Watu wenye hofu huwa wanapenda kuzungukwa na watu wenye hofu.
Ungeweza kufikiri kwamba watu hao wangependa kuzungukwa na wasio na hofu, wanaojiamini ili nao washinde hofu zao.
Lakini hivyo sivyo ilivyo, watu wenye hofu wanapenda kuzungukwa na wengine wenye hofu ili kuhalalisha hofu zao. Wanachotaka kuamini ni kwamba hofu walizonazo ni sahihi. Hivyo anapokuwepo mtu ambaye hana hofu, anafanya hofu zao zionekane hazina msingi.
Hivyo kuhakikisha watu hao hawayumbishwi kwenye hofu zao, huwa wanahakikisha wanazisambaza kwa wengine. Wanapokutana na mtu ambaye hana hofu, wanahakikisha wanaingiza hofu ndani yake ili naye ahofie kama wao, na hapo waridhike kwamba hofu zao ni sahihi.
Sasa kwa kuwa sehemu kubwa ya wale wanaokuzunguka wamejawa na hofu, unapaswa kuwaepuka kama kweli unataka kuishinda hofu uliyonayo na uweze kuchukua hatua. Wajue wale wanaokuzunguka na hofu walizonazo, kisha epuka hali inayowapeleka kwenye kujadili mambo yanayohusu hofu hizo. Maana watahakikisha wanakupa hofu walizonazo pia.
Epuka kabisa vyombo vya habari, maana biashara kuu ya vyombo hivyo ni kusambaza hofu. Vinaweka uzito zaidi kwenye habari mbaya na hasi, zinazoibua hofu kwa wengi ili vipate wafuasi wengi na hapo kuwauza kwa njia ya matangazo. Hakuna kikubwa unachojifunza kwenye habari zaidi ya kujazwa hofu.
Kaa mbali kabisa na mitandao ya kijamii, hii imekuwa njia rahisi ya wenye hofu kusambaza hofu zao. Kila ambaye ana hofu, amekuwa anatumia mitandao hiyo kuisambaza kwa wengine. Kuwa kwenye mitandao hiyo ni kujiweka kwenye mazingira yatakayokujaza hofu kila wakati.
Hatua ya kwanza ya kukabiliana na hofu ni kuepuka wale wenye hofu, ambao huwa wanazisambaza hofu zao kwa makusudi ili wapate watu wa kuwa nao kwenye hali ya hofu.
Hatua ya pili ni kufanya kile unachohofia, huku ukiwa na picha chanya ya matokeo mazuri unayokwenda kupata kwenye kitu hicho. Haikusaidii chochote kufikiria matokeo mabaya muda wote, hata kama huna uhakika, wewe tengeneza picha ya matokeo bora unayotaka kufanya kisha iangalie hiyo muda wote. Kwa kuangalia picha hiyo na kuchukua hatua, hofu haitapata nafasi ya kukuzuia. Hapo ni kama umejiondoa kabisa kwenye mazingira yanayochochea hofu zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante sana kocha, kupitia kitabu cha Dune, The prophet Cha 1-3,maisha na Mambo Paul,jessica,chan na wengineo wengi waliyoyapitia ,na hasa juu ya kuishinda na kuikabili hofu, hakika ni MAISHA ambayo unaweza kujifunza na kuchukua hatua katika maisha ya sasa na ukawez kupiga hatua zaidi za kimafanikio.
LikeLike
Kweli kabisa Beatus.
LikeLike