Tulipozaliwa hatukuwa tunajua kitu chochote kwenye maisha, zaidi ya kulia na kunyonya. Mengine yote tunayojua sasa, tumekuwa tunajifunza.
Na kwa kuwa hatujui, katika kujifunza kwetu tumekuwa tunakosea mara kwa mara na makosa hayo ndiyo yanatufanya kuwa bora zaidi.
Hukusimama na kuanza kutembea moja kwa moja, bali ulianguka kabla hujajua jinsi ya kutembea vizuri. Kadhalika uliyajua madhara ya mto baada ya kuushika moto na kuungua.
Yale tuliyojifunza na kuyaelewa kwenye maisha, ni matokeo ya makosa mbalimbali ambayo tumeyafanya. Kwa kujifunza kutoka kwenye makosa hayo, tulijua kile ambacho ni sahihi kufanya.
Lakini tunapokuwa watu wazima, tunaondoka kwenye msingi huo muhimu wa kujifunza. Lengo letu linakuwa ni kutokukosea. Kwa kukazana kutimiza lengo hilo, tunaishia kutokufanya chochote kikubwa na kutojifunza chochote kipya.
Hali hii haiji tu yenyewe, bali ni matokeo ya miaka mingi ya kufundishwa kwenye jamii na hata shuleni, kwamba kukosea ni dhambi kubwa. Ukikosea unapata adhabu kali. Ulipofika kwenye kazi pia nako kukosea ni uzembe mkubwa ambao unaweza kukugharimu kazi yako.
Hivyo umejifunza kuwa mtu wa kuepuka makosa na ili usikosee unafanya yale tu unayojua au ambayo umezoea kufanya. Nje ya hayo hakuna kipya unachofanya kwa sababu huna uhakika na matokeo na hutaki kukosea.
Rafiki, kosa kubwa kwenye maisha siyo kufanya makosa, bali kutokujifunza kupitia makosa unayofanya. Na kosa kubwa zaidi ni kutokufanya makosa, kwa sababu unakuwa hujifunzi chochote kipya.
Kwa chochote unachofanya kwenye maisha yako, kile ambacho unataka kufanikiwa sana, kila wakati jifunze na kujaribu vitu vipya, utakosea katika vingi, lakini utajifunza na kuwa bora sana.
Sayansi inapiga hatua kila siku kwa sababu kwenye sayansi hakuna kukosea, bali kuna kujaribu na kujifunza. Mtu akifanya utafiti fulani na majibu anayopata yakawa tofauti na aliyotegemea, huyo hajakosea, bali ameongeza maarifa kwenye sekta aliyofanyia utafiti. Mwingine atakayekuja kufanya utafiti, hatarudia yale ambayo mwenzake alifanya na hakupata majibu sahihi. Au wakati mwingine anaanzia hapo na kujaribu kingine kipya.
Maisha yako ni mwendelezo wa majaribio na kujifunza na siyo kupatia au kukosea. Lengo lako lisiwe kutokukosea, bali liwe kujifunza na kuwa bora zaidi. Huwezi kujifunza na kuwa bora kama haupo tayari kufanya vitu vipya. Na huwezi kufanya vitu vipya, kama haupo tayari kukosea.
Chagua upande sahihi na ishi kwa misingi ya upande huo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Katika kukosea ndipo napijifunza na kufanya kwa usahihi zaid,kuliko kuogopa kukosea,asante kocha
LikeLike
Vizuri.
LikeLike