Habari rafiki yangu mpendwa,

Jana tarehe 28/05/2020 ilikuwa tarehe ya kumbukizi ya kuzaliwa kwangu, ambapo siku kama hiyo miaka 32 iliyopita ndipo nilipozaliwa.

Jana sikuwa na mpango wowote kuhusu siku hiyo, na wala sikuwa nakumbuka, mpaka pale mke wangu aliponikumbusha kwa kunitakia heri. Baadaye mitandaoni nilipokea salamu za heri kutoka kwa marafiki zangu, huku wengine wakiweka moja ya picha zangu za zamani ambayo ilinifurahisha sana.

Picha ya zamani tukiwa shule ya msingi.

Kwa miaka mitano, tangu mwaka 2015, kila mwaka kwenye siku yangu ya kuzaliwa, nimekuwa nashirikisha makala maalumu ya salamu za siku yangu ya kuzaliwa, pamoja na kushirikisha mikakati mbalimbali ninayokwenda kuchukua kwenye mwaka mpya ninaokuwa nimeuanza.

Lakini kumbukizi ya mwaka huu 2020 sijafanya hivyo, sijaandaa wala kushirikisha makala ya salamu za siku yangu ya kuzaliwa na kushirikisha mipango mbalimbali ninayokwenda kuchukua kwenye mwaka wangu huo mpya.

Hii ni kwa sababu tarehe hii imenikuta katikati ya mpango mwingine ninaofanyia kazi sasa, mpango wa miaka kumi wa kujisukuma na kufanya makubwa mno. Katika mpango huu, nimeacha kuzitofautisha siku na badala yake kila siku naiishi kwa ukamilifu yake. Yaani kila siku kuna vitu ambavyo lazima nivifanye, bila ya kujali ni siku ya wiki, mwisho wa wiki au sikukuu. Siku hii imenikuta kwenye mpango wa muongo mmoja (miaka 10) wa kuweka kazi kila siku ili kuweza kufikia moja ya malengo mawili makubwa ambayo nimejiwekea kwenye maisha yangu.

Kila mwaka nimekuwa nakukumbusha malengo hayo mawili, na leo hii nikukumbushe tena malengo hayo makubwa mawili. Lengo kubwa la kwanza ni kuwa bilionea mpaka kufikia mwaka 2030 na lengo la pili ni kuwa raisi wa Tanzania mwaka 2040. Nimeyafafanua kwa kina malengo hayo mawili kwenye makala za nyuma na kwa nini nimeyachagua. Kwenye makala hii ya leo sitaingia ndani zaidi, unaweza kubonyeza kwenye kila lengo na kujifunza zaidi.

Sasa kwa nini naandika hapa leo kama sikuwa na mpango wa kuandika?

Rafiki yangu na mwanamafanikio mwenzetu kwenye familia ya KISIMA CHA MAARIFA, Dr Raymond Mgeni, ameniomba niseme neno kwa wale wanaofanya kazi hizi; Utabibu, Uandishi na Usomaji na uchambuzi wa vitabu. Nimemuahidi kufanya hivyo na hapa natimiza ahadi hiyo.

Nilimuahidi kusema neno kwenye vitu hivyo vitatu, na kuandaa makala kabisa kwa sababu ndiyo vitu vitatu pekee ambavyo nimejipa jukumu la kuvifanya kwa undani kwa miaka 10 ijayo.

Muongo wa kuelekea kwenye mabilioni.

Tarehe 01/01/2020 kwenye diary yangu, pamoja na mengine mengi, niliandika sentensi tatu muhimu sana kwenye maisha yangu.

Sentensi ya kwanza ilikuwa 2020’s DECADE TO BILLIONS, ikimaanisha miaka ya 2020, (2020 – 2030) ni muongo wa kwenda kufikia lengo langu la kuwa bilionea.

Sentensi ya pili ilikuwa SOMA.ANDIKA.TIBU. hii ikimaanisha vipaumbele vitatu tu ambavyo nitavifanyia kazi katika muongo huo wa kuelekea kwenye mabilioni. Kila mwaka nimekuwa nafanya tathmini ya mengi ninayofanya na kisha kupunguza na kubaki na machache. Kwenye muongo huu nimepunguza mengi na kubaki na hayo matatu.

Sentensi ya tatu ilikuwa CODE 487 #NoDayOff, hii ikimaanisha siku yangu ya kazi itakuwa inaanza saa kumi asubuhi (4am) na kumalizika saa mbili usiku (8pm) kwa siku 7 za wiki. Kila siku itakuwa siku ya kazi kwangu na sitakuwa na siku ya mapumziko.

Hivyo ndivyo ninavyoenda na mwaka huu na muongo huu mzima ambao tumeuanza. Najua safari hii haitakuwa rahisi, lakini naishi kwenye msingi wa kuikabili siku moja na kumalizana nayo, kisha kuianza tena siku nyingine, na siku siyo nyingi utasikia muongo huu umeisha na kama nitafuata msingi huo, najua nitaweza kufanya makubwa sana.

Mpango wa kuandika vitabu 100 ndani ya miaka kumi.

Kwa miaka miwili, nimekuwa napata wazo la kuandika vitabu vingi zaidi kama njia ya kurahisisha maarifa kwa wengi. Nimekua nahamasisha sana watu wasome vitabu, lakini wengi wamekuwa wanasingizia hawapati vitabu vya kusoma, kutokana na lugha na vikwazo vingine.

Kwa miaka hiyo miwili, kuna wazo ambalo limekuwa linanijia mara kwa mara, kwa nini nisiandike kitabu kimoja kila mwezi? Mwanzo nilikuwa nakwepa wazo hilo, nikijiambia ni jukumu kubwa na linahitaji maandalizi makubwa na kuhusisha watu wengi, kitu ambacho ni rahisi kukwama.

Kitu kikubwa ambacho kilikuwa kinanikwamisha ni usambazaji. Kama vitakuwa vitabu vya kuchapa, kuchapa kitabu kipya kila mwezi ni jukumu kubwa, ambalo linahitaji kuwa na mfumo bora sana wa usambazaji wa vitabu hivyo, kitu ambacho bado kinakosekana kwa mazingira yetu.

Na ikiwa ni kuvitoa kama nakala tete, njia ambayo nimekuwa natumia kwa vitabu hivyo ni mtu kulipia, kisha kutuma email na kutumiwa vitabu. Sasa kwa kutoa kitabu kipya kila mwezi, haitakuwa shughuli rahisi hiyo. Hivyo nikawa najiambia hili ni wazo zuri, lakini nitafanyia kazi baadaye.

Lakini wazo hili halikuacha kunijia, kadiri ninavyoendelea kujifunza kupitia usomaji wa vitabu, ndivyo ninavyopata maarifa na maudhui mengi na ndiyo ninavyoona fursa ya kushirikisha maudhui hayo kwa wengine kwa mfumo wa vitabu.

Katika kuanza muongo huu ambapo uandishi ni moja ya vipaumbele vikubwa, nilianza kufanya utafiti ninawezaje kutekeleza wazo hilo la kutoa kitabu kipya kila mwezi. Na hapo ndipo nilipopata wazo, niwe na jukwaa ambalo nitaweka vitabu hivyo kwa mfumo wa nakala tete, na mtu ataweza kulipia na kusoma moja kwa moja kwenye jukwaa hilo, bila ya mlolongo mwingine.

Kwa kuwa na jukwaa hilo, itarahisisha usambazaji, na hivyo kazi pekee itabaki kwenye uandishi. Sasa kwa kuwa uandishi ni kitu ninachofanya kila siku, haitakuwa kazi ngumu tena.

Nashukuru baada ya kuongea na wabunifu mbalimbali, nimeweza kupata ambao wanaweza kufanya kazi hiyo ya kutengeneza jukwaa litakalobeba vitabu hivyo na kwa sasa mchakato wa kutengeneza jukwaa hilo unaendelea, likiwa tayari nitawashirikisha.

Hivyo basi rafiki, mpango wangu ni huu, kwa miaka 10, nitaandika vitabu 100 ambavyo vitakuwa vya nakala tete. Kila mwezi nitatoa angalau kitabu kimoja. Ni jukumu kubwa ambalo nimejipa, na nitajisukuma kuhakikisha nalifikia. Na ndiyo maana nimepunguza vitu vingi, ili kubaki na vichache ambavyo nitaweka juhudi kubwa ili niweze kutoa matokeo makubwa pia.

Neno kwa wanaofanya Utabibu.

Wakati narudi kumalizia masomo yangu ya udaktari mwaka 2014 baada ya kusimama kwa miaka mitatu, nilijiambia naenda kumaliza kile nilichoanza, lakini nilijiambia sitatibu, kwa kuwa nilishakuwa nimeshachagua kufanya vitu vingine.

Lakini mwaka 2017 nilisoma kuhusu maisha ya Dr Shigeaki Hinohara, daktari wa Japan aliyefariki akiwa na miaka 105. Kilichonishangaza kuhusu daktari huyo na kikabadili kabisa mtazamo wangu ni kwamba, alikuwa akiendelea kutibu wagonjwa mpaka anakufa. Na hata wakati ana kufa, bado alikuwa na miadi (appoitments) na wagonjwa wake kwa miaka miwili mbele.

Kingine nilichoifunza kwa daktari huyu na kunibadili kabisa ni kwamba katika maisha yake, aliandika vitabu 75. Moja ya kauli zake ni kwamba mtu hapaswi kustaafu, badala yake anapaswa kufanya kile anachopenda kila siku, na hivyo ataweza kuishi miaka mingi.

Hivyo neno langu kwa wale waliopo kwenye fani ya Utabibu ni hili, TIBU MAISHA YAKO YOTE.

Moja ya faida za fani ya utabibu ni kwamba unaweza kuifanya kazi hiyo mpaka siku unakufa. Kadiri unavyokwenda na hasa ukiwa mtu wa kujifunza, ndivyo unavyozidi kuwa bora zaidi. Uzoefu wako unakuwa mkubwa na unaweza kuwasaidia wengi.

Hivyo kwa kuwa ukifanya kazi hiyo kwa kuajiriwa utalazimika kustaafu pale umri unapokwenda, ni vyema ukaanza kujipanga mapema na kufungua kituo chako cha kutoa tiba, hata kama ni kidogo na ukaendelea kufanya kazi yako mpaka siku unakufa.

Kwa kufanya hivyo, siyo tu utawasaidia wengi, lakini pia utajisaidia wewe mwenyewe, kwa sababu kadiri unavyoendelea kufanya kazi, ndivyo unavyoishi miaka mingi zaidi. Ukistaafu na miaka 60, kwa nafasi kubwa ndani ya miaka 10 inayofuata utakuwa umekufa kama huna unachofanya. Lakini kama ukiendelea kufanya kazi, utakuwa imara kwa muda mrefu.

Hii pia inafaa kwa fani zote, uwe ni mwalimu, mwanasheria, mhasibu na wengineo, tengeneza mfumo ambao utakuwezesha kufanya kazi maisha yako yote. Kama umeanza kwa kuajiriwa pembeni fanyia kazi mpango wa kufungua kitu chako mwenyewe kitakachokufanya uendelee na kazi hata utakapostaafu kwenye ajira. Kama ni mwalimu panga kuanzisha shule au chuo, kama mhasibu anzisha kampuni ya kutoa huduma za uhasibu, kadhalika kwenye taaluma nyingine.

Usikubali ujuzi na uzoefu unaoendelea kuupata kwenye taaluma yako uje upotee kwa sababu sheria inakutaka ustaafu. Badala yake tengeneza mapema mfumo utakaokupa nafasi ya kuendelea kufanya kazi yako mpaka siku unakufa, na hilo litakuwezesha kuishi miaka mingi.

Neno kwa wasomaji na wachambuzi wa vitabu.

Nimekuwa napenda kusoma vitabu tangu zamani, kumbukumbu kubwa niliyonayo kwenye usomaji wa vitabu ni nikiwa shule ya msingi, kati ya darasa la nne au la tano, niliweka mpango wa kusoma biblia kuanzia mwanzo mpaka mwisho, na hiyo ni kwa sababu ndiyo kitabu pekee kilichokuwa kinapatikana nyumbani. Japo sikuimaliza kwa kipindi kile, lakini nakumbuka nilienda kitabu kwa kitabu mpaka kufika zaburi na mithali.

Baadaye, kadiri nilivyokuwa nakutana na vitabu, hasa vya shule, nilikuwa napendelea kusoma zaidi hivyo kuliko notisi, na hili ndiyo lilikuwa linanisaidia kufaulu sana.

Mwaka 2012 ndiyo nilianza rasmi kusoma vitabu vya maendeleo binafsi na mwaka 2014 niliweka lengo la kusoma vitabu 500 ndani ya miaka 5, yaani vitabu 2 kila wiki ambayo inaleta vitabu 100 kila mwaka na vitabu 500 kwa miaka mitano. Mwishoni mwa mwaka 2019 nilifanya tathmini ya vitabu vyote nilivyosoma na kupata ni vitabu 655.

Neno langu kwenye usomaji na uchambuzi wa vitabu ni hili, SOMA KILA SIKU, SHIRIKISHA ULIYOJIFUNZA.

Kila siku unalisha mwili wako chakula, basi pia lisha akili yako chakula ambacho ni usomaji. Kila siku unasafisha mwili wako kwa kuoga, basi pia ogesha akili yako kwa kuipa maarifa sahihi. Usikubali siku ipite hujasoma kitabu, kama ambavyo hukubali siku ipite hujala kabisa.

Lakini huwezi kukumbuka kila unachosoma kwenye vitabu, hasa unaposoma vitabu vingi. Hivyo jenga tabia ya kushirikisha wengine yale uliyojifunza kwenye kitabu ulichosoma. Tumia lugha rahisi ya kuhakikisha mtu yeyote anakuelewa, hata kama kitabu ni kigumu kiasi gani. Kwa njia hiyo, siyo tu utajifunza mengi, lakini pia utakuwa na ushawishi kwa wengi, ambao watakuamini kupitia yale unayowashirikisha na kuwa tayari kushirikiana na wewe kwenye mengine mengi.

Niongeze kidogo hapo kwenye usomaji, jiwekee utaratibu wa kusoma vitabu ambavyo hupendi kuvisoma au hukubaliani navyo. Kwenye usomaji kuna tabia ya kusoma vile tu unavyopendelea wewe, na hivyo kujikuta hujifunzi vitu vipya.

Kwa mfano, kwenye usomaji wangu wa miaka ya nyuma, nimekuwa nasoma vitabu visivyo vya kutunga (non fiction) na kujiambia sina muda wa kusoma vitu ambavyo watu wametunga (fiction) badala yake nataka kusoma vitu ambavyo ni halisi, ambavyo watu wamefanyia kazi au wametafiti na kupata majibu sahihi.

Lakini mwaka huu 2020 nilijiambia nitachagua kusoma vitabu kutoka mtandao wa MOST RECOMMENDED BOOKS, ambao unaorodhesha vitabu ambavyo wale waliofanikiwa wamekuwa wanashauri wengine wavisome. Nilijiambia nitasoma kila kitabu kilichopendekezwa, iwe na kubaliana nacho au la, maana kama kuna watu waliofanikiwa wanakipendekeza, kuna kitu cha kujifunza.

Hapo nikaanza kukutana na riwaya, na ya kwanza ilikuwa kitabu cha Atlas Shrugged cha Ayn Rand, kitabu kina kurasa zaidi ya elfu moja. Nilianza kujishawishi siwezi kukisoma, kwanza ni riwaya pili ni kirefu mno. Lakini nikajikumbusha msimamo niliojipa kwamba nitasoma na kuchambua kila kitabu kilichoorodheshwa kama sijafanya hivyo kwa siku za nyuma. Basi nikaanza kusoma, kwa kweli nimejifunza mengi mno, mno, mno kupitia riwaya ile. Nikajifunza kumbe riwaya zinaweza kutumika kufikisha ujumbe kwa njia rahisi zaidi.

Nikaendelea kukutana na riwaya nyingine, Fountainhead cha mwandishi huyo huyo, nacho kizuri mno. Pia nimesoma riwaya ya kisayansi inayoitwa DUNE, na ninachoweza kusema ni kama hujasoma riwaya hizo tatu, unajinyima kuziona pande mbalimbali za maisha, ambazo tunakabiliana nazo kila siku.

Lakini pia usomaji wa riwaya hizi, umeibua hamasa ndani yangu ya kufikisha ujumbe kwa njia ya riwaya pia. Hivyo naona kuna fursa nzuri ya kuelimisha kupitia uandishi wa riwaya.

Usisome vitabu unavyopenda au kukubaliana navyo tu, bali soma vitabu usivyopenda au kukubaliana navyo, na utajifunza mengi.

Neno kwa waandishi.

ANDIKA KILA SIKU. Hilo ndiyo neno ninaloweza kuwapa wale wote ambao wanafanya uandishi. Usisubiri mpaka upate hamasa ndiyo uandike, bali weka ratiba yako ya uandishi na andika kila siku. Ili uweze kuandika kila siku, lazima pia uwe unajifunza kila siku. Hivyo kusoma na kuandika vinakwenda pamoja, huwezi kuandika kama husomi.

Nina mengi sana ya kushirikisha kwenye uandishi, kwa uzoefu wangu binafsi na makosa ambayo nimekuwa nafanya na nawaona wengine wakifanya, lakini makala ya leo imeshakuwa ndefu. Hivyo hapa nitayataja, na siku nyingine nitaingia ndani kuyachambua zaidi.

1. Andika kile ambacho kinatoka ndani ya moyo wako, kile ambacho unasukumwa kukiandika, na siyo kuandika kuwafurahisha watu.

2. Tengeneza sauti yako ya uandishi, unaweza kuwa na waandishi au mwandishi unayemkubali au kujifunza kwake, ukajikuta unaandika kama yeye, huwezi kufika mbali kiuandishi, tafuta mtindo wako mwenyewe wa uandishi, ambao utakutofautisha.

3. Kazi ya uandishi kuna wakati ina upweke mkubwa, inakuhitaji uwe na muda mwingi peke yako kuliko kazi wanazofanya wengine, lazima uwe tayari kwenye hilo.

4. Unastahili na unapaswa kulipwa kupitia uandishi wako, usiache kuwataka watu walipie pale wanapotaka zaidi kutoka kwako.

5. Chagua hadhira utakayoiandikia na cha kutaka kila mtu awe msomaji wako, kama unalenga kila mtu huna unayemlenga. Jua kabisa unamwandikia mtu wa aina gani, na hapo uandishi wako utagusa maisha ya mtu.

6. Unaweza kuandika makala 100 nzuri kabisa, na watu wachache mno wakakushukuru au kukupa moyo kwa unachofanya. Lakini ukaandika makala au kutuma ujumbe mmoja ambapo umekosea na utashangaa kila mtu anakukosoa na kukupinga. Hata watu ambao hawajawahi kukupa moyo kwa makala nzuri 100 ulizoandika, watakuwa wa kwanza kukuhukumu kwa makala moja mbaya uliyoandika. Elewa hilo na usikubali likuumize.

7. Sehemu kubwa ya wale wanaokukosoa kwenye uandishi ni wivu tu. Wanatamani wangeandika, ila hawawezi kukaa chini na kuandika, wakiona wewe unaandika wanatafuta makosa ya kuonesha kwamba wewe siyo bora kuliko wao.

8. Epuka sana kujisifia kila wakati kupitia uandishi wako, watu wana wivu, kadiri unavyojisifia ndivyo wanavyotafuta makosa ya kukurudisha nyuma.

9. Usisubiri ukamilifu, andika na toa, iwe ni makala au kitabu au chochote, una nafasi ya kuboresha zaidi baadaye, kwa kutoa toleo la pili na mengine mengi.

10. Fanya uandishi kuwa kitu cha kwanza kwenye siku yako, andika kabla hujaendelea na ratiba nyingine za siku yako. Ukishindwa kutenga muda wa asubuhi na kuandika, ni vigumu sana kupata muda siku yako ikishaanza, na pia siku inavyoenda unachoka, na akili ikishachoka, utajipa kila sababu kwa nini usiandike.

KARIBU TWENDE PAMOJA.

Rafiki yangu mpendwa, nimalize makala hii kwa kukukaribisha twende pamoja kwenye safari hii. Kama unataka kufanya makubwa kwenye muongo huu wa 2020 – 2030 basi njoo tusafiri pamoja.

Kama nilivyokushirikisha, nimepunguza mambo mengi sana, na hivyo njia pekee ambapo tunaweza kwenda pamoja ni kwa kuwa mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA. Hapa ndipo sehemu pekee tunayoweza kukutana mtandaoni, hakuna sehemu nyingine yoyote unaweza kunipata, isipokuwa kwenye kundi la wasap la KISIMA CHA MAARIFA.

Hivyo kama bado hujawa mwanachama, chukua hatua sasa, tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap kwenda namba 0717396253 na utapata maelekezo ya jinsi ya kuwa mwanachama.

Kama unahitaji chochote kutoka kwangu, nje ya makala na vitabu ninavyoandika, iwe ni ushauri au kujifunza zaidi, basi hakikisha kwanza umekuwa kwenye KISIMA CHA MAARIFA, hiyo ndiyo sehemu pekee ambapo naweza kukufuatilia kwa karibu.

Karibu sana twende pamoja kwenye safari hii, haitakuwa rahisi, tutakutana na changamoto nyingi, lakini mwisho tutashinda, kwa kishindo kikubwa, kama tu hatutakata tamaa na kuishia njiani.

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail  

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania