Ipo kauli kwamba kama umepotea njia, kuongeza mwendo kunakufanya uzidi kupotea na siyo kufika unakotaka kufika.
Hivyo basi, jukumu lako la kwanza kabla hujaongeza mwendo ni kuhakikisha kwamba upo kwenye njia sahihi.
Kuna malengo mengi ambayo huwa tunajiwekea kwenye maisha, kisha tunapambana kweli kuyafikia, lakini tunapoyakamilisha malengo hayo, ndiyo tunagundua kwamba siyo tulichokuwa tunataka. Matokeo tunayopata yanakuwa kinyume kabisa na matarajio yetu.
Kwa namna hii, ushindi uliopambana sana kuufikia, unageuka kuwa kushindwa. Kwa sababu muda uliowekeza kwenye kupata ushindi huo, ni muda ambao huwezi kuupata tena na ukautumia kwenye kile kilicho sahihi.
Kwenye safari yako ya mafanikio, unataka kupata ushindi wa kweli na siyo ushindi ambao unageuka kuwa kushindwa.
Na njia pekee ya kupata ushindi huo ni kuhakikisha kile unachofanyia kazi ndiyo unachokitaka kweli, ndiyo chenye maana kwako na unakijali. Hakikisha hufanyi kwa sababu wengine wanafanya au kwa sababu ndivyo wengine wanataka wewe ufanye.
Unapaswa kuwa makini sana kwenye hili, kwa sababu siyo rahisi kuona kama wengine wanakusukuma kufanya vitu fulani, unaweza kuona umeamua mwenyewe, lakini kumbe kuna ushawishi wa wengine. Hivyo unapambana na unapofika mwisho ndiyo unagundua umepoteza.
Njia nyingine ya kutambua mapema ushindi ambao utakuwa kushindwa kwako, waulize wale ambao wameshapata unachotafuta wewe, kisha waulize mtazamo waliokuwa nao kabla hawajapata na mtazamo walio nao baada ya kupata. Hapa utajifunza kitu kikubwa sana, utaona wengi walifikiri kupata kitu hicho basi maisha yao yatakuwa yamekamilika, lakini baada ya kukipata wanagundua bado maisha yao hayajakamilika.
Chochote unachotaka na unachopambana kukipata kwenye maisha yako, kwanza jua siyo mwisho wa kila kitu, kupata chochote hakukamilishi maisha yako. Hivyo pambana kupata kile unachojali kweli, kwa sababu hata baada ya kukipata, utahitaji kuendelea kutafuta vingine zaidi. Maisha yako hayakamiliki mpaka siku unapokufa, hivyo usiyapoteze kwa mambo yasiyokuwa na umuhimu au maana kwako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Shukrani kocha kwa ukweli huu.
LikeLike