Kama hakuna kitu ambacho uko tayari kufa kuliko kukisaliti, basi pia huna kitu ambacho kinakusukuma kuwa na maisha bora hapa duniani.

Kwa kifupi, huna maisha, na kama huna maisha, tofauti yako wewe na wanyama wengine kama mbuzi ni ndogo sana.

Maana utazaliwa, utazurura zurura hapa duniani, kisha utakufa, utazikwa na utasahaulika.

Angalia watu wote ambao leo tunawajua japokuwa walishakufa miaka mingi iliyopita, ni kwa sababu walikuwa tayari kusimamia kitu fulani hata kama iligharimu maisha yao.

Nani asiyemjua Nelson Mandela, aliyefungwa jela miaka 27 kwa sababu alikataa katukatu kukubaliana na utawala wa kibaguzi nchini kwake? Na mwisho akaibuka mshindi.

Leo hii tunamjua Mwl Nyerere na kumwita baba wa taifa kwa sababu alikataa kabisa utawala wa kikoloni na kupigania kupata uhuru wa Tanganyika. Siyo kwamba Nyerere ndiye aliyekuwa wa kwanza kutaka tuwe na uhuru, ila alikuwa ni mmoja wa wale ambao walikuwa tayari kufa kuliko kukosa uhuru.

Mahtma Gandthi alikataa kukubaliana na utawala wa kikoloni, lakini pia hakuwa na jeshi la kupambana, hivyo aliamua kutumia nguvu aliyonayo, ambayo ilikuwa ni kuweka mgomo kwa wakoloni, kitu ambacho kilipelekea nchi yake ya India kupata uhuru. Alifungwa mara nyingi lakini hilo halikumrudisha nyuma.

Wavumbuzi wa teknolojia mbalimbali walipingwa sana, wengine mpaka walipelekwa hospitali kwa nguvu kwa kuaminika kwamba wana ugonjwa wa akili, lakini hawakukubali, na leo dunia ni bora sana kwa ajili yao.

Sasa turudi kwetu sisi, je ni kitu gani uko tayari kufa kuliko kukisaliti?

Jiulize swali hilo na kutafakari kwa kina, na kama hupati jibu la uhakika, maana yake mpaka leo hujawahi kuwa na maisha, umekuwa unawasindikiza tu wengine.

Kuchagua kile ambacho kitayaongoza maisha yako, kile ambacho uko tayari kufa kuliko kukisaliti, unapaswa kutengeneza kanuni za maadili ambazo utaziishi bila ya kuzivunja. Unapaswa kujiwekea viwango vya juu kwenye maisha yako na kila wakati kujisukuma kufikia viwango hivyo.

Unapaswa kukubali na kupenda maadili na viwango vyako kuliko unavyoyapenda maisha yenyewe, yaani kuwa tayari kuyapoteza maisha lakini siyo kusaliti maadili na viwango ulivyojiwekea.

Ili kuweza kujiwekea maadili na viwango hivi, jibu maswali haya matatu;

  1. Ni kipi muhimu zaidi kwako?
  2. Kitu gani upo tayari kufa kuliko kukisaliti?
  3. Ni jinsi gani nataka maisha yangu yawe?

Anza kuishi sasa, kwa kuwa na kile unachothamini sana na upo tayari kupoteza maisha kuliko kukisaliti. Maisha ya aina hii ndiyo yenye thamani kwako na kwa wengine pia.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha