Kwenye maisha ya mafanikio, unamjua nani ni muhimu kama ilivyo unajua nini. Mtandao wa wale unaowajua na wanaokujua una mchango mkubwa sana kwenye mafanikio yako.

Wengi wamekuwa wanahangaika kukuza mitandao yao kwa njia ambazo huwa naita ni za kujipendekeza. Njia za kuhangaika ili uonekane na wewe upo, lakini mtandao unaotengeneza huwa siyo imara, kwa sababu unakuwa umejengwa kwenye maonesho na siyo uhalisia.

Kuhangaika ili tu watu wajue na wewe upo itawafanya wakujue kweli, lakini kama hakuna wanachoweza kutegemea kutoka kwako kukujua kwao hakutakusaidia chochote wewe.

Hapa kuna njia bora na rahisi unazoweza kutumia kukuza mtandao wako.

Moja; kuwa wa msaada, kwa kila unachofanya, hakikisha unawasaidia wengine, unaongeza thamani kwenye maisha yao na unayafanya maisha yao kuwa bora kuliko yalivyo sasa. Fanya kitu hiki kimoja na kila mtu atakuwa anakuzungumzia kitu ambacho kitakuza sana mtandao wako.

Mbili; jiamini kupitia ushindi unaotengeneza kwenye maisha yako. Kama wewe mwenyewe hujiamini, hakuna anayeweza kukuamini. Njia bora kwako kujiamini ni kutengeneza ushindi mdogo mdogo kwenye maisha yako mara kwa mara.

Tatu; kuwa mnyenyekevu, usijione wewe unajua sana kuliko wengine, au ni bora kuliko wengine. Jua kila mtu ni muhimu, jua una cha kujifunza kwa kila mtu. Waoneshe watu umuhimu wao, kuwa mtu wa kusikiliza na kujifunza na kila mtu atapenda kuwa karibu na wewe.

Nne; wapende wengine, upendo wa kweli kutoka ndani yako na siyo upendo wa kutaka kupata kitu. Upendo ni jawabu kwa mambo mengi, na pia upendo una nguvu ya kuwavuta watu sahihi kwako.

Fanyia kazi mambo haya ambayo yote yapo ndani ya uwezo wako na utaweza kutengeneza mtandao mkubwa utakaokusaidia kufanikiwa sana kwenye maisha yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha