Moja ya kikwazo kikubwa kwa wengi kufanikiwa ni kutokufanya maamuzi ya kuchagua eneo ambalo watalibobea na kufanya vizuri.
Wengi hupenda kuwa na machaguo mengi wakiamini kufanya hivyo ni kuwa huru na kutokufungwa kwenye eneo moja.
Lakini kwenye dunia tunayoishi sasa, dunia yenye ushindani mkali, huwezi kufanikiwa kama unafanya kila kitu.
Utafanikiwa kama utachagua eneo ambalo utalibobea na kufanya vizuri.
Lakini kubobea pekee haitoshi, unahitaji pia kuhudumu, kuwapa watu huduma bora sana kiasi kwamba wanakuamini na kukusikiliza.
Kuchagua eneo la kubobea ni mtihani kwa sababu ukishachagua eneo, inabidi ufanye vizuri sana kwenye eneo hilo. Huna tena nafasi ya kufanya kawaida, huna nafasi ya kujitetea kwamba umetingwa na mambo mengi ndiyo maana hujakamilisha. Unachagua eneo na kufanya vizuri kwenye eneo hilo.
Kuhudumu unahitaji kuwajali sana wale unaowalenga, kujiweka kwenye viatu vyao na kufanya kilicho sahihi. Unakazana kuongeza thamani kwa wengine, kwa kwenda hatua ya ziada na kuwapa zaidi ya walivyokuwa wanatarajia kupata.
Kazi inahitajika, kwenye kufikia ubobezi unaotaka na kuwahudumia wale unaowalenga. Kuchagua eneo moja au machache hakukufanyi upunguze kazi, bali kunakufanya uweke kazi zaidi kwenye maeneo ambayo ni muhimu.
Uzuri wa kubobea ni kwamba, juhudi zote unazoweka hazipotei, kadiri unavyobobea ndiyo thamani yako inakua zaidi. Ndiyo unavyoweza kutatua matatizo makubwa yanayowakabili watu na wakawa tayari kukulipa zaidi.
Acha kuhangaika na kila kitu, chagua eneo lako la kuhudumu, bobea kwenye eneo hilo, jiwekee viwango vya juu, toa thamani kubwa kwa wengine na matokeo yatakuwa wazi kwako, utapiga hatua zaidi ya hapo ulipo sasa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,