Kama una shilingi elfu kumi, na ukaipoteza kwa kununua kitu ambacho hakina umuhimu wowote kwako, labda umekunywa pombe au kununua nguo ambayo huna uhitaji nayo sana.
Utajiambia ni elfu kumi tu nimepoteza, hakuna shida kubwa.
Siyo kweli, umepoteza zaidi ya shilingi elfu kumi, tena ukikaa chini na kupiga mahesabu, utajikuta umepoteza mamilioni ya fedha.
Chukua mfano kama ungetumia hiyo elfu kumi kununua kitabu ambacho kitakufundisha mambo mazuri kuhusu mafanikio, ukakisoma na kuyafanyia kazi, elfu 10 hiyo ingekulipa kiasi gani?
Fikiria elfu 10 hiyo ungeiwekeza sehemu ambayo hutaigusa kwa miaka mingi ijayo, sehemu inayozalisha faida hata kama ni kidogo, elfu kumi hiyo itakulipa kiasi gani?
Na hapo usisahau, sisi binadamu huwa hatufanyi kitu mara moja, ukipoteza elfu kumi leo, haitakuwa mwisho wako, utaendelea kuzipoteza nyingi, inakuwa ni tabia. Lakini hiyo elfu kumi ukiitumia vizuri, itakuwa ndiyo tabia yako pia.
Hivyo kwa kila fedha kabla hujaitumia, jiulize kama unaipoteza ni kiasi gani halisi unachopoteza kwa kuangalia fursa nyingi unazojinyima kwa sasa na baadaye.
Kwenye muda pia mambo ni hayo hayo, tena ni mabaya zaidi. Unapopoteza muda, unapoteza zaidi ya ule unaohesabu.
Chukua mfano umepoteza saa moja kwenye siku yako, ukihangaika na habari au mitandao ya kijamii isiyokuwa na mchango wowote kwa mafanikio yako. Ukijiambia umepoteza saa moja pekee unajidanganya, umepoteza sehemu kubwa ya maisha yako.
Hebu fikiria kama saa hiyo moja ungeiwekeza kujifunza kitu kipya, ambacho kitakufanya uwe bora zaidi kwenye kazi yako au biashara yako. Ungekuja kupata manufaa makubwa kiasi gani kwa kitu kimoja ambacho umekijua na utakifanyia kazi kila siku?
Hebu fikiria saa hiyo moja ungekaa na mwenza wako au yeyote wa muhimu kwako, kwa saa moja nzima bila ya kuwa na usumbufu wowote ule, ni kwa kiasi gani utaweza kuboresha mahusiano yako na wengine?
Na hapo bado hujahesabia tabia, kama tulivyoona, huwa hatufanyi kitu mara moja, hivyo ukipoteza saa moja leo kwa kuzurura mitandaoni, na kesho pia utafanya hivyo, na siku nyingine, mwisho inakuwa ndiyo maisha yako ya kila siku, haiwi tena kupoteza muda, bali inakuwa ni kujua yanayoendelea, japokuwa hayana mchango wowote kwenye mafanikio yako.
Anza sasa kuangalia thamani halisi ya kitu kabla hujakipoteza, usiangalie leo pekee, bali angalia siku nyingi zijazo. Usiliangalie tukio moja pekee, bali angalia tabia unayoijenga kwa kitu kimoja unachofanya.
Ukiweza kukokotoa thamani halisi ya unachopoteza, utakuwa makini kwa kila unachofanya.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Ningekuwa na mtazamo huu wa kuangalia miaka mingi ijayo kwenye chochote ninachofanya au kupoteza ningeepuka mengi kwenye maisha yangu.
LikeLike
Sasa unao,
Usirudie makosa.
LikeLike