Kwa kutumia akili peke yake au nguvu peke yake, unaweza kufika asilimia 90 ya mafanikio yako.
Lakini ukitumia vyote kwa pamoja, yaani akili na nguvu, unafika kwenye asilimia 99 ya mafanikio yako.
Utawasikia wengi wakisema usitumie nguvu, tumia akili, lakini hawa siyo wale wanaofikia mafanikio makubwa, wanaweza kuwa na mafanikio ya kawaida, lakini siyo yale makubwa kabisa.
Mafanikio makubwa yanakutaka uwekeze vitu hivyo viwili ndiyo uweze kupata matokeo bora.
Lakini wapo wanaotumia vyote viwili na hawapati mafanikio makubwa, kwa sababu hawavitumii kwa mpangilio sahihi.
Wengi huanza na nguvu, halafu wakishashindwa ndiyo wanaweka akili.
Wewe unapaswa kuanza na akili, kisha kuweka nguvu kutekeleza yale ambayo akili imeafikia.
Kama umekutana na tatizo au changamoto, kabla hujakimbilia kuweka nguvu kutatua, jipe muda wa kufikiri na kutafakari kwa kina kuhusu changamoto au tatizo ulilokutana nalo. Jua kwa undani, jua mzizi wake na jua wapi ukiweka nguvu sahihi matokeo yatakuwa makubwa, kisha weka nguvu kwenye eneo hilo.
Akili yako ndiyo rasilimali kubwa uliyonayo, anza kuituma kwanza kisha weka nguvu katika kutekeleza maamuzi uliyofikia kwa kufikiri kwa usahihi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,