“Fear defeats more people than any other one thing in the world.” —Ralph Waldo Emerson

Hebu fikiria ni mambo gani ungekuwa umefanya na hatua zipi umepiga mpaka sasa kama usingekuwa na hofu?
Biashara ambayo umekuwa unajiambia utaianza miaka mingi ungeshaianza tayari.
Vitu vipya ambavyo umekuwa unatamani kuvifanya kwa muda mrefu sasa ungeshavifanya.
Hatua kubwa ambazo umekuwa unataka kupiga kwenye maishs yako kila wakati, ungeshazipiga.
Na hata wale wanaokusumbua ambao unatamani sana kuachana nao, ungeshawaweka pembeni.

Lakini mengi unayopanga au unayotaka kufikia yanashindwa kwa sababu ya hofu.
Kwa kuwa unahitajika kufanya kitu ambacho hujawahi kufanya, na hivyo kuwa kwenye nafasi ya kupata matokeo ambayo hujawahi kuyapata, hofu ya kushindwa inakuwa kubwa.
Na kwa kuwa watu hatupendi kushindwa, basi tunaachana kabisa na kile tunachohofia.

Ndiyo maana hofu imekuwa kikwazo kikuu cha wengi kwenye maisha,
Ndiyo maana hofu imewaangusha wengi kuliko kitu kingine chochote hapa duniani.
Kwa sababu ni adui anayeanzia ndani, adui anayejua idhaifu wako ulipo na kuutumia vizuri.

Hatua ya kwanza muhimu unayopaswa kupiga kwenye maisha yako ni kuishinda hofu.
Siyo kuiondoa au kuikwepa, hilo liko nje ya uwezo wako,
Bali kukabiliana nayo na kuivuka, ambalo lipo ndani ya uwezo wako.
Hofu ni taarifa ambayo akili yako inakupa kwamba mambo hayapo kama ulivyozoea na huna uhakika wa kupata unachotaka.
Wanaoshindwa wanaamini taarifa hii na kutokuchukua hatua.
Wanaoshinda na kufanikiwa wanapokea taarifa hiyo na kujiuliza wanawezaje kupata wanachotaka licha ya kutokuwa na uhakika?

Hivyo hapo unaona wanaoshindwa na wanaoshinda wote wanakutana na hofu,
Wakati wanaoshindwa wanaisikiliza na kukubaliana nayo,
Wanaoshinda wanaisikiliza na kukabiliana nayo.
Je wewe umechagua upande upi, KUKUBALI au KUKABILI?
Maisha ni yako na chaguo ni lako,
Utakuwa pazuri sana ukichagua kuikabili hofu yako,
Kwa sababu ni mara chache sana mambo yataenda kama unavyohofia.
Mara nyingi mambo huenda vizuri, hasa pale unapojua ni nini unataka na kuwa tayari kuchukua hatua sahihi ili kupata unachotaka.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania