi ambao hawana muda wa kukagua madaftari ya watoto wao, hata kufanya nao kazi za nyumbani hawajawahi. Mtoto anakuwa anajiongoza mwenyewe bila mwelekeo mpaka mzazi anakuja kushtuka mtoto ameshaharibika.
Kumpatia mtoto mahitaji yake muhimu hilo ni jukumu lako wewe kama mzazi, hupaswi kumlalamikia mtoto kwa yale mazuri unayomfanyia hapo unatimiza wajibu wako kama mzazi.
Mtoto afanye vizuri au vibaya huwezi kumkataa bali unaalikwa kumpokea kadiri ya matokeo yake.
Zawadi ambayo watoto wanakosa kutoka kwa wazazi wao zama hizi ni zawadi ya kufuatiliwa. Watoto wengi siku hizi hawafuatiliwi na wazazi wao na watoto wakishajua hawafuatiliwi wanakuwa huru kufanya kile wanachotaka.
Mtoto anakuwa makini na kuacha kufanya uzembe pale anapojua kuwa kuna mtu nyuma yake anayemfuatilia. Hivyo anakuwa makini kwa kila anachofanya, hata watu wazima wanafanya vizuri pale wanapokuwa na mtu anayewafuatilia kwa undani hatua kwa hatua.
Wajengee watoto msingi mapema, kama mtoto akienda shule akirudi fuatilia alienda shule kusoma nini, usiwe mzazi wa kukubali kila unachoambiwa na mtoto kwa mdomo tu,bali kuwa mtu wa kuhakikisha na ukifanya hivyo utamjengea umakini katika kile anachofanya.
Kwa mfano, wako watoto ambao wanaomba fedha za matumizi kwa wazazi wao na wazazi wanapa kweli lakini wanakosea kitu kimoja ambacho ni kumfuatilia yale matumizi ya fedha aliyoomba. Mjengee mtoto utaratibu kuwa kiais cha fedha unayompa mwambie akupe mchanganuo wa matumizi hayo, kama ni elfu Kumi , basi akupe mchanganuo wa matumizi wa hiyo elfu kumi imetumikaje.
Hapa utakua unamfundisha mtoto msingi muhimu wa fedha na kuwa na nidhamu ya fedha.
Hata mtoto ambaye anakuomba ruhusa ya kwenda sehemu fulani fuatilia je ruhusa aliyoomba amekwenda sehemu husika. Ukiwa unachukulia poa juu ya mambo madogo kama haya unakuta mtoto anatumia muda huo kufanya yale ambayo siyo.
Kumfuatilia mtoto ni kumpenda na kumjali. Unapomuacha bila kumfuatilia hata yeye mwenyewe anajiona kuwa humjali wala humthamini na kama unavyojua hitaji la kwanza la kila binadamu ni kuhisi anathaminiwa.
Hatua ya kuchukua leo; Kuwa mtu wa kumfuatilia mtoto wako kwa kila jambo, fuatilia mienendo yake, tabia na hata makuzi, marafiki, vitu anavyopenda na vile ambavyo havipendi.
Kazi yoyote unayompa ifuatilie kama ameifanya vile inavyotakiwa kufanywa.
Usiwe mtu wa kukubali kwa mdomo kila unachoambiwa na mtoto bali fuatilia na hakikisha.
Kwahiyo, mtoto ni malezi, malezi ni pamoja na ufuatiliaji wa mtoto hatua kwa hatua kadiri ya mtoto anavyokuwa.
Kuna mambo mengi huwa yanaenda ndivyo sivyo kwa mtoto wako kwa sababu ya kukosa ufuatiliaji, mtoto bila ufuatiliaji utampoteza bila kujua.
Kila la heri rafiki yangu.
Rafiki na mwalimu wako,
Mwl. Deogratius Kessy
0717101505//0767101504
deokessy.dk@gmail.com
kessy@ustoa.or.tz
Au unaweza kutembelea blog yake kujifunza zaidi
http://kessydeo.home.blog
Karibu sana na
Asante sana.