“It’s not enough to understand; you’ve got to do something.” — Sandra Day O’Connor

Umesoma kitabu na kuielewa dhana fulani vizuri, usiishie hapo, fanya kitu kwa dhana hiyo uliyoielewa.
Umemsikiliza mtu akifundisha kitu fulani na kuelewa vizuri, usiishie hapo, nenda kachukue hatua mara moja kwa kile ulichoelewa.
Unaweza kuelewa vizuri sana chochote unachojifunza,
Lakini kama hakuna hatua unayochukua kwa ulichoelewa, haina maana kwenye maisha yako.

Kwa zama za mafuriko ya maarifa na taarifa tunazoishi sasa,
Nguvu haipo kwenye maarifa unayopata,
Bali nguvu iko kwenye hatua unazochukua kwa maarifa unayopata.
Changamoto ya mfumo rasmi wa elimu ni mwanafunzi kukusanya maarifa kwa muda mrefu, bila ya kuchukua hatua.
Anapokuja kufika wakati wa kuchukua hatua anakuwa ameshasahau au aliyokuwa anajua yameshapitwa na wakati.
Ndiyo maana elimu ya maendeleo yako binafsi ni muhimu sana,
Kwa sababu unajifunza kile ambacho una uhitaji nacho.

Lakini usijifunze na kufurahia kuelewa,
Bali kwa kila unachojifunza, ondoka na hatua unazokwenda kuchukua kwenye maisha yako.
Hiyo ndiyo namna pekee ya kunufaika na maarifa unayopata.
Kuelewa unayojifunza ni kuzuri, kuchukua hatua kwa kile ulichoelewa ndiyo bora zaidi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania