Njia ya uhakika ya mkato ya wewe kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako ni kuacha kukimbizana na njia za mkato.

Hii ni kwa sababu njia za mkato ndiyo njia ndefu kuliko zote kwenye safari ya mafanikio.

Muda na nguvu unazoweka kwenye njia ya mkato ni umechagua kuzipoteza moja kwa moja, haziwezi kurudi tena kwako.

Na ubaya zaidi ni kwamba njia za mkato huwa haziishi, hivyo moja ikishindwa, utaambiwa kuna nyingine, na nyingine na nyingine.

Karibu kila mtu huwa anapoteza miaka mpaka kumi kwenye maisha yake akiwa hakuna hatua yoyote anayopiga bali kujaribu njia za mkato.

Ni mpaka pale kila njia anayokuwa amejaribu inashindwa na muda unakuwa umeenda ndiyo anaamua akae chini na kufuata njia sahihi.

Watu wengi kati ya miaka 20/25 mpaka miaka 30/35 ni miaka ambayo huwa wanaipoteza kwa kujaribu kila aina ya njia ya mkato. Akisikia hiki kinalipa yupo, akisikia kile ni habari ya mjini hakosekani, akisikia kuna fursa mpya ni wa kwanza.

Wengi katika umri huo huwa hawajaamua wanataka nini, hivyo kujikuta wanahangaika na kila kitu, wakiamini kwamba ipo siri ambayo hawajaijua, siri ambayo ni njia ya mkato kwa mafanikio yao.

Ni kweli siri inakuwepo, ila hawaijui mpaka pale wanapomaliza kila aina ya njia ya mkato. Kwa kuwa siri hiyo ni hakuna njia ya mkato. Lakini wakiambiwa hawasikii wala kuamini, hivyo wanatafuta wenyewe mpaka wanapogundua njia hiyo haipo ndiyo wanakuwa wameijua siri kwamba hakuna njia wanayoitafuta.

Haijalishi uko kwenye umri gani sasa, ni wakati wa kuacha kukimbizana na kila kitu na kuchagua nini unachotaka. Na ukishachagua unachotaka, fanya kilicho sahihi ili kukipata.

Acha kukimbizana na njia za mkato, hakuna njia ya mkato inayofanya kazi, kama ingekuwa ni sahihi na inafanya kazi, isingekuwa njia ya mkato, ingekuwa njia kuu. Inaitwa ya mkato kwa sababu haifanyi kazi, hivyo epuka njia za aina hiyo.

Fedha, kazi, biashara, mahusiano, elimu na mengineyo, kadiri unavyohangaika na njia za mkato, ndivyo unavyojichelewesha kupaya unachotaka. Epuka miaka ambayo ungeipoteza kwa kujaribu njia nyingi za mkato na chagua njia sahihi na anza kuifanyia kazi mapema. Wakati wenzako wanazinduka usingizini kwamba njia za mkato hazifanyi kazi, njia sahihi unayotumia wewe itakuwa imeanza kukulipa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha