Kuwa makini sana na kile unachokitegemea kwenye maisha yako, maana unakipa nguvu kubwa kwenye maisha yako.

Chochote kile unachokitegemea ndiyo kinachoyatawala maisha yako.

Kile unachotegemea kikuinue na kukupandisha juu, ndiyo hicho kicho kitakachokushusha na kukuangusha.

Kama upendeleo wa wengine ndiyo umekupandisha wewe juu, jua pia upendeleo huo utakapoondolewa ndicho kitakachokuangusha chini.

Na kama uwezo wako ndiyo umekupandisha, uwezo huo huo utakushusha kama utaacha kuutumia au kushindwa kuuendeleza.

Kwa upande mwingine, kinachowaleta watu kwako ndiyo pia kitakachowaondoa.

Kama watu wamekuja kwako kwa sababu ni maarufu, pale umaarufu unapoisha wanaondoka. Kama walikuja kwa sababu ya fedha, zikiisha hutawaona tena.

Kadhalika, kama wateja wamekuja kwenye biashara yako kwa sababu una bei rahisi, bei hiyo rahisi ndiyo itawaondoka kwako pia. Utakapopandisha bei au akitokea mwingine mwenye bei rahisi kuliko wewe, watakuhama.

Nakukumbusha haya rafiki yangu ili uache kuwalaumu wengine na uchukue hatua sahihi.

Usilaumu wengine kwamba wanakuangusha, jua wewe ndiyo umewapa nguvu ya kufanya hivyo kwa kuwaruhusu wakupandishe. Hivyo kama hutaki yeyote awe na nguvu ya kukuangusha, hakikisha hakuna uliyempa nguvu ya kukuinua.

Usilalamike pale watu wanapokuacha kwa sababu kitu fulani ulichokuwa nacho huna tena. Utasikia mtu anasema alikuwa na marafiki alipokuwa na fedha ila fedha zimeisha hawaoni tena marafiki hao. Kabla hujalalamikia hali kama hiyo, jua kilichowavutia watu hao kuja kwako hakipo tena, unategemea wabaki kwako kufana nini?

Ukielewa msingi huu muhimu, utajiepusha na mengi sana kwenye maisha yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha