Rafiki yangu mpendwa,

Tumekuwa tunaona watu wanafanya maovu makubwa hapa duniani mpaka tunajiuliza nini kinawasukuma kufanya hivyo.

Tunajaribu kuelewa msukumo wao wa kufanya maovu hayo lakini hatupati majibu.

Mifano ipo mingi sana, lakini mkubwa na ambao umekuwa unajirudia rudia mara nyingi ni pale mtu anapokuwa chini au hana mafanikio anaonekana ni mwema.

Lakini mtu huyo huyo anapopanda juu, labda kupata nafasi ya uongozi au madaraka au akapata mafanikio fulani, anabadilika na kuwa mtu mkatili, asiyejali na anayewasumbua na kuwanyanyasa wengine.

watu feki.jpg

Ayn Rand kupitia kitabu chake cha The Fountainhead ametuonesha kwa nini baadhi ya watu wamekuwa waovu.

Anasema sababu kubwa ni kwamba watu hawa ni FEKI akiwapa jina Second-handers. Anaeleza kwamba watu hawa wameacha kufikiri kwa akili zao na wanafanya kile wengine wanafanya, wameacha kuishi ndoto na maono yao na wanafanya kile ambacho wengine wanafanya au kitawapa umaarufu.

Rand ambaye falsafa yake ilisimamia sana uwezo wa mtu binafsi na umuhimu wa kutumia fikra aliamini mtu akishaacha kujali uwezo wake na kuacha kutumia fikra zake, ndiyo chanzo kikuu cha maovu hapa duniani.

Wale tunaowaona wanaiba, kutapeli, kufisadi, kutesa wengine na kunyang’anya ni kwa sababu wameamua kuzika uwezo mkubwa ulio ndani yao na kuacha kabisa kufikiri kwa akili zao. Wamemezwa na fikra za kundi na kuiga kile ambacho wengine wanafanya.

SOMA; Uchambuzi Wa Kitabu The Fountainhead (Jinsi Ya Kuishi Maisha Ya Ndoto Yako Licha Ya Kupingwa Na Jamii).

Hotuba ya Howard Roark kuhusu watu feki.

Hapa nakwenda kukupa kipande cha mazungumzo kati ya wahusika wawili kwenye riwaya ya Fountainhead ambao Rand aliwatumia kufikisha ujumbe huu kuhusu watu feki. Kupata uchambuzi kamili wa kitabu hiki ambao una mengi sana kwako kujifunza ili kuwa na maisha huru, fungua; www.t.me/somavitabutanzania

Katika mazungumzo kati ya Howard na Gail wanagusia kuhusu maisha ya watu ambao hawana msimamo, na hapa Howard anapata nafasi ya kutoa hotuba yake kuhusu watu feki.

“Mzizi wa maovu siyo watu kuwa wabinafsi, bali watu kukosa kabisa nafsi. Mtu anayeiba na kudanganya, lakini mbele ya watu anajifanya ni mwenye heshima. Mtu anayejijua kabisa kwamba siyo mwaminifu lakini anawadanganya wengine wamwone ni mwaminifu. Watu wanaochukua sifa kwenye kazi ambazo hawajazifanya wao, anajijua hana uwezo lakini mbele ya wengine anajifanya ana uwezo mkubwa. Hawa ndiyo watu feki.

“Mtu ambaye lengo lake kuu ni kupata pesa, na hakuna ubaya wowote kwenye kutaka pesa. Lakini pale mtu anapotumia pesa kama njia ya kupata kitu kingine ndiyo ubaya na uovu unapoanzia. Pale mtu anapotafuta pesa kwa kusudi lake binafsi, kufanya uwekezaji kwenye kazi au biashara yake, kutengeneza, kujifunza, kusafiri na kuyafurahia maisha, ni sahihi kabisa. Lakini watu wanaoipa pesa nafasi ya kwanza wanaenda zaidi ya hapo, wanachotaka ni kujionesha kwa wengine, kujilinganisha na wengine na kuwafurahisha. Hawa ni watu feki. Watu hawa huwa hawana msimamo, hawafanyi jambo lolote kwa ajili yao, bali kwa ajili ya wengine. Mtu wa aina hii anaweza kukaa kwenye mhadhara ambao haelewi chochote, lakini hataki kuondoka kwa sababu anataka aonekane naye alikuwepo kwenye mhadhara huo.

“Watu feki hawajali kuhusu ukweli, fikra na kazi, bali wanajali kuhusu watu. Hawaulizi; je hii ni kweli? Wanauliza; je hiki ndicho wengine wanafikiri ni kweli? Hawahoji bali kurudia kile kinachofanywa na wengine. Hawafanyi chochote kwa ukamilifu, bali wanajionesha wanafanya. Hawatengenezi chochote kipya bali maonesho. Hawana wala kutumia uwezo, bali urafiki.

“Dunia inaendeshwa na wale wanaofikiri, wanafanya kazi na kuzalisha. Hawa wanaitwa wenye majivuno na kujijali wenyewe, lakini kupitia kujijali kwao ndiyo dunia inanufaika. Huwezi kufikiri kwa kutumia akili ya mwingine, huwezi kufanya kazi kupitia mikono ya mtu mwingine. Unaposimamisha uwezo wako wa kufikiri kwa uhuru unakuwa umesimamisha ufahamu wako. Na unaposimamisha ufahamu unakuwa umesimamisha maisha yako.

“Watu feki hawana uhalisia. Ukweli haupo ndani yao, bali kwa wengine. Ni watu wasio na nafsi, wenye maoni bila kufikiri, mwendo bila breki, madaraka bila majukumu.

“Watu feki wanatenda, lakini chanzo cha matendo yao ni kwa ajili ya wengine na siyo wao binafsi. Huwezi kufikiri nao kwa sababu hawana fikra, huwezi kuongea nao kwa sababu hawasikii. Unapojihusisha nao ni sawa na kuwa na kipofu anayekuja kwako kukuharibu bila ya kuwa na maana au kusudi.

“Angalia watu wanaokuzunguka, unashangaa kwa nini wanateseka, kwa nini wanatafuta furaha na hawaipati? Kama mtu angeacha anachofanya na kujiuliza kama amewahi kuwa na kusudi au hitaji binafsi, angepata jibu. Angeona kwamba matakwa yake, juhudi zake, ndoto zake na matarajio yake yanatokana na watu wengine na siyo yeye. Hateseki kwa ajili ya kupata anachotaka, bali kuonekana na wengine, ili wamkubali. Hapati furaha yoyote kwenye kile anachofanya na wala hafurahii anapofanikiwa katika kukifanya, kwa sababu siyo alichotaka yeye, bali amefanya kuwafurahisha wengine.

“Watu feki hawajawahi kujiambia; hiki ndicho ninachotaka, kwa sababu ninakihitaji na siyo kwa sababu kitawafurahisha wengine. Halafu anashangaa kwa nini hana furaha. Furaha ni kitu kinachoanzia ndani ya mtu mwenyewe na siyo nje yake.

Rafiki, hivyo ndivyo Howard Roark anavyotueleza kuhusu watu feki, kwa sifa hizo, unaona ni jinsi gani jamii imejaa watu feki na kwa nini maovu hayaishi kwenye jamii zetu. Ni kwa sababu karibu kila mtu anaishi kwa ajili ya mwingine, kwa kufanya vitu ambavyo havina maana kwao lakini wanataka kuonekana na wengine. Mwishowe wanakosa furaha kwenye kile wanachofanya, na hivyo inabidi waitafute kwa njia nyingine, kama ulevi, uzinzi, kuwatesa wengine na kadhalika, vitu ambavyo haviwapi furaha ya kudumu, zaidi ya kuharibu maisha yako.

Njia pekee ya kuwa halisi na kuwa na maisha mazuri kwako na kwa wengine, ni kuendesha maisha yako kwa namna yako mwenyewe. Tumia akili yako kufikiri, jua uwezo mkubwa uliopo ndani yako na uutumie na fanya kile ambacho ni sahihi na kinaleta matokeo unayoyataka, siyo kile ambacho wengine wanafanya au wanataka ufanye. Ukishaona unasema ndiyo kwenye jambo ambalo unataka sana kusema hapana, basi jua hapo umeanza kuishi maisha feki, na yatakugharimu.

SOMA; Wakishakulipa, Wanakupangia Cha Kufanya, Na Hapo Ndipo Unapoteza Uhuru Wako.

Kwenye kitabu cha The Fountainhead Ayn Rand ametufundisha jinsi tunavyoweza kuwa na msimamo na kuyaishi maisha yetu kupitia mhusika mkuu Howard Roark, ambaye amepitia magumu sana, lakini kwa kusimamia alichoamini aliweza kuwa na maisha bora na yenye mafanikio makubwa. Wakati mwenzake Peter Keating aliamua kufuata njia rahisi ya kufanya kile wengine wanamtaka afanye, akapata mafanikio ya haraka lakini hakuwa anayafurahia na mwisho akapata anguko kubwa.

Kitabu cha The Fountainhead ni kitabu ambacho kila anayetaka kuwa na mafanikio makubwa na maisha yenye uhuru anapaswa kukusoma. Karibu upate kitabu hiki pamoja na uchambuzi wake wa kina kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA. Fungua www.t.me/somavitabutanzania kisha bonyeza JOIN CHANNEL na hapo utapata uchambuzi wa kitabu hiki na vingine vingi.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania