Katika mapambano ya kuutafuta utajiri, watu wengi wamekuwa wanaangalia upande wa fedha tu, lakini kusahau eneo muhimu sana katika utajiri wa kweli, ambalo ni uhuru.

Utajiri wa kweli siyo tu kuwa na fedha nyingi utakavyo, bali pia kuwa huru kadiri utakavyo kwenye maisha yako.

Watu wengi wamepambana sana kupata fedha nyingi, lakini katika kufanya hivyo wamepoteza uhuru wao kabisa.

Mfano ni mtu ambaye anakuwa amepambana sana kupanda vyeo kwenye kazi yake aliyoajiriwa, anapanda vyeo na kufika ngazi za juu ambapo analipwa vizuri sana. Lakini hawezi kuacha kazi hiyo maana ndiyo njia kuu ya kuingiza kipato. Na kwa kuwa anaitegemea sana, basi hawezi kuwa na msimamo pale mambo yanapokuwa siyo sahihi. Kwa namna hii mtu anaweza kuwa na kipato kikubwa sana, lakini hayupo huru, analazimika kufanya kile anachoambiwa kufanya hata kama hakubaliani nacho.

Mfano mwingine ni mtu anayeanzisha biashara, ambapo yeye ndiye msimamizi wa kila kitu. Anafanya kazi usiku na mchana na kweli biashara inakua, na kipato kinakuwa kikubwa sana. Lakini kadiri biashara inavyokuwa kubwa, ndivyo inavyomhitaji zaidi. Hivyo licha ya kuwa na kipato kikubwa, hayupo huru na maisha yake, hawezi kuchagua aendesheje siku yake, kwa sababu biashara inamtegemea na kutokuwepo kwake kutapelekea biashara ife na akose fedha alizokuwa nazo.

Tuziangalie sifa chache za utajiri wa kweli;

Utajiri wa kweli ni pale unapoweza kusema HAPANA kama unataka kusema hapana, na hulazimiki kusema NDIYO ili kumridhisha yeyote.

Utajiri wa kweli ni pale ambapo hulazimiki kwenda kwenye vikao na mikutano mbalimbali kama hutaki kufanya hivyo.

Utajiri wa kweli ni pale unapochagua kuzungukwa na watu unaowapenda na kuwakubali na hulazimiki kuzungukwa na watu ambao inabidi tu uwavumilie.

Utajiri wa kweli ni kuishi maisha yako kwa viwango na vigezo vyako na siyo kushindana na wengine kwenye vitu vya nje, kwamba una nini.

Utajiri wa kweli ni kuwa huru kufanya chochote utakacho, popote utakapo na kwa wakati wowote unaochagua wewe.

Kama unavyoona, utajiri wa kweli unakupa wewe uhuru kamili wa maisha yako, lakini unahitaji mkakati mkubwa na mzuri unaofanyiwa kazi ili kukupa wewe uhuru kweli.

Kwa sababu wengi ambao wameweza kufikia ngazi za juu na kuingiza kipato kikubwa, wanakuwa wamefungwa kwenye kile wanachofanya, hivyo hawapo huru kuishi maisha wanayotaka wao, kuna wakati wanalazimika kusema NDIYO hata kama ndani yao wanajisikia kusema HAPANA. Na pia kuna nyakati nyingi wanalazimika kufanya kazi na watu wasiowapenda wala kuwakubali, kuwa kwenye mikutano ambayo wanajua kabisa wanapoteza muda, lakini hawana namna.

Katika harakati zako za kujijengea utajiri wa kweli, mara zote angalia uhuru wako. Kabla hujafanya chochote, jiulize kama kinakuongezea uhuru au kinakunyima uhuru, sasa na hata baadaye. Na weka vipaumbele kwenye yale mambo ambayo yanakufanya kuwa huru zaidi, hata kama yanapelekea uingize kipato kidogo kuliko mengine ambayo yatakupa kipato kikubwa lakini yatakunyima uhuru.

Usiwe mtu wa kuangalia leo tu, angalia kesho, angalia miaka 10, 20 mpaka 50 ijayo na pima kila unachofanya leo kinaitengenezaje kesho yako.

Ukifikiria kwa msimamo huu wa uhuru, utaweza kufanya makubwa huku pia ukitunza uhuru wako na hapo ndipo utakapoufikia utajiri wa kweli.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha