“Every day I walk myself into a state of well-being and walk away from every illness; I have walked myself into my best thoughts, and I know of no thought so burdensome that one cannot walk away from it.” — Soren Kierkegaard

Umewahi kuianza siku yako ukiwa na furaha kubwa na mipango mizuri ambayo unakwenda kuitekeleza kwenye siku hiyo.
Halafu unapata taarifa fulani ambazo hukuzitegemea, na furaha nzima inaisha huku mipango uliyoweka unashindwa kuitekeleza?
Unajua nini kilichoharibu siku yako na furaha uliyokuwa nayo?
Siyo kile ulichosikia au kilichotokea, bali fikra unazoruhusu zitawale akilo yako.
Kwa sababu ulitegemea upate taarifa fulani na wewe ukaishia kupata taarifa nyingine, unaruhusu fikra nyingi hasi kutawala akili yako.
Linaweza kuwa jambo dogo ambalo siku kadhaa zijazo utakuwa umelisahau kabisa, lakini ukalifikiria na kulipa ukubwa ambao haustahili.

Sasa, moja ya wajibu mkubwa unaopaswa kujipa kwenye maisha yako, ni kulinda sana fikra zinazotawala akili yako.
Kwa sababu kama ambavyo tumekuwa tunajifunza, huwa tunakuwa kile tunachofikiri.
Matokeo unayoyapata sasa siyo ajali, bali ndiyo fikra zilizotawala akilo yako.
Hivyo kama unataka kupata matokeo tofauti, lazima kwanza uanze kufikiri tofauti.

Kila siku ondokana na fikra mbovu, fikra zisizo sahihi kwako na utakuwa na siku bora.
Kila siku futa kabisa fikra za magonjwa na afya mbovu, na utaondoa magonjwa mengi kwenye maisha yako na kukaribisha afya nzuri.
Kila siku ondoa fikra za kushindwa na utajiepusha na hali zinazopelekea kushinda huku ukiona ushindi kwenye kila jambo, hata kama matokeo tuliyopata siyo uliyokuwa unategemea.
Uzuri ni kwamba, hakuna fikra yoyote ile ambayo huwezi kuiondoa kwenye akili yako,
Hivyo usije kumlalamikia yeyote kuharibu maisha yako, ni wewe mwenyewe na fikra ambazo umekuwa unakumbatia kwenye akili yako.

Amani, furaha na utulivu wa maisha yetu unaanzia kwenye fikra zetu.
Unaweza kupita eneo lile lile, mchana ukapita kwa utulivu kabisa, lakini usiku ukapita kwa hofu kubwa, wakati hakuna chochote kilichobadilika kwenye eneo hilo isipokuwa mwanga, lakini fikra zako zinazalisha matokeo ya tofauti kabisa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania