Wahunzi huwa wanaunda vitu kwa chuma wakati chuma ni cha moto, ukisubiri chuma kipoe huwezi kuunda kile unachotaka.
Kadhalika ndiyo maisha yetu yalivyo, kuna wakati ambapo huwa tunapata hamasa kubwa sana, lakini tusipoitumia, huwa tunaipoteza.
Hivyo unapopata hamasa ya juu, hakikisha kuna hatua unachukua wakati hamasa hiyo iko juu, hatua ambayo itakulazimu uendelee kuchukua hatua zaidi.
Lakini kama utapata hamasa na kujiambia wacha usubiri mpaka uwe tayari, muda mchache baadaye hamasa hiyo inakuwa imeshuka na huwezi tena kuchukua hatua.
Kuna fursa nyingi unazokutana nazo kila siku ambazo zinachochea hamasa ndani yako, usizipoteze.
Mfano umesoma kitu kikakupa hamasa, au umemsikia mtu anaongea akakupa hamasa, au kuna kitu umeona na kikakuhamasisha sana. Usiache hamasa hiyo ikapoa, badala yake itumie wakati bado ni ya moto.
Anza na hatua yoyote ile, ambayo itakugharimu kama hutaendelea kuchukua hatua zaidi. Unaweza kumwahidi mtu kwamba utafanya kitu fulani na usipofanya umpe adhabu atakayokupa.
Ukweli ni kwamba, ukiwa na hamasa unaweza kutamani kufanya makubwa, na kuona inawezekana, lakini hamasa hiyo inaposhuka huwa unaona ulikuwa unajidanganya, kwani huwezi kufanya makubwa uliyodhani unaweza.
Sasa hakikisha unatumia nafasi hiyo vizuri, wakati hamasa iko juu na ndiyo nafasi nzuri kwako kujidanganya, tumia nafasi hiyo kujifunga ili uendelee kufanya. Hata kama hamasa itaisha na ukaona huwezi, kile ulichojifunga nacho kitakusukuma uendelee kufanya, na hutabaki kama ulivyokuwa awali.
Kikwazo cha kwanza kwenye mafanikio yetu, kinachotuzuia tusifanye makubwa ni akili zetu za kawaida, yaani ile akili inayofikiri. Lakini ndani yetu tuna akili isiyo ya kawaida, yenye nguvu na isiyoshindwa chochote, lakini hatuipi nafasi. Wakati wa hamasa ndiyo akili hiyo inapata nafasi na kukuonesha unaweza kufanya makubwa.
Hivyo ukweli ni kwamba yale unayoona unaweza kuyafanya unapokuwa na hamasa, siyo unajidanganya, bali ndiyo ukweli ambao umekuwa unaukwepa muda mrefu. Ndiyo maana ninakutaka ukishapata ukweli huo, usiuache uponyoke, badala yake utumie vizuri. Jiwekee kifungo ambacho kitakulazimisha kufanya na usipofanya utaingia gharama kubwa.
Mfano umeona eneo ambalo unaweza kufanya biashara ambayo ulikuwa unaifikiria muda mrefu, likakuhamasisha sana, cha kufanya lipia eneo hilo mara moja, hata kama bado hujajua nini kitaendelea. Kwa sababu ukilipia, kodi inaanza kuhesabiwa na hivyo itajisukuma uanze. Lakini usipolipia, utaendelea kujiambia unasubiri na hutachukua hatua. Na huenda siku utakayotaka kuja kuchukua hatua, ukakuta eneo lenyewe halipo tena.
Tumia vizuri fursa ya hamasa unayoipata, itumie kujiweka kwenye kifungo ambacho kitakulazimisha ufanye. Na kumbuka, kile unachoona kinawezekana unapokuwa na hamasa, ndiyo ukweli uliojificha ndani yako, usione unajidanganya pale hamasa inapoisha.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante sana kwa makala hii kuna sindano nimeipata hapa kocha wangu
LikeLike
Karibu Hendry
LikeLike
Kumbe hamasa ndio inaipa nafasi akili yetu ya ndani kufanya kazi kwa uhuru….nimegundua kitu hapa.
Asante sana Kocha.
LikeLike
Karibu.
LikeLike