Kama unataka kufanya maamuzi sahihi kwenye maisha yako, badili muda ambao unaotumia katika kufanya maamuzi yako.
Badala ya kuangalia dakika 10 zijazo au siku moja ijayo, anza kwa kuangalia miaka kumi ijayo.
Kabla hujaafikia kufanya kitu chochote kile, jiulize kama utaendelea kukifanya, je miaka kumi ijayo maisha yako yatakuwa wapi.
Wale ambao wanajikuta kwenye magonjwa, umasikini, madeni na tabia nyingine zinazowarudisha nyuma, siyo kwa sababu waliamka ghafla na kujikuta kwenye tabia hizo, bali kuna maamuzi madogo madogo ambayo wamekuwa wanayafanya kila siku na sasa yamewafikisha walipofika sasa.
Mtu anaanza na maamuzi madogo, ambayo hayana madhara yoyote pale anapoanza, na pia yanampa raha kwa muda huo. Lakini miaka mingi baadaye anajikuta yupo kwenye shimo ambalo anatamani kutoka lakini hawezi.
Angalia waliopo kwenye madeni, ni maamuzi madogo madogo ya miaka mingi yamewafikisha pale. Waliona ni sahihi kuwa na matumizi makubwa kuliko mapato kwa wakati fulani, lakini hawakuangalia mbali. Mpaka wanapokuja kujikuta wamenasa kwenye madeni.
Angalia walio kwenye ulevi na uteja, siku wanatumia kilevi kwa mara ya kwanza hawakuangalia miaka mingi inayokuja, wao waliangalia raha ya muda mfupi.
Anza zoezi hili la kuangalia miaka mingi ijayo, kiwango cha chini miaka 10 na hakikisha hufanyi kitu ambacho kitaharibu miaka yako ijayo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kweli natakiwa kubadili muda ambao ninafanya maamuzi kwenye maisha yangu.
LikeLike