“There is in our soul something that, if we see it as it is and give it the proper attention, will always give us great pleasure; this something is the moral disposition or quality which was given to us at our creation.” —IMMANUEL KANT

Ndani ya kila mmoja wetu kuna kitu ambacho mtu akikitambua na kukipa umakini, kinampa matokeo makubwa na raha pia.
Kitu hicho ni kusudi la mtu kuwa hapa duniani, kile anachoweza kukifanya kwa ubora zaidi na maadili ambayo anayo.
Kwa bahati mbaya sana, hakuna anayezaliwa akiwa na maelekezo ya nini kipo ndani yake,
Na hakuna mtu yeyote wa nje anayeweza kumwambia mtu ni nini kipo ndani yake.
Unaweza kukitambua kilicho ndani yako, kwa kutafakari na kujitathmini wewe mwenyewe.
Na hilo linahitaji muda na uvumilivu, linahitaji kujaribu vitu vingi na kushindwa.

Tunaishi kwenye jamii ambayo inakazana kutufanya tuwe kama wengine,
Jamii ambayo inatuzuia tusijue kusudi letu wala uwezo mkubwa tulionao.
Maana jamii inajua tukiyajua hayo, tutafanya makubwa sana, tutakuwa huru na hakuna atakayeweza kututawala.
Kwa kuwa jamii inataka kututawala, inahakikisha hatuitambui wala kuitumia nguvu kubwa iliyo ndani yako.

Kuwa mjanja na tambua mitego mbalimbali inayowekwa na jamii ili kukuzuia kutambua kilichopo ndani yako.
Kila ubachoona kinafanywa na kukubalika na wengi, jua hicho ndiyo sumu ya kuwazuia watu wasitambue kusudi na nguvu zao.
Mfumo wa elimu unaomfanya kila mtu akazane kuwashinda wengine,
Mfumo wa imani unaosisitiza maisha yetu si hapa wala leo,
Mfumo wa siasa unaoaminisha watu kwamba kiongozi fulani au chama fulani ndiyo suluhisho la matatizo yetu,
Mfumo wa biashara ambao unatushawishi kununua vitu fulani, hasa vilevi ili tujisikie vizuri,
Mfumo wa habari ambao kila wakati unatuletea habari mpasuko na kuona kama tumefikia mwisho wa dunia,
Mfumo wa teknolojia ambao umetuletea teknolojia mpya ambazo zimetugeuza kuwa kama misukule, muda wote tukihangaika na yasiyo na manufaa yoyote kwetu, kama mitandao ya kijamii.

Mifumo hii inaungana pamoja kuhakikisha hatuwi huru, kuhakikisha hatutambui kusudi na nguvu kubwa iliyopo ndani yetu na hivyo kuendelea kuwa chini ya utawala wa wengine.
Ni wakati sasa wa kushika hatamu ya maisha yako,
Kutambua ndani yako kuna kusudi na uwezo mkubwa,
Na hivyo kuchukua hatua ya kujua na kuishi kusudi na uwezo huo.
Utakapoanza kufanya hivyo, jamii haitakuachia kirahisi,
Jua utakuwa umeanzisha vita na mifumo hiyo inayotaka kukutawala,
Na mifumo hiyo ina mbinu nyingi za kuhakikisha hakuna anayetawaliwa anachomoka,
Hivyo hakikisha unajitoa kweli kupambana ili uweze kuwa huru.

Uhuru kamili wa maisha yako unaupata pale unapojua kusudi na nguvu kubwa iliyopo ndani yako na kuanza kuviishi vitu hivyo.
Uhuru huu huwa haupewi kirahisi, bali mtu anauchukua mwenyewe kwa kuwa tayari kuupigania.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania