“If you haven’t read hundreds of books, you are functionally illiterate, and you will be incompetent, because your personal experiences alone aren’t broad enough to sustain you.” ― Jim Mattis

James Norman Mattis (kuzaliwa Septemba 8, 1950) ni jenerali mstaafu wa jeshi la maji na anga la Marekani. Katika maisha yake ya uanajeshi na uongozi aliweza kushiriki kwenye vita mbalimbali, ikiwepo vita kubwa kama Vita ya Persian Gulf, vita ya Afghanistan, na vita ya Iraq. Pia amewahi kupata nafasi ya kuwa katibu mkuu wa wizara ya ulinzi wa Marekani kuanzia Januari 2017 mpaka Januari 2019.

James ana kitu kimoja ambacho anasema kimemsaidia sana kwenye maisha yake kama mwanajeshi na Jenerali aliyeweza kushiriki na kushinda vita nyingi. Kitu hicho ni usomaji wa vitabu.

knowledge is power.jpg

Kwenye moja ya barua pepe zake kwa wanajeshi wenzake, James aliwahi kuandika hivi; “Binadamu tumekuwa tunapigana vita kwa zaidi ya miaka 5,000 sasa, hivyo tunapaswa kutumia uzoefu huo kwenye vita tunazopigana.  Kutumia mazoea na uzoefu binafsi huku tukirudia makosa ambayo yalishafanywa huko nyumba, ni kujipa gharama na maumivu makubwa.”

Rafiki, naamini sasa unapata picha ya kichwa cha makala hii, kwamba kama hujasoma mamia ya vitabu basi wewe ni mjinga. Na u mjinga kwa sababu kwa chochote unachofanya, unarudia makosa ambayo watu wengine walishayafanya huko nyuma, wakajifunza na kisha wakaandika kitabu cha jinsi ya kuepuka makosa yako.

Wajibu wako wewe ni kujifunza kupitia makosa ambayo wengine walishayafanya huko nyuma na kuhakikisha hurudii makosa yao ili uweze kupata matokeo ambayo ni bora zaidi.

Albert Einstein amewahi kunukuliwa akisema ujinga ni kufanya jambo lile lile kwa njia zile zile halafu kutegemea kupata matokeo tofauti.

Otto von Bismarck amewahi kusema; “Ni mpumbavu pekee anayejifunza kwa makosa yake mwenyewe. Mwenye hekima hujifunza kutokana na makosa ya wengine.”

Njia rahisi na ya uhakika ya wewe kujifunza kutokana na makosa na uzoefu wa wengine, ni kusoma vitabu.

Na ni jambo la kushukuru sana kwamba zama tunazoishi sasa, ni zama ambazo upatikanaji wa vitabu umekuwa rahisi sana, huhitaji kwenda maktaba ndiyo upate vitabu, na wala huhitaji fedha nyingi ndiyo uweze kununua vitabu.

Simu yako ya mkononi ni maktaba tosha, inaweza kubeba mamia mpaka maelfu ya vitabu. Unaweza kupata vitabu vingi bure kabisa na vingine vizuri utalipia gharama ndogo kuvipata.

Nina swali kwako rafiki yangu, je umeshasoma mamia ya vitabu? Na kama jibu ni hapana, kwa nini unaendelea kung’ang’ana na ujinga?

Niambie changamoto yoyote unayokabiliana nayo sasa, na kuna mamia ya vitabu vinavuyoeleza jinsi ya kutatua changamoto hiyo.

Una changamoto ya kipato, unachoingiza hakitoshelezi na upo kwenye madeni, kuna vitabu vingi mno vya kukufundisha jinsi ya kuongeza kipato chako, kudhibiti matumizi yako, kuondoka kwenye madeni, kuweka akiba na kuwekeza.

Mahusiano yako ya ndoa yana changamoto kubwa inayokukosesha utulivu kwenye maisha. Kuna vitabu vingi mno ambavyo vimefundisha kuhusu changamoto za mahusiano, zikieleza tofauti baina ya jinsia mbili na jinsi ya kuzitumia kufikia makubaliano mazuri. Kwa nini wewe unaendelea kujaribu na kurudia makosa ambayo majibu yake yapo?

Una biashara ambayo inakupa changamoto, haikui licha ya kujituma sana, kufanya kazi usiku na mchana na kukosa kabisa maisha mengine. Vitabu vingi vimeandikwa kwenye eneo la biashara, kuanzia upande wa masoko, mauzo, fedha, rasilimali watu na uongozi na usimamizi. Kuna maarifa mengi na yaliyofanyiwa tafiti ya jinsi ya kuendesha biashara yenye mafanikio. Lakini wewe unafikiri una akili kuliko vitabu vyote ambavyo vimeandikwa, unajaribu makosa ambayo wengine walishafanya, halafu unashangaa kwa nini hufanikiwi!

Rafiki, ni wakati sasa wa kuamua kuachana na ujinga, ni wakati sasa wa kuacha kurudia makosa ambayo wengine walishafanya, wakayatatua na kuweka majibu yake kwenye vitabu mbalimbali ambavyo wameandika.

Ni wakati sasa wa kujenga tabia ya kujisomea vitabu, uweze kusoma mamia ya vitabu, upate maarifa sahihi na uyatumie kufanya maamuzi sahihi ili kuweza kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako.

Kama hujui wapi unaweza kupata vitabu vizuri vya kusoma, nikukaribishe ujiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA (https://www.t.me/somavitabutanzania), kwa kujiunga na channel hii, utapata mamia ya vitabu pamoja na chambuzi zake. Yaani hata kama huelewi lugha ya Kiingereza ambayo ndiyo vitabu vingi vimeandikwa kwa lugha hiyo, hata kama huna muda wa kusoma vitabu vingi na virefu, chambuzi utakazozipata kwenye channel hii, zitakufanya uwe sawa na aliyesoma kitabu husika.

Mfano kitabu cha ATLAS SHRUGGED (ambacho kinaonesha mapambano kati ya nguvu na akili, ambapo akili inashinda) kina kurasa zaidi ya elfu moja na mia mbili, lakini uchambuzi wake una kurasa zisizozidi 50, ambao umeshiba kwelikweli, umechambua yale mambo muhimu unayopaswa kujifunza kwenye kitabu hicho pamoja na hatua za kuchukua ili uwe bora kabisa.

Karibu ujiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA, kwa kufungua https://www.t.me/somavitabutanzania kisha kubonyeza JOIN CHANNEL na twende pamoja kwenye safari hii ya kutokomeza ujinga wetu kupitia usomaji wa mamia ya vitabu na kujifunza kutoka kwenye uzoefu wa wengine ili tusirudie makosa yao.

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania